CURRENT NEWS

Wednesday, July 27, 2016

DC BAGAMOYO AJITUA MZIGO WA MADAWATI ,AOKOA MAMILIONI YA FEDHA

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ,alhaj Majid Mwanga ,wa kwanza kushoto ,wa pili afisa mahusiano wa kampuni ya MMI Abubakar Mlawa na wa tatu ni mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo na wengine wakiangalia madawati 6,946 yaliyokabidhiwa na mkuu wa wilaya huyo juzi wilayani Bagamoyo. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
Mmoja wa wadau waliochangia madawati wilayani Bagamoyo, afisa uhusiano wa kampuni ya MMI ,Abubakar Mlawa ,akimkabidhi mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, madawati 1,200 yaliyochangiwa na kampuni hiyo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
MKUU wa wilaya ya Bagamoyo,alhaj Majid Mwanga amekabidhi madawati 6,943 yenye thamani ya sh.Mil 557.6 kwa mkuu wa mkoa wa Pwani ,ambayo yatagawanywa katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.

Alhaj Mwanga amesema madawati hayo yametolewa na wahisani mbalimbali hivyo kuokoa kiasi hicho ambacho kingetumika kutolewa na serikali ya wilaya hiyo.

Akikabidhi madawati kwa mkuu wa mkoa wa Pwani ,Mhandis Evarist Ndikilo,alisema amefanikiwa kuokoa fedha hizo baada ya wilaya yake kuzungumza na wahisani na wadau ambao walikubali kuchangia fedha zote.

Alhaj Mwanga aliwataja waliochangia kuwa ni pamoja na kampuni ya MMI, kampuni ya IPP,  madiwani,  wakuu wa Idara,  TANAPA, TASAF na wadau wengine wa ndani na nje ya wilaya hiyo .

Alieleza kuwa kati ya madawati 6,943 ,madawati 2,036  ni kwa ajili ya shule za sekondari ambayo yamegharimu kiasi cha sh.115.9.

Aidha alisema,  kwa upande  shule wa shule za msingi ni madawati  4,907 yametengenezwa kwa gharama ya sh.mil.441,630,000 .

Alhaj Mwanga alisema, baada ya kukamilisha zoezi hilo sasa wanajipanga kutatua  tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa ulipo katika baadhi ya shule  wilayani hapo.

"Nawashukuru wahisani wote ,na natumia nafasi hii jamii ijenge tabia ya kushirikina katika kuchangia masuala ya kijamii na elimu ili kuinua maendeleo ya wilaya yetu pasipo kujali itikadi zetu" alisema alhaj Mwanga.

Akipokea madawati hayo ,mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Ndikilo alimpongeza mkuu huyo wa wilaya na watendaji wake kwa kukamilisha zoezi hilo.

Mhandisi Ndikilo alieleza kuwa katika mkoa huo  zoezi la madawati kwa upande wa shule za sekondari limekamilika na lipo kwenye hatua za mwisho.

Alisema  madawati ya shule za msingi zoezi bado linaendelea ambalo linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.

Mhandisi Ndikilo aliwataka walimu wakuu wa shule kuzingatia utunzaji wa madawati hayo na kuwaasa maafisa tarafa ,watendaji wa kijiji na kata kusimamia vizuri madawati hayo.
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania