CURRENT NEWS

Wednesday, September 21, 2016

DC MTATURU: SERIKALI ITAVISAIDIA VIKUNDI VITAKAVYO KUWA TAYARI KUJIHUSISHA NA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akisisitiza umakini kwa wananchi waliojitokeza kwenye Kikao cha Mafunzo ya namna bora ya kushiriki katika kilimo chambogamboga na matunda kupitia umwagiliaji
Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ayub Sengo akiwasihi wananchi kutumia njia za kisasa katika kilimo cha umwagiliaji na kufuata taratibu wanazoelekezwa na wataalamu wa kilimo
Baadhi ya viongozi wa vikundi mbalimbali vya ujasiriamali sawia na wajumbe washiriki kwenye mafunzo hayo wakifatilia kwa makini Muelimishaji
Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya kiserikali ya RIWADE Mhandisi Ayubu Massau, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu, Moses Msai Mratibu wa RIWADE mkoa wa Singida na Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ayub Sengo
Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu na kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bi Haika Massawe wakifatiliakwa makini mafunzo ya namna bora ya kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Gree House
Kutoka Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Hassan Tati, Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya kiserikali ya RIWADE Mhandisi Ayubu Massau, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bi Haika Massawe, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu, Moses Msai Mratibu wa RIWADE mkoa wa Singida na Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ayub Sengo
Dc Mtaturu akisisitiza jambo wakati wa kufunga mafunzo hayo

Na Mathias Canal, Singida

Uongozi wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida umeahidi kuvisaidia vikundi mbalimbali ambavyo vitakubali kujihusisha na kilimo cha mbogamboga na matunda (Perishable Crops) sambamba na kilimo hicho kwa kutumia Kitalu Nyumba (Green House).

Kauli ya serikali imetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakati akifunga mafunzo kwa wajasiriamali, wakulima na wafugaji yaliyoendeshwa na Asasi isiyo ya kiserikali ya Right Way For Development (RIWADE) kwenye ukumbi wa Mikutano katika Shule ya Sekondari Ikungi na kuhudhuriwa na watu 115 ambao wanatokea katika Kata 24 kati ya Kata 28 zilizopo Wilayani humo.

Katika Mafunzo hayo jumla ya Vikundi 39 vimehudhuria ambavyo vimetakiwa kujishughulisha zaidi kukimbia kilimo cha mazoea ambacho wakulima hulima msimu mmoja hadi mwingine na hatimaye kujihusisha na kilimo cha umwagiliaji ambacho kinatumia muda mchache kukamilika na kuanza kwa mavuno.

DC Mtaturu amevitaka vikundi hivyo kwa pamoja kutumia vyema fursa ya Makao makuu ya serikali kuhamia Mjini Dodoma kwani itakuwa taswira chanya katika kukuza soko la mazao yao pasina kupata ugumu wa uuzaji.

Amesema kuwa Mkoa wa Singida mara nyingi umekuwa ukitajwa kama mkoa masikini nchini Tanzania kati ya mikoa 10 ambayo ipo mkiani katika maendeleo ya kiuchumi kwa sababu ya wananchi wenyewe kutofanya ubunifu katika kilimo chao jambo ambalo linasababisha uzalishaji mdogo na kupelekea kipato kuendelea kuwa duni ilihali maandalizi ya mashamba ni makubwa.

Mtaturu amesema kuwa wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa serikali katika kukamilisha adhma yake katika uwekezaji na Tanzania ya viwanda kwani endapo watakubali kulima kilimo cha kisasa na kuwa na uzalishaji mkubwa itakuwa rahisi kwa serikali kuanzisha viwanda vya kusindika mazao.

Kwa upande wake muwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya kiserikali ya RIWADE ambayo imesajili kwa lengo la kiwasaidia vijana wasio na ajira waweze kufanya kilimo, Ufugaji, Uvuvi na Mazingira Mhandisi Ayubu Massau alisema kuwa wananchi wanapaswa kufikia kilimo cha kuachana na kuuza mazao yao kwa madalali badala yake kuuza moja kwa moja kwa mtumiaji jambo ambalo litatoa fursa chanya ya mafanikio makubwa katika pato la mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo amepigia chepuo zaidi kilimo cha Kitalu Nyumba (Green House) na kusema kuwa ndicho kilimo pekee chenye uwezo wa kuwatoa wananchi kwenye kadhia ya umasikini kwani kilimo hichp kupitia umwagiliaji wa kisasa unatumia maji machache na matokeo yake ni makubwa kama wakulima watafuata taratibu zote za utunzaji wa shamba.

Massau alisema kuwa umefika wakati wa wananchi kuachana na vyama vya kufa na kuzikana badala yake kujihusisha zaidi na vyama vya kujikwamua kiuchumi kupitia vikundi mbalimbali.

Naye Moses Msai ambaye ni Mratibu wa RIWADE mkoa wa Singida alisema kuwa wakulima wanapaswa kutambua kuwa sekta pekee yenye uwezo wa kuajiri watu wengi na kuwatoa kwenye lindi la umasikini ni Sekta ya Kilimo hivyo ni vyema kufanya kilimo cha kisasa kwani ndicho kitakacho wanufaisha wananchi.

Ametoa fursa kwa wananchi kujiunga na RIWADE kwani watapata fursa ya kuunganishwa na wataalamu ili kuelekezwa namna bora ya kulima kilimo cha umwagiliaji.

Hata hivyo Mjasiriamali na mkulima aliyeshika nafasi ya Kwanza kanda ya kati katika sekta ya kilimo Hassan Tati aliwasihi wakulima hao waliopatiwa mafunzo kuwa mafanikio kwenye kilimo ni makubwa endapo wakulima watafuata taratibu za kilimo na kuwasikiliza wataalamu.

Tati amesema kuwa hakuna ajira nzuri duniani kama kuwekeza kwenye kilimo lakini amewasihi wananchi kuing'ang'ania Asasi ya RIWADE kwani ni taasisi muhimu kwa kila mmoja kwa kujitolea kutoa mafunzo ya kilimo na ufugaji.

Asasi isiyo ya kiserikali ya Right Way For Development (RIWADE) ilianzishwa Mwezi June 2016, ikiwa ni dhima ya kutengeneza na kutoa fursa kwa watanzania wote ili waweze kupata elimu ya ujasiriamali na namna ya kutengeneza mitaji kwa ajili ya ukuaji endelevu wa kijamii na kiuchumi.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania