CURRENT NEWS

Thursday, July 28, 2016

SAYONA FRUITS LTD YAMPIGA TAFU RIDHIWANI KIKWETE

Mbunge wa jimbo la  Chalinze Ridhiwani Kikwete akikabidhiwa  viti na meza kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari tano za jimbo hilo  ,kutoka kwa mwakilishi wa kampuni ya sayona  fruits ltd ,Abubakary Mlawa huko katika shule ya sekondari ya Lugoba .Kampuni hiyo imetoa viti 724 na meza 724 vyote vikiwa na gharama ya mil.80.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ,amepokea msaada wa viti 724  na meza 724 kwa ajili ya wanafunzi wa  shule ya sekondari tano jimboni humo.
Msaada huo umetolewa na kampuni ya Sayona fruits ltd ambapo viti na meza hizo zimegharimu kiasi cha sh.mil80.
Aidha mdau huyo wa maendeleo ametoa madawati 1,200 yaliyogharimu sh.mil 90 ,katika shule za msingi wilayani Bagamoyo ambapo kati ya madawati hayo 600 ni ya jimbo la Chalinze na 600 ni jimbo la Bagamoyo.
Akipokea msaada huo,kutoka kwa mwakilishi wa kampuni ya sayona fruits na kampuni mama ya MMI ,Abubakary Mlawa,mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani alisema walimfuata mkurugenzi mtendaji  wa kampuni hizo Shubash Patel ambae amewatatulia tatizo lao.
Alieleza kuwa ufadhili huo ni mkubwa kwani awali halmashauri hiyo ilikuwa ikikabiliwa na mapungufu ya meza na viti 1,500 katika shule za sekondari lakini kwasa itabaki upungufu wa meza na viti 120.
Ridhiwani alisema wanaelekeza nguvu zao kuhakikisha wanamaliza tatizo hilo ifikapo mwezi octoba mwaka huu.
Alisema jitihada hizo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli na ya mikakati yake ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya elimu hivyo halmashauri ya Chalinze inafanya kwa vitendo kuunga mkono mikakati hiyo.
Hata hivyo Ridhiwani alisema kuwa amejipanga na halmashauri ya Mji wa Chalinze kuendelea kutatua tatizo la meza,viti na madawati ili hali kumaliza hali hiyo na kubaki historia.
Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akiwa  na mwakilishi wa kampuni ya sayona fruits ltd Abubakary Mlawa kwenye moja ya meza na kiti ambavyo alikabidhiwa kutoka kwa kampuni hiyo kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari tano jimboni humo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Alieleza kwasasa wanajielekeza katika kutatua tatizo la upungufu wa madarasa ambalo limejitokeza kutokana na mpango wa elimu bure.
“Tumejipanga kujielekeza katika tatizo lililoibuka la mahitaji mapya la madarasa ,maeneo mengine madawati sio tatizo lakini sasa yamejaa hadi walimu hawana nafasi ya kuandika kutokana na wingi wa wanafunzi “
“Tumetenga fedha kuanza ujenzi katika baadhi ya shule lakini pia tunaomba wahisani wajitokeza kuungana nasi kuboresha sekta ya elimu ili wanafunzi waweze kusoma kwenye manzingira mazuri”alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema kuwa program hiyo inatarajia kumalizika ndani ya miaka mitatu kutokana na halmashauri yao kuwa bado changa .
Awali akikabidhi viti na meza kwa mbunge huyo, mwakilishi wa kampuni ya Sayona fruits ambae pia ni afisa mahusinao wa kampuni ya MMI  ,Abubakary Mlawa alisema wataendelea kushirikiana na jamii ili kutatua changamoto mbalimbali.
Alisema lengo la kusaidia vitu hivyo ni kuhakikisha wanafunzi wanakaa kwenye viti ,meza na madawati na kuondokana na kero ya kukaa chini.
Mlawa alisema wanatarajia kujenga kiwanda eneo la Mboga jimbo la Chalinze kutokana na hilo ni sehemu yao kushirikiana na jamii inayowazunguka ili kuinua maendeleo .
Nae mkuu wa shule ya sekondari ya Lugoba Abdallah Sakasa aliishukuru kampuni hiyo na kuueleza bado wana changamoto nyingi hivyo wasichoke kuwasaidia.
Sakasa alimuomba mwakilishi  huyo amfikishie salamu za shukrani mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Shubash Patel  ambapo walikabidhiwa choroko kilo 50 kama zawadi yao.


Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania