CURRENT NEWS

Thursday, August 4, 2016

KOKA:AAHIDI KUTOA MIL.7 KUNUNUA JENERETA DOGO LA CHUMBA CHA UPASUAJI


Mbunge wa jimbo la  Mji wa Kibaha Silvestry Koka, akizungumza na waandishi wa habari,namna alivyojipanga kutatua changamoto za kiafya jimboni hapo,hususan kituo cha afya  cha mkoani. (Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MBUNGE wa jimbo la Mji wa Kibaha,Silvestry Koka ,ameahidi kutoa kiasi cha sh.mil 7 ,kwa ajili ya kununua jenereta dogo, itakayotumika kwenye chumba cha upasuaji kwenye wodi ya akinamama wajawazito,katika kituo cha afya ya Mkoani .

Amesema kwa kupatikana jenereta hilo, itasaidia kuanza haraka kwa huduma ya upasuaji kwa akinamama hao ili kupunguza vifo vinavyotokea kwa mama na mtoto .

Aidha Koka amesema ni lazima huduma katika kituo hicho cha afya ziboreshwe,ikiwemo huduma za upasuji ili hali kuondokana kukimbilia hospitali ya rufaa ya Tumbi .
Koka aliyasema hayo ,kwa waandishi wa habari baada ya kuulizwa ni namna gani ,amejipanga kuhimiza kuanza kwa huduma za upasuaji kwa wakinamama katika kituo cha afya Mkoani baada ya kuonekena kuna kusuasua kwa kuanza huduma hizo .

Alisema atahakikisha anatoa fedha kwa ajili ya kununulia jenereta hilo,huku halmashauri ya Mji wa Kibaha ikijipanga kununua jenereta kubwa kwa matumizi ya hospitali nzima.

“Kituo cha afya Mkoani kinachopiganiwa kuwa hospitali ya wilaya kinakabiliwa na tatizo kubwa la kukosekana kwa huduma ya operesheni kwenye wodi ya kinamama ,hivyo ni lazima kufanya jitihada zitakazookoa maisha ya mama na mtoto”

‘Hospitali nzima inahitaji jenereta kubwa yenye uwezo wa kv 72 litakalogharimu  mil .45 hadi 50,kuliko kuendelea kusubiri fedha nyingi za jenereta la hospitali nzima ni vyema kununua jenereta ndogo lenye uwezo wa kuendesha chumba hicho”alisema Koka.

Hata hivyo,Koka alieleza kuwa kwasasa jitihada zimefanyika kujenga chumba cha upasuaji lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa jenereta na baadhi ya vifaa vinavyoletwa kutoka bohari kuu ya madawa(MSD).

Nae Elina Mgonja ambae pia ni diwani wa viti maalumu katika halmashauri ya Mji huo, alisema kuna kila sababu ya halmashauri na wadau kushirikiana kuboresha huduma za afya upande wa mama na mtoto.

Alisema huduma za upasuaji zianze haraka ili kunusuru maisha ya mama na mtoto na kuacha kutegemea kukimbizwa hospitali jirani.

“Sisi kama halmashauri hatuna budi kupambana ili kuwepo kwa huduma hiyo muhimu na kuisukuma bohari ya madawa kufikisha vifaa na madawa yanayohitajika katika chumba  “alisema mama Mgonja.

Mama Mgonja aliomba suala hilo lizingatiwe ili kinamama wasiweze kupoteza uhai wao kirahisi na kuomba tatizo hilo liwekewe kipaombele pasipo kupuuzwa.

Mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Kibaha,dk Happiness Ndosi ,akitoa ufafanuzi,alisema chumba cha upasuaji kipo tayari kwa asilimia 90.

Alisema kikwazo kikubwa kinachosababisha huduma hizo kukwama ni kutokana na kukosekana vifaa mbalimbali muhimu ambavyo huwezi kuanza huduma hizo hadi viwepo kwa vifaa na hivyo.

Dk.Ndosi alisema hatua walizozichukua ni kufuatilia vifaa hivyo huko MSD ili waweze kuanza kutoa huduma hizo.

‘Tumeshapeleka na madakatari wetu kupata elimu pale hospitali ya Tumbi,kwa ajili ya kujifresh ,pia matayarisho ya chumba yapo kwenye hatua za mwisho za umaliziaji"

Dk.Ndosi aliomba ushirikiano wa kupata standby generator kwenye chumba hicho ili kianze kazi .


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania