CURRENT NEWS

Sunday, July 31, 2016

KOKA:AWAASA WALIMU WAKUU NA WATENDAJI KUTUNZA MADAWATI YA MISAADA Inbox x

MBUNGE wa jimbo la Mji wa Kibaha,Silvestry Koka wa kushoto akikabidhi madawati 537 yenye thamani ya zaidi ya mil. 37 yaliyotolewa na serikali ikiwa ni mgao wa wabunge nchini kwenye sehemu ya posho zao,kwa afisa elimu wa halmashauri ya Mji huo ,Maajabu Mkanyemka aliyemwakilisha mkurugenzi wa halmashauri hiyo Jennifer Omolo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
MBUNGE wa jimbo la Mji wa Kibaha,Silvestry Koka akikabidhi madawati 537 yenye thamani ya zaidi ya mil. 37 yaliyotolewa na serikali ikiwa ni mgao wa wabunge nchini kwenye sehemu ya posho zao ,kwa mtendaji wa kata ya Mailmoja ,Thadeo Mtae baada ya kukabidhi kwa uongozi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MBUNGE wa jimbo la Mji wa Kibaha ,Silvestry Koka ,amewataka walimu wakuu wa shule za msingi na watendaji wa mitaa na kata katika halmashauri ya Mji huo, kusimamia na kuhakikisha wanayatunza madawati mapya yanayotolewa na wadau mbalimbali ili kuondoa tatizo la ubaha wa madawati mashuleni.
Amesema mwalimu mkuu ama mtendaji ambae atazembea kusimamia suala hilo basi atawajibishwa .
Koka aliyasema hayo ,wakati akikabidhi madawati 537 yenye thamani ya zaidi ya mil. 37 yaliyotolewa na serikali ikiwa ni mgao wa wabunge nchini kwenye sehemu ya posho zao .
Alieleza kuwa serikali haitakuwa tayari kuona madawati yanayotolewa na wahisani,wadau na yale yaliyotengenezwa na wadau hayafuatiliwi wala kupewa matunzo.
“Ni wajibu wa kila mtendaji,walimu na wanafunzi wenyewe kuwa wasimamizi kutokana na fedha zilizotumika ni kodi za wananchi hivyo lazima zilindwe kwa faida ya watoto hao “alisema Koka.
Aidha Koka alisema awali wanafunzi walikuwa wanapata shida na kero wakati wa kusoma ambapo wengine walikuwa wakikaa chini na kuchafuka kwa vumbi na kuandikia chini hivyo kushindwa kupata elimu yao kwenye mazingira yasiyo bora.
Alisema serikali ya awamu ya tano chini ya rais John Magufuli ,iliona iweke mkakati madhubuti wa kuchangia madawati na viti na meza katika shule za msingi na sekondari ili kuondoa kero ya upungufu uliokuwepo miaka ya nyuma.
Koka alisema kuwa ni jambo la lazima na sio hiari kwa walimu wakuu kuwa moja ya wakaguzi na wasimamizi wakuu wa madawati hayo ili hata kama yatakuwa yameharibika kidogo yatengenezwe na si kuyaacha hadi yaharibike .
Nae mwakilisha wa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha Jennifer Omolo,afisa elimu wa halmashauri ya Mji huo,Maajabu Mkanyemka alisema kabla ya agizo la rais kulikuwa na mahitaji ya madawati 9,162.
Alieleza hadi kufikia June 30 walikuwa tayari wametengeneza na kukarabati madawati 6,979 hivyo kwasasa wana upungufu wa 2,183.
Maajabu alisema hadi sasa madawati yaliyopatikana  ni 2,500 kati ya mapungufu ya 2,183 huku 572 yakiwa yanatengenezwa na mara yatakapokamilika kutakuwa na ziada ya madawati 312 hivyo kutarajia tatizo la madawati kubaki historia mjini hapo.
Alisema katika upande wa shule za sekondari mahitaji ya meza yalikuwa 7,032 vilivyopo ni 6,041 na kubakia na upungufu wa meza 991 huku viti walivyokarabati na kutengeza ni viti 6,099 kukiwa na upungufu wa viti 933 hadi sasa.

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania