CURRENT NEWS

Wednesday, April 15, 2015

COMNETA WAMPONGEZA PROF. MBWETE


DSC_0348
Mwenyekiti wa mtandao wa Redio Jamii nchini (COMNETA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio ya Jamii ya Wilayani Karagwe ya FADECO FM, Bw.Joseph Sekiku akizungumza katika hafla fupi ya kumuaga Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) ambaye amemaliza muda wake, Prof. Tolly Mbwete (katikati) iliyoandaliwa na Mtandao wa Redio za Jamii nchini (COMNETA). Kushoto ni Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu.
DSC_0359
Katibu wa mtandao wa Redio Jamii nchini (COMNETA), Riziki Leisuya akisoma risala fupi wakati wa hafla ya kumuaga Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Prof. Tolly Mbwete.
Na Mwandishi wetu
MTANDAO wa Radio za Kijamii nchini Tanzania (COMNETA) na Chuo Kikuu Huria (OUT) kwa umoja wao zimepongeza mchango mkubwa wa aliyekuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Tolly Mbwete kwa jitihada zake za kuziunganisha redio jamii na chuo kuhakikisha taarifa zinawafikia walio wengi hasa vijijini.
Katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa OUT hivi karibuni mtandao wa COMNETA umesema jitihada za Profesa Mbwete kuziunganisha taasisi hizo mbili zimefanikishwa kwa kiasi kikubwa kufikisha taarifa za kozi mbalimbali zinazoendesha chuoni na kwa bei nafuu kwa Watanzania wengi ambao umesaidia kukifahamu na hatimae kujiunga na chuo.
Akisoma risala fupi iliyotayarishwa na COMNETA, Katibu wa mtandao huo Riziki Leisuya alisema kwamba makubaliano na mashirikiano kati ya Comneta na OUT yaliyowezeshwa na Profesa Mbwete yamezaa matunda mengi baina ya pande hizo mbili kiasi cha kulishawishi Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu ,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kukubali kujenga studio ya redio katika chuo hicho ili kurahisisha mawasiliano kwa kutayarisha vipindi lakini pia itatumika na wanafunzi wanaochukua taaluma ya uandishi kufanya mazoezi kwa vitendo kuboresha mafunzo yao.
“Comneta kupitia redio zake imefanikiwa kupeleka habari wilayani na vijijini kwa kukitangaza chuo kwa watu wasiojiweza jambo ambalo limesababisha ongezeko la idadi ya wanafunzi chuoni hapo kutokana na unafuu wa gharama” iliongeza risala hiyo iliyosomwa na Riziki.
Profesa Mbwete ambaye muda wake wa utumishi chuoni hapo umefikia kikomo kwa sasa amechaguliwa kuwa Mkuu wa Vyuo Vikuu vya Kikanda (Pan African Universities-PAU) na Umoja wa Nchi huru za Afrika kuanzia mwezi Januari mwaka 2015.
Akiwashukuru na kuwaaga wana-Comneta ambao walihudhuria ulingo wa siku tatu kutathminimradi wa demokrasia na Amani (DEP) Profesa Mbwete alisema amefarijika na ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo mbili ambao umekuwa na mafanikio ya kipekee kwa umma wa Tanzania na kuahidi kumkabidhi atakayechukua nafasi yake kuendeleza ushirikiano huo na kumshauri ofisi ya COMNETA iendelee kwa mkataba wa ushirikiano kwa miaka mitatu na kila mwaka kuufanyika mapitio na mrejesho.
Naye Balozi Christopher Liundi ambaye ni mshauri wa Unesco akimzungumzia Profesa Mbwete alisema kwamba Profesa Mbwete anastahili pongezi kutokana na jinsi alivyoimarisha Chuo Kikuu Huria na kuimarisha ushirikiano kati ya Chuo hicho na Comneta kwa kutoa ofisi ambayo mtandao wa redio za jamii unaitumia kwa kutekeleza majukumu yake kama jitihada za kutoa uwezo kwa mtandao huo.
“Profesa Mbwete alikuwa mstari wa mbele kupanua chuo na namshukuru sana kwa kauli yake ya kuipa COMNETA miaka mingine mitatu kutumia ofisi iliyotolewa na chuo chini ya usimamizi wake. Ninaamini kwamba huko aendako atapeperusha bendera ya Tanzania na ataiwakilisha vizuri kwenye PAU, nina matarajio makubwa sana kutoka kwake,’ alisema Balozi Christopher Liundi.
DSC_0386
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) ambaye amemaliza muda wake, Prof. Tolly Mbwete akipokea risala iliyosomwa na Katibu wa mtandao wa Redio Jamii nchini (COMNETA), Riziki Leisuya wakati wa hafla fupi ya kumuaga iliyoandaliwa na WanaCOMNETA.
DSC_0373
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania ambaye amemaliza muda wake, Prof. Tolly Mbwete (wa pili kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mhariri wa Sibuka FM, Anita Balingilaki kwa niaba ya Wanamtandao wa Redio Jamii nchini Tanzania (COMNETA) kama ishara ya kumuaga rasmi wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na wanamtandao huo ya kumtaki kheri katika majukumu mapya anayoenda kufanya nchini Addis Ababa. Kushoto ni Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu na Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa mtandao wa Redio Jamii nchini (COMNETA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio ya Jamii ya Wilayani Karagwe ya FADECO FM, Bw.Joseph Sekiku akifutiwa na Mshauri wa UNESCO, Balozi mstaafu Mh. Christopher Liundi.
DSC_0430
Mshauri wa UNESCO, Balozi mstaafu Mh. Christopher Liundi akitoa wasifu wa Prof. Tolly Mbwete kwenye hafla hiyo fupi.
DSC_0436
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) ambaye amemaliza muda wake, Prof. Tolly Mbwete katika picha ya pamoja na wakufunzi na washiriki wa warsha ya siku tatu kutathmini mradi wa demokrasia na Amani (DEP) yenye lengo la kuimarisha ushiriki wa redio za jamii nchini kuelekea uchaguzi 2015 na kura ya maoni kwa wanamtandao wa Redio Jamii nchini (COMNETA) iliyoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) ambayo imemalizika mwishoni mwa juma katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Huria (OUT).
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania