CURRENT NEWS

Friday, September 9, 2016

MAZUNGUMZO YA KITAIFA DRC, MIJADALA ISIYO NA NATIJA

Mazungumzo ya kitaifa ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanaendelea kwa ajili ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo katika hali ambayo mivutano ya kisiasa ya ndani, mapigano na ukosefu wa amani kwenye maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo bado hayajapungua.
Shirika la habari la Ufaransa limemnukuu Bertand Bisimwa, mkuu wa Harakati ya Machi 23 akisema katika taarifa maalumu kwamba mazungumzo hayo yanayoendelea mjini Kinshasa hayana uwezo wa kutatua mgogoro wa nchi hiyo. Mgogoro wa kisiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulinza tangu alipochaguliwa tena Rais Joseph Kabila kuongoza nchi hiyo mwaka 2011.
Hivi sasa kipindi cha uongozi wa Joseph Kabila kinakaribia kumalizika yaani tarehe 20 Disemba mwaka huu na hali ya kisiasa nchini humo bado si shwari. Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba, ijapokuwa washiriki wa mazungumzo ya Septemba Mosi yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika na kususiwa na idadi kubwa ya wapinzani wa Rais Joseph Kabila yangali yanaendelea, lakini baadhi ya duru zinasema kuwa, mazungumzo hayo yamevunjika.
Taasisi nyingi za kieneo na kimataifa zinasisitizia mno suala la kushirikishwa makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo kutokana na hali tete ya kisiasa iliyo nayo hivi sasa nchi hiyo kubwa zaidi ya katikati mwa Afrika. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba, mazungumzo ya kisiasa yatakayoyashirikisha makundi yote ya nchi hiyo ndiyo yenye uwezo wa kuandaa mazingira mazuri ya kufanya uchaguzi wenye itibari nchini humo.
Ijapokuwa baadhi ya duru zina matumaini ya kufanikiwa mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Umoja wa Afrika, lakini kumefanyika maandamano ya kupinga mazungumzo hayo nchini Kongo, na upinzani ni mkubwa kiasi kwamba hivi karibu polisi ya nchi hiyo iliwatia mbaroni wananchi 85 kwa kushiriki kwenye maandamano ya kupinga mazungumzo hayo.

wapinzani wa Rais Joseph Kabila wanasema kuwa, mazungumzo hayo yanafanyika kwa ajili ya kumzidishia nguvu Rais Kabila.
Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiandamana mjini Kinshasa

Wanadai kuwa Rais huyo ameitisha mazungumzo ya kitaifa ili apate nguvu ya kubakia madarakani kwa madai ya kuendesha mazungumzo hayo na hatimaye aweze pia kubadilisha Katiba ili imruhusu kugombea tena katika uchaguzi mkuu ujao. Miongoni mwa mambo yanayowatia wasiwasi wapinzani hao ni madai ya kutokuweko bajeti ya kuwaandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2017.
Mahakama ya Katiba ya Kongo imetumia madai hayo kuaikhirisha uchaguzi wa mwakani. Wafuatiliaji wa masuala ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaamini kuwa, kwa vile serikali ya Rais Joseph Kabila ina nia ya kuitisha uchaguzi wa serikali za mitaa na za mikoa kabla ya uchaguzi wa rais, wananchi wa nchi hiyo hawataweza kushiriki katika uchaguzi mwingine hadi mwaka 2018 au 2019.
Viongozi wa vyama vya kisiasa vya Kongo wanasema kuwa, hata kama Rais Kabila ametaka kufanyike mazungumzo ya kitaifa kwa lengo la kufanyika kwa usalama na amani chaguzi za nchi hiyo, lakini mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo ni mkubwa zaidi ya inavyotarajiwa, na hauwezi kutatuliwa kwa mazungumzo tu.
Inavyoonekana ni kuwa, kuheshimu matakwa ya wananchi na kuheshimu sheria ikiwa ni pamoja na kukubali Rais Kabila kuachia madaraka baada ya kumalizika vipindi vyake vya utawala kwa mujibu wa Katiba, ndiyo njia pekee za kuweza kutatua mgogoro huo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania