CURRENT NEWS

Saturday, July 30, 2016

DC MTATURU AZINDUA UCHANGIAJI WA DAMU SALAMA


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akichangia damu kwa ajili ya wananchi wanaofariki kwa kukosa huduma ya damu katika hospitali mbalimbali nchini


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akihojiwa kuhusu umri na mambo kadha wa kadha ili kufanyika utambuzi kama damu yake inatosha kiasi cha kutoa kwa ajili ya wengine, Mtaturu amechangia Unit 450 ya damu yaani chupa moja.


Na Mathias Canal, Singida

Wananchi wametakiwa kufanya kazi kwa kushiriana na viongozi na watumishi wengine wa afya ili kuleta mabadiliko na kuhakikisha kuwa maisha ya wananchi yanakuwa bora zaidi.

Mwito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe. Miraji Jumanne Mtaturuwakati wa uzinduzi wa uchangiaji wa damu salama, Mfuko wa Afya (CHF) na Daftari la ufuatiliaji akinamama wajawazito Wilayani humo.

Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo Mtaturu amesema kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali  suala la vifo vya kina mama wajawazito, watoto wadogo pamoja na upungufu wa dawa katika vituo vya afya bado ni changamoto.

Amesema Takwimu zinaonyesha kuwa katika Wilaya ya Ikungi vifo vya akina mama vinaongezeka mwaka hadi mwaka ikiwa mwaka 2013 ilikadiriwa kupoteza akinamama 79 kwa kila vizazi hai 100,000 na hesabu hiyo imeongezeka na kufikia 94/100,000 kwa mwaka 2014 na 201/100,000 kwa mwaka 2015.

“Hali hii haikubaliki ndugu zangu wa Kata ya Minyughe na Wilaya ya Ikungi kwa ujumla  mbaya zaidi matatizo yanayopelekea vifo hivyo yanatokana na sababu ambazo zinaweza kuzuilika, kwa mfano, ukosefu wa damu katika vituo vyetu vya afya na kutozingatia vidokezo vya hatari tunavyoelekezwa wakati wa mahudhurio ya kliniki” Alisema Mtaturu.

Sanjari na hayo Mtaturu alisema kuwa  matatizo makubwa yanayopelekea vifo vya akina mama wajawazito ni kutokuzingatia vidokezo hatari kama wataalamu wanavyoelekeza  kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, hali ambayo inapelekea akinamama wanaotakiwa kujifungua Hospitalini wanalazimika kujifungulia nyumbani au kwenye Zahanati ambapo pakitokea dharura wanashidwa kupata msaada.

Kutokana na hali hiyo Mtaturu amesema kuwa ili kuhakikisha wajawazito wote wanaenda Kliniki na kufuata wanayoelekezwa Wilaya ya Ikungi imeanzisha daftari la ufuatiliaji ambapo jamii itasaidia kuwakumbusha wajawazito kwenda Kliniki na kuchukua hatua pale ambapo hawatafanya hivyo.

“Lengo kuu ni kuhakikisha akina mama wajawazito wote wanahudhuria kliniki mapema  na kuhudhuria angalau mara nne ili kupunguza vifo ambavyo vinaweza kuzuilika Sasa ninawataka wenyeviti  na watendaji wote wa vijiji kufanya ufuatiliaji wa daftari hilo kuona kama akina mama wajawazito  wanahudhuria kama wanavyotakiwa na kunipatia taarifa ya utekelezaji wake kila mwezi.”Alisema Mtaturu

Akizungumzia suala la ukosefu wa damu salama katika vituo vya afya Mtaturu amesema kuwa Wilaya ina mahitaji ya wastani wa Unit 1000  kwa Mwaka na kwa kuzingatia hilo umewekwa  mkakati wa kuhamasisha jamii angalau iweze kutoa damu mara moja kila mwezi kwa kila Kata.
“Kwa Mwananchi au mtu yeyote ambaye atakuwa amepata tatizo la upungufu wa damu na kuhitaji kuongezewa damu katika hospitali zetu hatahitajika kulipia gharama yeyote inayohusu kuongezewa damu kwa sababu tutakuwa tumejiwekea akiba ya damu yetu wenyewe” Alisema Mtaturu.

Aidha Mtaturu ameongeza kuwa  mabadiliko katika sekta ya Afya yanayoendelea kutekelezwa katika utoaji huduma yana lengo la kuinua kiwango cha ubora wa huduma za afya kwa wananchi na kuongeza kiwango cha uwajibikaji kwa wasimamizi na watoaji wa huduma hizo na ili kufanikisha lengo hilo, madaraka, majukumu na kazi, rasilimali zaidi za Afya zinahitajika kwa kuitaka jamii kuchangia katika mifuko ya afya ya jamii (CHF).

Alisema Mfuko wa afya ya jamii (CHF) kwa Kaya moja itatakiwa kuchangia Tsh. 10,000/= na atatibiwa Baba, Mama na Watoto wanne kwa mwaka mzima na kuongeza kuwa mfuko huo hautaimarika kama hautakuwepo usimamizi imara na unaoambatana na uadilifu.

“Miongoni mwa manufaa ya mabadiliko ya sekta ya afya ni pamoja na jamii yenyewe kuwa na madaraka zaidi ya kuamua kuhusu huduma za afya zinazotolewa na kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma hizo kwa kuwakilishwa katika bodi ya afya ya wilaya na kamati za huduma za afya za vituo” Alisema Mtaturu

Katika kuhitimisha uzinduzi huo Mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi Mtaturu Jumanne Mtaturu alizindua rasmi matumizi ya Daftari la ufuatiliaji kwa kuwakabidhi madaftari hayo wenyeviti wa vitongoji wa kata hiyo pamoja na kuanza zoezi la utoaji damu kwa wilaya nzima ya Ikungi.

Jumla ya Watu waliochangia Damu ni 36 ambapo Wastani wa damu iliyotolewa kwa mtu mmoja ni Unit 450. Hivyo tukizidisha 36 × 450 tunapata Unit 16,200 ambazo ni sawa na lita 16.2 za Damu zilizopatikana mara baada ya uzinduzi.

DC Mtaturu amehamasisha wananchi Wilayani Ikungi kujiunga na mfuko wa Afya ya jamii (CHF) kwani itasaidia kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa Wilaya ya Ikungi ambayo ina Kaya 53823 huku wananchi waliojiunga na mfuko huo wakiwa ni asilimia 24% tu
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania