CURRENT NEWS

Monday, September 26, 2016

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWATUMBUA WANNE IDARA YA MISITU RUFIJI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Utete na Ikwiriri .

Na Mwamvua Mwinyi,Rufiji
WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa,amewasimamisha maafisa misitu watatu pamoja na meneja wa wakala wa misitu (TFS)wilayani Rufiji ,kutokana na kushindwa kudhibiti na kusimamia shughuli za uvunaji misitu na kusababisha wilaya kukosa mapato .
Amesema watumishi hao ambao ni pamoja na mkuu wa idara ya misitu wilaya Paul Ligonja,maafisa misitu Gaudence Tarimo,Jonas Nambua na meneja wa misitu (TFS),ambao wanasimamishwa hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Aidha Majaliwa amekemea utozwaji wa ushuru kwa watu wanaochoma mkaa unaofanywa na halmashauri ya Rufiji kwani kwa kufanya hivyo ni kuruhusu ukataji ovyo wa miti.
Majaliwa amezuia geti (kizuizi)la Ikwiriri litoke limejaza wezi na ni lazima litoke na kuanzia sasa libaki geti la Jaribu Mpakani,Utete na Marendego.
Akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji na wananchi wa wilaya hiyo ,alisema sekta ya misitu ni tatizo kwa kila wilaya na Rufiji ni moja ya wilaya hizo .
Alisema magogo yanazalishwa bila utaratibu,na ndio wanakata miti kwenye misitu ya Utete na kupiga nyundo maeneo ya Kilwa.
Majaliwa alisema hakuna manufaa na TFS hivyo ameamua kusimamisha shughuli zote za uvunaji,katika wilaya hiyo na watumishi hao hadi wizara itakapotoa majibu.
“Kuna orodha ya vinara wa kujinufaisha na uvunaji wa misitu ambapo wamekuwa fedha wakiweka mifukoni badala ya kufikisha eneo husika wakiwemo hawa wanne wa hapa wilayani Rufiji”
“Hao nawasimamisha hadi watakapojulishwa,mtakaguliwa na atakaepona atajulishwa na magogo yote yaliyopo msituni yaratibiwe na kama kuna mtu kapata leseni taarifa itolewe na meneja wa misitu ataingia katika orodha hii’
“Nimepita njiani nimekuata magogo yanapitishwa sanjali na vigogo vidogo kwenye baiskeli ,hii ni hali mbaya ,inaonekana jinsi gani hakuna usimamizi katika suala hili”alisema Majaliwa.
Alisema wilaya ya Rufiji inaongoza katika suala la utoroshaji wa misitu na kuruhusu uvunaji holela suala ambalo halikubaliki.
Majaliwa alieleza kuwa endapo watumishi hao wangesimamia kikamilifu katika sekta hiyo basi zingepatikana fedha nyingi na hatimae kuinua maendeleo na uchumi wa wilaya.
Katika hatua nyingine alihimiza uwajibikaji na uadilifu katika maeneo ya kazi na kuwataka watumishi wabadilike na waache kufanya kazi kwa mazoea.
Majaliwa alisema hataki kuona baraza la madiwani likitumika kufuja fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo hivyo kuanzia sasa kuna kila sababu ya madiwani kusimamia bila kuzembea kwenye fedha za miradi.
Alimtaka mkurugenzi wa halamshauri na mkuu wa wilaya ya Rufiji kusimamia mapato na matumizi ya fedha ili kuongeza mapato ya halmashauri ili iweze kupiga hatua ya kimaendeleo.
Kwa upande wake mbunge wa Rufiji,Mohammed Mchengelwa ,alisema nidhamu kwa watumishi inaonekana kupungua kwa baadhi ya watumishi kwenye halmashauri hiyo.

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania