CURRENT NEWS

Monday, September 26, 2016

KIWANDA CHA KUUNGANISHA MATREKTA KILICHOPO PWANI KUANZA NOVEMBA


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

KAMPUNI ya equator SUMAJKT iliyoko Ruvu, mkoani Pwani, kwa mara ya kwanza itaanza kuunganisha matrekta ya farmtrac hapa nchini baada ya kuingia mkataba wa uhawilishaji teknolojia na kampuni inayotengeneza matrekta hayo ya Escort ya India.

Kupitia makubaliano hayo equator SUMAJKT itaweza kuunganisha  matrekta kwa ajili ya soko  la Tanzania  na masoko ya bara  la Afrika kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari, waliokwenda kutembelea kiwanda hicho, mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Robert Mangazeni alisema awali matrekta yalikuwa yakiletwa kutoka India.

Alisema lakini baada ya makubaliano hayo kampuni hiyo haitaleta tena matrekta hapa nchini badala yake  yataunganishwa katika kiwanda hicho cha kampuni ya Equator SMJKT.
" Hatujawahi kuwa na kiwanda wala karakana  za kutengeneza matrekta hapa nchini,  yanapohabirika hutengenezwa kiwango cha chini  na mafundi wasio na ujuzi,"

"Mara nyingi yakishindikana  huegeshwa na kutelekezwa baada ya kushindwa kufanya Kazi, kwa mara ya kwanza equator SUMAJKT tutafanya Kazi hiyo, tunayetengeneza pia kuyahudumia yanapoharibika, "alisema Mangazeni.

Alisema matrekta hayo watayauza wakulima kupitia wakala wao  kwa bei nafuu lakini pia watakopesha wakulima walipe kidogo kulingana na uwezo wa kila mtu  ili kusaidia waweze kulima kilimo chenye tija na kupata kipato na faida.

Aidha Mangazeni alisema kiwanda hicho kinatarajia kuanza kazi rasmi mwezi novemba.
Alielezea kuwa mbali na kazi yaykuunganisha matrekta pia kiwanda hicho kitaunganisha mabasi, na magari  mbalimbali, pia  zana za kilimo.

" Tunatarajia kushirikiana na viwanda vya ndani kwa ajili ya kuzalisha vipuli mbalimbali vya magari, matrekta na zana za kilimo, tunategemea kushirikiana na kampuni  ya Automech, kiwandacha TATC- Nyumbu, SIDO, UDSM na vingine.

Alisema wataalamu kutoka nje kwa ajili ya ufungaji wa mitambo  wameshafika na hatua za awali za ujenzi wa majengo  ya kiwanda hicho na usimikaji wa mitambo na vifaa zimeshaanza.

Mangazeni alisema hadi sasa zimeshatumika kiasi cha sh.bil 2,ambapo hadi  kukamilika kwake mwishoni mwa mwezi novemba  kinatarijia kutumia bil.3.

Kampuni  ya equator SUMAJKT ni ubia kati ya shirika la  uzalishaji mali la JKT (SUMAJKT) na kampuni ya equator  Automech ambayo ni ya watanzania wakiwamo wastaafu kutoka jeshi la ulinzi la  wananchi wa Tanzania (JWTZ).

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania