CURRENT NEWS

Tuesday, September 13, 2016

DC IKUNGI AITAKA KAMPUNI YA SHANTA GOLD MINE KUWALIPA FIDIA WANANCHI WALIOFANYIWA TATHIMINI ILI KUPISHA UCHIMBAJI WA DHAHABU

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kilichohudhuriwa na Wawakilishi wa kampuni ya Shanta Gold Mine Ltd, Wananchi wawakilishi kutoka Kijiji Cha Mlumbi na Uongozi wa kikosi kazi
Wananchi wawakilishi kutoka Kijiji Cha Mlumbi na Uongozi wa kikosi kazi wakijadili jambo nje ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya kabla ya kuingia kwenye kikao
Meneja wa Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Shanta Gold Mine Ltd Philbert Rweyemamu akielezea namna ambavyo watawalipa wananchi 67 ndani ya wiki hii


Dc Mtaturu akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho kushoto kwake ni Kaimu katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi Dijovson Ntageki na wengine ni wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo
Wananchi wawakilishi kutoka Kijiji Cha Mlumbi na Uongozi wa kikosi kazi wakisikiliza kwa makini maelezo ya mkuu wa Wilaya
Kamishina wa Madini Kanda ya Kati Sospita Masorwa akielezea namna ambavyo uthamini unakuwa umekamilika kuwa ni mara baada ya Mthamini Mkuu wa serikali kupitisha
Kutoka kushoto ni Afisa Tarafa ya Ikungi Josephine, Kamishina wa Madini Kanda ya Kati Sospita Masorwa, Ally Kassim Mjiolojia kampuni ya Shanta Gold Mine Ltd, Meneja Mkuu Shanta Gold Mine Ltd Philbert Rweyemamu, David Rwechungura Meneja Rasilimali watu kampuni ya Shanta Gold Mine Ltd, na Daniel Mwita

Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akifunga kikao mara baada ya maridhiano
 
Na Mathias Canal, Singida

KAMPUNI ya Uchimbaji wa Madini ya dhahabu (Shanta Gold Mining  Limited) iliyopo katika kijiji cha Sambaru Kata ya Mang’onyi Wilayani Ikungi, Mkoani Singida imetakiwa kuwalipa wananchi 69 waliosalia kulipwa fidia zao kwa ajili ya kupisha mradi wa uchimbaji dhahabu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Miraji Jumanne Mtaturu kufuatia malalamiko ya wananchi wa maeneo mbalimbali waliopo kwenye eneo la mradi huo waliotaka kufahamu hatima ya malipo yao kutokana na awamu ya kwanza kuonyesha kuwa watu 67 ndio watakaolipwa mwishoni mwa wiki hii na wengine waliobaki kulipwa katika awamu zijazo.

Dc Mtaturu ametoa agizio hilo wakati wa kikao cha pamoja kilichohudhuriwa na Wawakilishi wa kampuni ya Shanta Gold Mine Ltd, Wananchi wawakilishi kutoka Kijiji Cha Mlumbi na Uongozi wa kikosi kazi ambacho kilipewa jukumu la kuhakikisha wananchi wote ambao watapitiwa na mradi huo wanalipwa fidia sambamba na kusimamia uhamishaji wa makazi.

Kapuni ya Shanta Gold Mine ltd imetakiwa kutumia siku 68 yaani hadi kufikia mwezi Novemba mwaka huu kumaliza malipo ya watu 69 kati ya 136 ambao wanatakiwa kulipwa katika awamu ya pili ili wananchi hao waweze kupisha mradi huo ambao kwa kiasi kikubwa umeshindwa kuanza uchimbaji wa madini aina ya dhahabu kutokana na malalamiko ya malipo ya fidia kwa baadhi ya wananchi ambao tayari wamefanyiwa uthamini wa maeneo yao.

Sambamba na hayo pia Mkuu huyo wa wilaya ameagiza kikosi kazi kuendeleana kazi yake mpaka pale malipo ya wananchi hao yatakapokamilika pamoja na kuwapo kwa maneno kuwa kilivunjwa mwanzoni mwa mwezi wa tatu, jambo ambalo limepingwa vikali na uongozi huo wa Wilaya.

Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Shanta Gold Mine Ltd Philbert Rweyemamu amesema kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi hao juu ya kutaka wananchi wote walipwe kwa wakati mmoja jambo ambalo sio rahisi kutokana na pesa iliyopatikana kutoka kwa wawekezaji wa hisa tangu mwaka 2012 mpaka sasa bado inatumika haijaanza kuingiza faida hivyo malipo ya awamu yatakuwa muarobaini wa malipo hayo mara baada ya kuanza kwa uchimbaji hivyo kadri mradi unavyoendelea kuchelewa kuanza ndivyo ambavyo fedha inapoteza thamani.

Hata hivyo amejibu hoja ya wananchi kuwa Kampuni hiyo ndiyo ilileta Mthamini wa maeneo ya wananchi jambo ambalo halina ukweli halisi kwani wananchi wenyewe ndio walioamua juu ya Mthamini wanayemtaka kutokana na makubaliano yao.

Rweyemamu alisema kuwa endapo kama mradi huo ungeanza mapema kama vile ilivyokuwa imepangwa ni dhahiri sasa ungekuwa umezalisha ajira zaidi ya mara tano kwa wakazi wa maeneo husika na Taifa kwa ujumla jambo ambalo lingerahisisha kuongeza pato la wananchi wa Wilaya husika na Taifa kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa wananchi walio katika eneo la mradi huo Ramadhani Said Nyeri amesifu juhudi za utendaji kazi wa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kumteua Mkuu huyo wa Wilaya ambaye anaonyesha maslahi mapana na wananchi kutokana na juhudi mbalimbali za utendaji kazi.

Pamoja na pongezi hizo Nyeri amesema kuwa endapo viongozi mbalimbali wa serikali watafanya kazi kwa mazoea kwa kutumia vibaya nafasi zao ni dhahiri kuwa lawama na malalamiko ya wananchi yatakuwa laana kwao.

Nyeri alisema kuwa kikosi kazi hicho kilianza kazi hiyo mwaka 2014 ambacho kilianzishwa na Kampuni ya Shanta gold Mine ltd kwa makubaliano na wananchi wa maeneo husika ambapo katika kipindi chote hicho vimefanyika vikao vitano ambavyo viliendeshwa vyema pasina malalamiko kwa upande wowote ule.

Akifunga kikao hicho Dc Mtaturu alisema kuwa katika makubaliano ya namna ya kuendesha utendaji kazi wa kikosi kazi hicho mbunge wa jimbo la Singida Mashariki Tundu lissu alipaswa kuwepo lakini hajawahi kushiriki hata kikao kimoja jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaashiria mbunge huyo kukimbia majukumu yake kama muwakilishi wa wananchi.

Aidha amekipongeza kikosi kazi hicho kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kwa kipindi chote hicho huku akiitaja miaka 10 waliyofanya kazi kumekuwa na daraja kutokana na baadhi ya viongozi kukimbia majukumu yao na kuwaacha wananchi kujishughulikia na kumaliza matatizo yao wao wenyewe.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania