CURRENT NEWS

Friday, September 2, 2016

KATIBU MKUU PROF.KAMUZORA ATOA WITO KWA VYUO KUANZISHA MITAALA INAYOHUSU USALAMA WA MITANDAO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Prof. Faustin Kamuzora akizungumza wakati akifunga warsha ya wadau na wataalamu kutoka Shirika la Mawasiliano la Jumuiya ya Madola (hawapo pichani) kuhusu uandaaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Usalama katika Mitandao nchini.
Na Jacquiline Mrisho 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ( Sekta ya Mawasiliano), Prof. Faustin Kamuzora ametoa wito kwa vyuo vyote nchini kuanzisha mitaala inayohusu usalama wa mitandao ya mawasiliano ili kukabiliana  na matumizi mabaya ya mitandao hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu huyo alipokuwa akifunga warsha ya siku ya wadau na wataalamu kutoka Shirika la Mawasiliano la Jumuiya ya Madola iliyohusu Uandaaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Usalama wa Mitandao iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

Prof. Kamuzora amesema kuwa moja ya vitu vilivyoelezewa katika Sera ya Tehama iliyotolewa mwezi Mei mwaka huu ni kuhakikisha mitandao ya mawasiliano inakuwa salama hivyo kila mwananchi anawajibu wa kulinda mitandao hiyo.

“Suala la usalama wa mitandao ya mawasiliano linapelekea kuwepo kwa fursa nyingi za ajira hivyo, napenda kutoa wito kwa vyuo mbalimbali nchini kuanzisha mitaala mipya itakayohusu masuala haya kwa sababu watu watatakiwa wajikite kwenye masomo yanayohusiana na mitandao”, alisema Prof.Kamuzora.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni zimebainisha kuwa dunia nzima inapoteza jumla ya dola bilioni 400 kwa mwaka kwa njia ya wizi wa mitandaoni hivyo kushindwa kulinda mitandao ya mawasiliano kunapelekea hasara kubwa kwa Taifa na Dunia kwa ujumla.

Naye Afisa Mwandamizi wa ufundi na ushauri  wa Shirika la Mawasiliano la Jumuiya ya madola, Fargani Tambeayuk amesema kuwa Jumuiya hiyo inawasaidia nchi wanachama katika kudhibiti usalama wa mitandao ili kusaidia nchi hizo kupata maendeleo kwa kutumia mitandao pamoja ma kuepukana na uhalifu.

Kwa upande wake Mratibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Makosa ya mitandao, Joshua Mwangasa amesisitiza suala la kutolewa kwa elimu ya usalama wa mitandao liwe endelevu akiamini kuwa elimu hiyo itawasaidia wananchi kuepuka kutumia vibaya mitandao ya mawasiliano.

Aidha, ameusifia mpango huo kwani utawasaidia Jeshi la Polisi kuweza kukabiliana kirahisi na wananchi wanaofanya makosa kwenye mitandao pia amesisitiza kuwa makosa ya kimtandao ni kama makosa mengine hivyo taratibu za kuripoti makosa hayo ni zile zile za kawaida.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania