CURRENT NEWS

Wednesday, September 28, 2016

MAJALIWA ATOA MWEZI MMOJA KWA WATUMISHI KIBITI KUHAMIA KUISHI MAKAO MAKUU YA WILAYA


Na. Mwamvua Mwinyi, Kibiti

WAZIRI mkuu, Kassim Majaliwa ametoa mwezi mmoja kwa watumishi wote waliopangiwa kufanya kazi wilaya na halmashauri mpya ya Kibiti, kukaa ndani ya makao makuu ya badala ya kukaa mbali na eneo la kazi. 


Aidha amesema wilaya hiyo ni mpya haina fedha hivyo waingie mikataba na taasisi ambazo zinaweza kuwapimia ardhi ikiwemo bank ya TIB ili kuuza viwanja kwa gharama nafuu

Majaliwa aliyasema hayo, wilayani Kibiti, katika ukumbi wa ofisi ya idara ya maji, wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya watumishi wa wilaya hiyo,kwenye muendelezo wa ziara yake mkoani Pwani.

Alisema kuwa watumishi waliopangiwa kufanya kazi wilayani hapo ni lazima warudi kukaa kwenye makao makuu ya wilaya na kujipangia pa kukaa.

Majaliwa alielezea kuwa watumishi hao wasikae Ikwiriri wala Kimanzichana, bali wakae karibu ili kuwaondolea usumbufu na gharama ambazo hazina tija.

Alisema wale ambao wanatakiwa kukaa kwenye nyumba za idara nao wanapaswa kukaa walipo hadi hapo nyumba zao zitakapokuwa tayari.

Hata hivyo alimtaka mkurugenzi na mkuu wa mkoa wa Pwani, kutafuta njia nyingine ya kuwasaidia kwa kuzungumza na mifuko ya hifadhi ya jamii na national housing kuangalia uwezo wa kuwajengea nyumba 10 ama 15.

Majaliwa aliwataka kutenga maeneo ili kukaribisha wawekezaji hao waweze kujenga nyumba hizo kwa ajili ya watumishi na wakuu wa idara.

Aliitaka jamii nayo kuboresha miundombinu kama fursa ya kushirikiana na wilaya kujenga nyumba za kupangisha na mahoteli.

Akiwa katika ziara hiyo alikutana na tatizo la uhaba wa watumishi, vitendea kazi na nyumba za watumishi.

Katika hatua nyingine Majaliwa, aliwataka wakuu wa idara, watumishi na madiwani kuendelea kutambua vyanzo vingine vya mapato ili kuweza kufanya matumizi mingine ya halmashauri ya wilaya.

Aliwaasa kuimarisha mapato ya ndani, na waendelee kutambua vyanzo vingine vipya vya kupata mapato na kuongeza mapato kwa mwaka ili yasaidie matumizi ya ndani.
Majaliwa aliwasisitiza kusimamia fedha zinazopelekwa na serikali.

Alihimiza uwajibikaji na uadilifu katika maeneo ya kazi na kuwataka watumishi wabadilike na waache kufanya kazi kwa mazoea.

Majaliwa alisema hataki kuona baraza la madiwani likitumika kufuja fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo hivyo kuanzia sasa kuna kila sababu ya madiwani kusimama bila kuzembea kwenye fedha za miradi.

Alikemea madiwani kuacha kubishana kwenye mabaraza ya madiwani kwani hakuna tija kwao na kuacha kulaghaiwa na fedha ama chakula na wakuu wa idara.

Mkuu wa wilaya ya Kibiti, Gulam Kifu alisema wanakabiliwa na uhaba wa watumishi na wakuu wa idara na waliopo ni wawili pekee.

Alitaja changamoto nyingine ni migogoro ya wakulima na wafugaji, uhaba wa walimu 169 na madawati 280.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Kibiti, Alvera Ndabagayo, wapo watumishi wanaokaimu na wakuu wa idara wawili.

Alisema wameomba jengo corecu ambapo watalikarabati na sasa wanasubiri kikao cha fedha kupitisha jengo hilo ambalo litawasaidia kama ofisi.

Alvera alisema wamejipanga kufanya kazi hata chini ya mti, wanachohitaji jengo na litakapopitishwa na vikao husika wataanzia hilo.

Akiwa wilayani Kibiti, Majaliwa alipata fursa ya kuzungumza na wananchi wa Kibiti na Nyamisati na kukagua kiwanda cha uchakataji muhogo kilichopo Bungu.
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania