CURRENT NEWS

Monday, September 12, 2016

KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI PWANI CHAKUSANYA BIL.2.033

Kamanda wa kitengo cha Usalama barabarani  mkoani Pwani, Abdi Issango pichani (Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi
Kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Pwani kimeliingizia serikali mapato ya zaidi ya sh.bil.2.033 katika kipindi cha januari hadi agosti mwaka huu .

Kikosi hicho kimekusanya mapato hayo kupitia ukamataji wa makosa mbalimbali ya usalama barabarani mkoani humo.

Mkuu wa usalama barabarani mkoani Pwani, Abdi Issango alisema  katika kupambana na ajali wameweza kuendesha misako na kufanya ukaguzi mbalimbali katika barabara kuu na za ndani ya miji.

Alieleza kuwa kwa kipindi miezi nane wamekamata jumla ya  makosa 68,109  ambapo yaliyolipiwa kiasi hicho cha fedha ni 67,785 mwaka huu.

Kamanda Issango alisema makosa hayo yakilinganishwa na ya mwaka jana kipindi hicho kuna ongezeko la makosa 20,797 ambayo ni sawa na ongezeko la sh. mil. 569,400 sawa na asilimia 38.89.

Alisema kuwa katika kipindi kama hicho mwaka 2015 kitengo hicho kilikamata makosa 47,109 na yaliyolipiwa ni 46,988 sh.bil. 1,464,150.

Aidha akizungumzia matumizi ya speed radar mpya 24 za kisasa walizopewa mwaka jana ambazo zinapiga picha na kurekodi wameweza kukamata makosa ya magari yanayokwenda kwa mwendo kasi 32,753 .

Kamanda Issango alisema magari hayo yaliyokamatwa kwa ajili ya kukimbiza magari yalilipiwa faini sh. mil 982,590 kutoka januari hadi agosti mwaka huu.

"Vitendea kazi tulivyonavyo ikiwa ni pamoja na speed radar hizi za kisasa, tunaweza kusema sisi Pwani tumefanikiwa kudhibiti ajali zitokanazo na mwendo kasi kwa asilimia 100 hasa mabasi ya abiria”alisema Issango.

Hata hivyo kitengo hicho kuelekea maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani wameanza kutoa mafunzo mbalimbali kwa waendesha pikipiki,wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na mikusanyiko ya watu ili kuwapa uelewa wa matumizi sahihi ya alama za barabarani.


Issango aliwataka madereva ,abiria na watumiaji wengine wa barabara kuu kuzingatia kanuni,sheria na taratibu ya matumizi ya njia hizo kuu ili kuendelea kudhibiti ajali
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania