CURRENT NEWS

Friday, September 16, 2016

MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA OZONI DUNIANI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. January Makamba akiongea na waandishi wa Habari juu ya Siku ya Kimataifa ya tabaka la Ozoni. Siku hii huadhimishwa Septemba 16 kila mwaka. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mazingira Bw. Richard Muyungi. (Picha kwa hisani ya Idara ya Habari Maelezo)


Tarehe 16 Septemba mwaka huu tutaungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kama ilivyoagizwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Azimio lake nambari 49/114 la tarehe 19 Desemba 1998 kama kumbukumbu ya tarehe ya kutiwa saini Mkataba wa Montreal (Montreal Protocol – 1987) kuhusu kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni angani. 

Ozoni ni hewa iliyoko kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 10 hadi 50 juu ya ardhi. Kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mnururisho wa mionzi kama “Ultraviolet B” isifike kwenye uso wa dunia. Ujumbe wa mwaka huu ni “Kuhuisha Tabaka la Ozoni na Tabia-Nchi kwa pamoja Duniani”. Ujumbe huu umeambatana na Kauli mbiu isemayo “Kukabiliana na ongezeko la gesi Joto Duniani HFCs chini ya Itifaki ya Montreal”. 

Tabaka la Ozoni linapoharibiwa huchangia kuruhusu mionzi zaidi ya “Ultraviolet B” kufika kwenye uso wa dunia na hivyo kusababisha kuongezeka kwa magonjwa kama vile saratani ya ngozi, uharibifu wa macho yaani “mtoto wa jicho” unaosababisha upofu, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi. Aidha, madhara mengine ni kuharibika kwa mimea hasa mazao ya kilimo kutokana na kuathirika kwa maumbile na mifumo ya ukuaji. 
 
Vile vile, baadhi ya kemikali hizi husababisha kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi. 
Ili kulinda tabaka la Ozoni, Serikali za mataifa mbalimbali zilikubaliana kuunda Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka 1985. Mkataba huu unasisitiza ushirikiano katika utafiti, usimamizi na ubadilishanaji wa taarifa za hali ya Tabaka la Ozoni kutokana na kupungua kwa matumizi yake. 
 
Vile vile ulianzishwa Mkataba wa Montreal (Montreal Protocol) unaohusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni na Mkataba huu ulipitishwa tarehe 16 Septemba, 1987. Lengo kuu la Mkataba huu ni kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa kudhibiti utengenezaji na matumizi ya kemikali zinazoharibu Tabaka hili. 

Hadi sasa Mkataba wa Montreal umepata mafanikio makubwa ya kupunguza zaidi ya kiasi cha asilimia 98 (takribani tani 1.8) ya uzalishaji wa matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni. Punguzo hilo la matumizi ya kemikali hizi limechangia katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu baadhi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni pia husababisha kuongezeka kwa joto duniani. 
 
 
Kwa mfano, kiasi cha kemikali kilichoondolewa katika matumizi ni takriban tani bilioni 135 za hewa ukaa na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, matokeo ya tafiti yanathibitisha kwamba kiwango cha kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni angani kinaendelea kupungua na inakadiriwa kuwa iwapo jitihada za utekelezaji wa Mkataba huu zitaendelea, Tabaka la Ozoni litarudi katika hali ya kawaida ifikapo katikati ya karne hii. 

Ili kufanikisha utekelezaji wa Mkataba wa Montreal, mwaka 1996 Serikali iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali hizi. Mikakati ya kitaifa ndani ya Programu hii ni pamoja na:
i) Kujenga uwezo wa Taasisi zinazosimamia utekelezeji wa Mkataba;
ii) Kuweka takwimu za kemikali hizo; 

iii) Kutoa elimu kwa wadau na kwa umma wa Watanzania kuhusu umuhimu wa Tabaka la Ozoni na hatari zinazolikabili; 
iv) Kusambaza habari kuhusu kemikali na tekinolojia mbadala;
v) Kubadilisha tekinolojia katika viwanda vinavyotumia kemikali haribifu;
vi) Kutoa mafunzo yanayolenga kuimarisha ujuzi katika sekta ya kuhudumia viyoyozi na majokofu; 
vii) Kuimarisha mbinu za upunguzaji wa matumizi ya kemikali husika kwa kuanzisha mtandao wa kunasa, kusafisha na kurejeleza vipoza joto;
viii) Kuhamasisha na kuhimiza matumizi ya kemikali na tekinolojia mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni; na 
ix) Kuweka taratibu za kudhibiti uingizaji na matumizi ya kemikali zinazodhibitiwa na Mkataba wa Montreal. 

Hatua hizi zimewezesha Tanzania kuondosha kemikali hizi kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa na Mkataba. Kwa mfano, Viwanda vitatu vilivyokuwa vinatumia kemikali haribifu vimebadilisha teknolojia hiyo. Aidha, wafanyabishara wengi ambao ni wauzaji wa kemikali husika wamekuwa na uelewa mkubwa na hivyo biashara ya kemikali mbadala imeendelea kukua mwaka hadi mwaka. 

Chini ya Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali haribifu, Serikali iliandaa Mpango wa Usimamizi wa Vipozi (Refrigerant Management Plan) ambao utekelezaji wake umefanyika kama ifuatavyo:
Kuandaa Kanuni za Usimamizi wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la hewa ya Ozoni na zilianza kutumika tarehe 7 Desemba 2007;
Jumla ya mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu 500 wamepatiwa mafunzo kuhusu njia bora za kuhudumia vifaa hivyo bila kuathiri Tabaka la hewa ya Ozoni; 
Kusambazwa kwa Vitambuzi vya kemikali hizi vipatavyo 18 kwa ajili ya usambazaji katika vituo vilivyo mipakani mwa nchi yetu; 
Mashine 20 za kunasa na 5 za kunasa na kurejeleza gesi chakavu zimenunuliwa na kusambazwa kwa karakana 20 na Vituo vitano vya Kikanda vya kunasa na kusafisha gesi chakavu za Majokofu na Viyoyozi katika vyuo vya VETA vya Mwanza, Chang’ombe – Dar es salaam, Kigoma, Mbeya na Mkokotoni-Zanzibar;
Mtambo wa kunasa na kurejeleza kemikali umewekwa katika Kituo cha Tanzania cha Uzalishaji Bora na Tekinolojia Endelevu (Cleaner Production Centre for Tanzania);
Utekelezaji wa Mpango wa Kusimamia Usitishaji wa Matumizi ya Kemikali hizi (Terminal Phase-out Management Plan (TPMP). 
Jumla ya maafisa forodha na wasimamizi wa sheria 172 wamepatiwa mafunzo kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la hewa ya Ozoni.

Hadi sasa Tanzania imeweza kupunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86 ya kiasi cha matumizi ya kemikali hizi cha mwaka 1999. Hapa nchini maadhimisho haya yatafanyika kwa njia ya uelimishaji umma kuhusu Tabaka la Ozoni, faida zake, madhara ya kuharibika kwa Tabaka hili na matumizi salama ya bidhaa zenye kemikali rafiki kwa Tabaka la ozoni. 
 
Hivyo kupitia kwenu wanahabari naamini elimu hii itaendelea kutolewa kwa jamii ya Watanzania ili kuongeza ushiriki wao katika kutekeleza jukumu hili muhimu la kulinda sayari hii. Makala zimeandaliwa ili muweze kuzitumia katika kuwafikishia Wananchi elimu hii muhimu. 

Ni muhimu tuzingatie kwamba juhudi za kila mmoja wetu zinatakiwa ili kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na bidhaa tunazonunua na kutumia majumbani au sehemu za biashara. Natoa wito kwa kila mwananchi kushiriki katika 
 
kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa kuzingatia mambo yafuatayo:
Kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mitumba) na ambavyo vinatumia vipoozi aina ya R11 na R12.
Kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni kama vile R22, R134a, R407, R404 na R717. 

Kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo “Ozone friendly” yaani “sahibu wa Ozoni” au “CFC-free” ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni. 
Kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni aina ya “CFCs” na “halon”. Pata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mafundi ama mamlaka zinazohusika.

Kuepuka matumizi ya kemikali aina ya “Methyl bromide” kufukizia udongo, na badala yake kutumia mbinu mbadala na salama pamoja na mbinu tungamanishi za udhibiti wa wadudu waharibifu yaani “integrated pest management”.

Mafundi wa majokofu na viyoyozi wahakikishe kuwa wananasa na kutumia tena vipoozi (refrigerants) kutoka kwenye viyoyozi, na majokofu wanayohudumia badala ya kuviachia huru visambae angani. Aidha, mafundi watoe elimu kwa wateja wao juu ya njia rahisi za kutambua uvujaji wa vipoozi kutoka katika majokofu na viyoyozi wanavyotumia. 
Nawatakieni maadhimisho mema ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni. 

JANUARY Y. MAKAMBA (MB.) 

WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS 

MUUNGANO NA MAZINGIRA
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania