CURRENT NEWS

Wednesday, August 3, 2016

RIDHIWANI:VIJANA WAJITAMBUE WAACHE KUTUMIWA /WACHANGAMKIE FURSA ZILIZOPO

Mbunge wa jimbo la  Chalinze Ridhiwani  Kikwete, akizungumza na vijana wa Chalinze Saccos iliyoanzishwa jimboni hapo ambapo Ridhiwani  ni mlezi wa saccos hiyo(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete amewataka vijana wajitambue na kuacha kutumiwa kama ngazi na baadhi ya watu kwa ajili ya maslahi yao binafsi na badala yake wajikite kwenye shughuli ndogondogo za kujiongezea kipato.
Aidha mbunge huyo amekubali kuwa mlezi wa Chalinze vijana saccos ambayo itakuwa mfuko wa kuwezesha vijana kiuchumi na kutambulishwa fursa mbalimbali za kimaendeleo.
Ridhiwani aliyasema hayo, kwa vijana mbalimbali mjini Chalinze katika mkutano wa kuchagua viongozi wa muda mfupi wa saccos hiyo na mlezi pamoja na kujadili masuala ya kimaendeleo .
Alisema vijana wabadilike kwa kuchangamkia fursa zilizopo sanjali na kujiajiri ili hali kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Ridhiwani alisema ipo tabia kwa baadhi ya vijana ambao hushawishiwa kujiingiza kwenye mambo yasiyo na tija katika maisha yao kuliko kuwashawishi kuwajengea uwezo wa kuinua uchumi wao kimaisha.
Aliwaasa vijana kujitambua kwa kutumia fursa chache zilizopo ikiwemo kuanzisha vikundi vya kiujasiliamali,kutumia mafungu ya fedha zinazotengwa na halmashauri,licha kuwepo changamoto za mtaji .
Ridhiwani alisema yupo bega kwa bega na vijana hao bila kujali itikadi za kisiasa ambapo atahakikisha anawaonyesha fursa mbalimbali.
“Tatizo ni kwamba vijana hawajazitambua fursa ama kushindwa kuzitumia,kwa upande mmoja na kwa upande mwingine wale walioziona hawana uwezo wa kifedha ili kuzifikia”alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alieleza kuwa ni imani yake  kama mlezi wa saccos hiyo kuwaonyesha fursa zilipo na kuzitumia huku akishirikiana nao kupata mitaji kwa kutumia wafadhili,halmashauri na taasisi zinazojishughulisha na masuala ya kusaidia vijana.
Hata hivyo Ridhiwani alisema ameshawezesha vijana wengi jimboni hapo kujikwamua kiuchumi lakini changamoto ipo kwenye kujitambua na kumtumia katika kumfikisha kijana husika katika hatua nzuri kimaisha.
Aliwaasa vijana kuwa na moyo wa kuwa na maendeleo pale wanapopata mtu wa kuwainua bila ya kufanya makosa ya kutumia nafasi wanayoipata na hatimae kujutia baadae.
Ridhiwani aliwataka vijana kujiunga makundi katika shughuli zao na kuacha ubinafsi ili kuweza kusaidiwa na kufikiwa kirahisi kuliko kuwa mmoja mmoja.
Kwa upande wa vijana hao wa halmashauri ya Mji wa Chalinze kwa ujumla wao walimchagua Ridhiwani kuwa mlezi wao .
Walisema wameamua kwa pamoja kuunga mkono hatua za serikali kuwezesha vijana kiuchumi kupitia vicoba na saccos.
“Tumeanzisha Chalinze vijana saccos,ambayo itakuwa mfuko wa kuwezesha vijana kiuchumi na kutambua fursa za kuzikimbilia ili kujikomboa katika kupiga vita umaskini’walisema.

Mwisho

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania