CURRENT NEWS

Tuesday, September 27, 2016

MBUNGE JIMBO LA RUFIJI MCHENGELWA AIKALIA KOONI RUBADA

Mbunge wa Rufiji Mohammed Mchengelwa ,akitoa taarifa na kero zinazoikabili wilaya ya Rufiji ,mbele ya Waziri mkuu wakati alipotembelea wilaya hiyo(Picha zote na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Rufiji
MBUNGE wa jimbo la Rufiji,Mohammed Mchengelwa,amemuomba waziri mkuu Kassim Majaliwa ,kuangalia uwezekano wa kuivunja taasisi inayojishughulisha na umwagiliaji na kuendeleza bonde la mto Rufiji(RUBADA)na kuipokonya majengo na ardhi waliyonayo ili ibakie kwa ajili ya tafiti za kilimo.
Amesema RUBADA imehodhi eneo la bonde hilo lenye ukubwa wa heka 500,000 pasipo kuliendeleza hivyo kuendelea kuwepo haina manufaa kwa wanaRufiji kwa kwasasa.
Aidha Mchengelwa,ameiomba serikali kushughulikia tatizo la kukatika kwa umeme wilayani hapo ambapo kwa siku hupata nishati hiyo kwa masaa manne pekee kwa takriban mwaka sasa.
Mbali ya hayo alisema hospital ya Utete inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa vifaa tiba hali inayosababisha akinamama wanaokwenda kujifungua kununua vifaa madukani kwa gharama ya zaidi ya sh. 40,000.
Mbunge huyo aliomba kutatuliwa kwa changamoto hizo ,wakati wa ziara ya waziri mkuu aliyoifanya sept 26,wilayani Rufiji katika mwendelezo wa ziara yake ya mkoani Pwani.
Mchengelwa alisema bonde la mto Rufiji lina rutuba ya kuweza kulima kilimo cha aina yoyote ikiwemo pamba hivyo endapo watawezeshwa hata vijana na jamii wataweza kutumia bonde hilo na kuinua sekta ya kilimo.
“Bunge lililopita tulipitisha sheria za tafiti za kilimo na kwa kuwa wa Marekani waliwahi kufanya tafiti katika bonde la mto huo, miaka ya nyuma na kugundua ni miongoni mwa mabonde yenye ardhi yenye rutuba kuliko eneo lolote katika afrika,ni vyema likatumiwa na wananchi kwa maslahi yao”alisema Mchengelwa.
Akizungumzia sekta ya nishati na madini alisema,inafanya viongozi wilayani hapo kugombana na wananchi kutokana na kukosa umeme wa uhakika kwani kwasasa wanapata umeme kwa masaa manne kwa siku takriban mwaka mzima uliopita.
Mchengelwa aliomba kurekebishwa mitambo iliyopo na kusema anafahamu kuna ufisadi mkubwa uliotendeka ambapo mitambo ilipekwa mitatu huku inayofanya kazi ni miwili pekee hali inayosababisha kushindwa kufanya kazi kwa siku nzima.
Kuhusu suala la migogoro ya wakulima na wafugaji  aielezea kuwa linakua siku hadi siku kwasababu ya baaadhi ya watumishi wa halmashauri,wenyeviti wa vijiji na watendaji kuchukua rushwa na kuingia idadi ya mifugo ambayo hairuhusiwi.
Mchengelwa alisema tatizo la migogoro hiyo ni sugu na kubwa kuliko ni kuchangiwa na viongozi na watendaji wenyewe kujihusisha kuingiza mifugo hiyo na kupelekea kukua kwa changamoto hiyo.
“Kuna mifugo 200,000 na uwezo wa ardhi ya Rufiji ni kuwa na mifugo 50,000 pekee,nidhamu ikiboreshwa kutapatikana idadi ya mifugo inayolingana na wilaya”alisisitiza .
Nae diwani wa Utete,Hawa Mtopa,alieleza kuwa serikali iwasaidie kupeleka vifaa na kuboresha huduma katika wodi ya uzazi- hospitali ya Utete.
Alisema akinamama wanagharamia huduma za uzazi zaidi ya 40,000 kwa kila kitu na ni lazima wanunue dukani hivyo akinamama wenye maisha ya kawaida kushindwa kumudu gharama hizo.
Hawa alisema hospitali hiyo imejengwa miaka ya 60 lakini huduma zake ni haba hivyo kusababisha akinamama na wazee kupata tabu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo,Juma Njwayo alisema wilaya imejiwekea mkakati wa kuwaondoa kwenye uongozi viongozi wa vijiji na watendaji wanaohusika kuingiza mifugo kwenye maeneo yao.
Akitolea ufafanuzi juu ya maombi na kero alizotolea taarifa mbunge Mchengelwa,waziri mkuu Kassim Majaliwa,alisema serikali haiwezi kuvumilia miradi isiyo na tija kama wa RUBADA.
Alielezea kuwa mapema kuanzia sasa kutafanyiwa uchunguzi juu ya mradi huo na ambae atabainika kufanya ubadhilifu atawajibishwa.
Akizungumzia juu ya migogoro ya wakulima na wafugaji alisema kiongozi ama mtumishi atakayejihusisha na uingizwaji wa mifugo kiholela achukuliwe hatua na kuondolewa katika uongozi.
Kuhusu umeme Majaliwa ,aliwataka ananchi wawe watulivu na serikali itamaliza suala hilo kwa kuongeza jenereta jingine ili kuwepo na umeme wa kutosha.
Alisema tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara limetokana na majenereta yanayotumika ni mawili hivyo umeme unaokuwepo ni mdogo hasa baada ya REA kuongeza vijiji  na kusababisha ongezeko la mahitaji ya nishati hiyo.
Majaliwa  alisema serikali imefanya utaratibu kuwa jenereta lisilofanya kazi lirudishwe kwa mkandarasi aliyoyapeleka ili abadilishe na kupelekwa jingine.
Waziri mkuu yupo kwenye ziara yake mkoani Pwani,ambapo alianza septemba 23 wilayani Mafia,septemba 28 anatarajiwa kuwa wilaya mpya ya Kibiti na atamalizia wilayani Mkuranga.

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania