CURRENT NEWS

Wednesday, September 14, 2016

MSHAMA:WAFUGAJI KATA YA KWALA WAONDOKE NDANI YA SIKU 30

MKUU wa wilaya ya Kibaha ,mkoani Pwani,Assumpter Mshama ,akizungumza na wakulima  na wafugaji wa Dutumi na kata ya Kwala  wilayani hapo. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama,akimsikiliza mkulima Tausi Maulid, aliyeliwa mazao yake na mifugo  ya Dotto Mabula huko kijiji cha Madege kata ya Dutumi.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Mfugaji  huko Dutumi wilayani Kibaha ,Samwel Robert ,akizungumza jambo mbele ya mkuu wa wilaya hiyo ,Assumpter Mshama aliyekwenda kutembelea eneo hilo na Kwala  kujua kero ya wakulima na wafugaji.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

MKUU wa wilaya ya Kibaha,mkoani Pwani ,Assumpter Mshama ametoa mwezi mmoja kwa wafugaji wa kata ya Kwala kuondoka,katika kata hiyo kwani hakuna eneo lililotengwa kwa ajili yao.

Aidha alisema wafugaji waliopo kihalali katika maeneo mengine ya wilaya hiyo wanatakiwa kuheshimu wakulima na endapo yupo atakaeingiza mifugo katika shamba la mkulima atatakiwa kulipa ng’ombe kulingana na hasara iliyopo.

Assumpter ametoa pia siku 30 kwa wafugaji waliopo kisheria kuweka alama kwenye ng’ombe zao huku akivitaka vijiji vitenge maeneo ya wakulima na wafugaji .

Aliyasema hayo wakati akizungumza na pande hizo mbili ,katika ziara yake aliyoianza kutembelea vijiji na maeneo yenye migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani hapo.

Akizungumza kwenye ziara yake Dutumi na Kwala ,alisema maamuzi hayo yatakuwa dawa na muarobaini wa tatizo hilo.

Assumpter alisema kwasasa barua rasmi zinaandaliwa kwa ajili ya kuwapatia wafugaji hao ikiwa ni taarifa na kumbukumbu.

Aliwataka maafisa mifugo kuitisha mikutano ya wananchi kutunga sheria ndogondogo zitakazobana makundi hayo.

Alisema serikali haiwezi kuvumilia kuona kundi moja linaumiza vichwa vya watu na kujigeuza wababe kuvunja amani na kujenga hofu ndani ya jamii.

“Kuanzia sasa ng’ombe ni halali ya mkulima ,ama watakaokamatwa  watauzwa na mfugaji kuchukuliwa hatua “

“Wasithubutu kunijaribu,najua wafugaji wanamtandao ndio maana wanaingia kila kukicha sasa kwa Kibaha basi inatosha ,sitaki kuona wafugaji wapya”alisema Assumpter.

Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa yeyote mwenye kosa ni lazima achukuliwe hatua kama kuna mfugaji hata mkulina anamkosea mwenzie.

Assumpter alisema mfugaji atakaekamatwa ng’ombe zake na kuziacha kwa siku 7  watatakiwa kupigwa mnada.

Alieleza kuna kila sababu ya kuheshimiana na kuishi kwa amani kwa pande hizo zote mbili pasipo kujipa hofu na kutishiana amani bila msingi.

Akiwa Dutumi Assumpter alitoa siku saba kwa wafugaji walioingia bila utaratibu kurudi makwao walipotokea na kupisha ardhi ya mji huo.

Alisema utajiri wa wafugaji usiwe chanzo cha kudhalilisha wakulima ambapo serikali imeshachoshwa na wimbo wa migogoro hiyo usiokwisha.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha,Tatu Selemani aliasa baina ya makundi hayo kuheshimu mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Alisema kwa upande wa kata ya Kwala hakuna eneo la wafugaji hivyo ni lazima wahame.

Tatu alisema,hakuna wafugaji waliopokelewa katika kata hiyo na kwamba wahamishe mifugo kwenye mikoa na maeneo mengine.

Alifafanua kuwa Dutumi kuna ng’ombe 4,195 na kulitengwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kuaniza mwaka 2014 ambao uataisha mwaka 2024.  

Mfugaji kutoka Dutumi Samwel Robert ,alisema ng’ombe wengi wametokea ngambo na ni wafugaji wavamizi.
Alisema kundi hilo linatokea Kisarawe,wasukuma na Morogoro –Kilosa kwahiyo serikali iangalie hilo.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania