CURRENT NEWS

Wednesday, July 27, 2016

WAZIRI SIMBACHAWENE:BAADHI YA WATUMISHI WANAFANYA KAZI KWA KUBUNI SAFARI ZA NJE


NA ADEN MBELLE ,SONGEA.
WAZIRI wa  nchi  ofisi  ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa [TAMISEMI] George Simbachawene amewataka wakuu wa idara wa Halmashauri za mkoa wa Ruvuma kufanya kazi za wananchi kwa kuzitatua kero zinazowakabili ,na kuachana na tabia ya kufikiria safari zenye posho.

Wito huo aliutoa jana wakati akizungumza na wakuu wa idara kutoka katika Halmashauri za mkoani Ruvuma wakiwemo wakurugenzi ,wakuu wa wilaya pamoja na  baadhi ya wabunge wanaotokea kwenye majimbo ya mkoa huo kwenye kikao cha kazi ambacho  kilifanyika kwa muda wa masaa yasiyopungua  12 huku kila Halmashauri ilitakiwa kuwasilisha utendaji kazi wake  hasa suala la madawati pamoja na vyumba vya madarasa.

Simbachawene ambaye yupo mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku mbili alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wakuu wa idara katika Halmashauri hapa nchini kutokutambua majukumu yao ya utendaji kazi kwa wananchi na badala yake wamekuwa wakiwazia safari zenye posho.

“Mimi ninajua hakuna mtu wa kunidanganya hata kidogo baadhi ya watumishi ambao ni wakuu wa idara wamekuwa siyo msaada kwa wanchi kwa kuwa wamekuwa wakifanya kazi kwa mawazo ya kubuni safari zenye posho jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo kwa wananchi”alisema Waziri Simbachawene.

  “Nawaagiza kuanzia leo kama kuna mkuu wa idara anawaza posho bila kuwaza kutatua kero za wananchi ni vema akatupisha kwa hiyari yake mwenyewe kabla hajatumbuliwa “alisema Waziri Simbachawene.

   Waziri huyo katika kikao hicho alibaini changamoto mbalimbali zinazozikabili Halmashauri hizo hasa kwa upande upungufu wa vyumba vya madarasa licha ya zoezi la utekelezaji wa madawati kwenye shule za msingi na sekondari kukamilika.

   Aidha katika hatua nyingine alizitaka Halmashauri hizo kukusanya mapato kwa njia ya kieletroniki pamoja kuyasimia kikamilifu ili yaweze kuleta tija kwa wananchi katika kufanikisha kutekeleza miradi mbalimbali kwa muda muafaka.
       MWISHO.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania