CURRENT NEWS

Tuesday, September 27, 2016

MAJALIWA AKEMEA NDOA ZA UTOTONI/ATAKAEBAINIKA MIAKA 30 JELA


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa ,amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuwaoza watoto wao wa kike wenye umri mdogo,ambapo atakaebainika kufanya hivyo atapelekwa mahakamani na kuhukumiwa miaka 30 jela.
Amesema wapo baadhi ya watu wanaofikiria ni suala la mzaha lakini kuanzia sasa serikali haina mzaha wala haipambi maneno kwa hilo.
Aidha Majaliwa amewataka wazazi na walezi hao kuwasimamia watoto wao katika elimu ili kuwajengea maisha bora ya baadae.
Waziri mkuu aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara Ikwiriri na Utete wakati wa ziara yake,aliyoifanya wilayani Rufiji.
Majaliwa alisema sheria ni lazima ichukue mkondo wake ili kupunguza ndoa za utotoni na kuwapa fundisho wale wote wanaohusika kuwapa wanafunzi mimba na kuwaoza watoto wakiwa shuleni na umri mdogo.
Alieleza jamii ibadilike iachane na tabia ya kumalizana na kesi majumbani bali, kesi na matukio ya aina hiyo yanapaswa kushtakiwa na kutendewa haki ili kupunguza vitendo vya aina hiyo ndani ya jamii zetu.
Majaliwa alisema kuwa baba na mama wa mtoto wa kike, wanaemuozesha wote watafunguliwa mashtaka na kufungwa katika kipindi hicho.
Alieleza kuwa pia anaesindikiza mtoto kwenda kuoa,anaekaa kwenye mkutano wa posa  kama shahidi atakaekamatwa wote watafungwa kwa kosa hilo.
“Mama na baba mnaooza watoto wenu ,miaka 30 inawangoja,anaesindikiza mtoto kuolewa,anaekaa kama shahidi wote kosa ni moja,serikali haipambi maneno wala haina mzaha katika hili”alisisitiza Majaliwa.
Hata hivyo aliwataka watoto wa wilaya ya Rufiji na mkoani Pwani wasome na sio kukimbilia ndoa za utotoni ambazo hazina manufaa kwao.
Majaliwa aliiomba jamii kusimamia watoto wao kwenye maadili mema ya kitanzania na kuwajengea mawazo ya kupenda elimu badala ya kujihusisha na masuala maovu.
Alisema elimu ndio ufunguo na nguzo ya maisha kwa watoto hao kuliko mambo mengine yasiyo na manufaa kwenye mstakabali wa maisha yao.
Aliwaasa wanafunzi wa kike kupenda masomo na kuachana na vishawishi na kudanganywa na wanaume wa mitaani wasiowatakia mema kwenye maisha yao.

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania