CURRENT NEWS

Monday, September 12, 2016

NDIKILO:APIGA STOP KUINGIZA MIFUGO MIPYA MKOANI PWANIMkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza na wajumbe wa kikao cha ushauri cha mkoa huo (RCC)kuhusiana na mipango na mkakati mbalimbali ya kuendeleza maendeleo ya kimkoa.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,amesema hataki kuona mifugo mipya ikiingizwa mkoani hapo,kwani iliyopo inatosha na inasababisha mkoa kuhemewa na kupelekea migogoro isiyo na tija.
Amewataka watendaji viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya kijiji,kata ,wilaya na wakurugenzi,kuwa wakali na kusimama kidete kukomesha uingiaji holela wa mifugo katika maeneo yao.
Mhandisi Ndikilo,amesema baadhi ya viongozi ngazi ya kijiji wanadaiwa kuwa chanzo na kula sahani moja na kugeuza mtaji wa kuingiza mifugo hiyo hivyo atakaebainika atawajibishwa.
Aidha ameeleza kuwa changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo ni kubwa na tishio hivyo amewataka maafisa tarafa,wakuu wa wilaya,makatibu tawala wilaya,mahakama,wakurugenzi wa halmashauri na wenyeviti na watendaji wa vijiji na kata kutofanya mzaha.
Akizungumza katika kikao cha ushauri mkoa wa Pwani,(RCC)mhandisi Ndikilo, alisema mkoa huo kwasasa una jumla ya ng’ombe 505,788 wakati eneo la malisho lilitengwa ni hekta 498,001 ambalo lina uwezo wa kuchukua ng’ombe 249,002 pekee.
Alisema ng’ombe 236,718 ndio wanaoleta tafrani katika mkoa wa Pwani ambapo wanasababisha migogoro ya wakulima na wafugaji hususan wilaya ya Bagamoyo,Rufiji,Kibaha Vijijini ,Kisarawe na Rufiji.
Mkuu huyo wa mkoa ambae pia ni mwenyekiti wa kikao hicho,aliwataka wakurugenzi kuacha kuwa waoga wa kuwawajibisha ama kuwafukuza watendaji wa vijiji ambao wanatajwa kushiriki kuingiza mifugo kwenye maeneo yao pasipo utaratibu .
Alisema wakurugenzi wawe wakali kwani suala hilo sio la kuchezea hivyo kuna kila sababu ya kuondoa viongozi ambao wanasababisha migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mhandisi Ndikilo ,alieleza wakuu wa wilaya nao waanze sasa kufukuza kazi wale ambao hawawajibiki na kusema kwa kuwafumbia macho ni kujipalia mkaa wenyewe na uongozi wa mkoa.
Alitoa rai kwao kuvunja hata serikali za kijiji ambacho kinaonekana kwenda kinyume na mikakati na mipango ya serikali .


“Tatizo la wakulima na wafugaji chanzo ni mifugo kuwa mingi na kuondoka kwenye maeneo yao ya malisho na kupelekea kuingia kwenye maeneo ya wakulima “
“Kwa hili haina budi kupiga stop uingizwaji wa mifugo mipya ili kutupa muda wa kushughulikia kesi zilizopo na kupunguza tatizo ambalo limekuwa kero kubwa kimkoa”alisema mhandisi Ndikilo.
Hata hivyo mhandisi Ndikilo,alisema wakulima na wafugaji ni tatizo kubwa mkoani hapo kwani kila kukicha ni migogoro baina yao.
“Ni suala zito hili watu wanafikia hatua ya kutandikana mikuki,kupigana na kubakana huko maeneo ya Makurunge na Kimange yaani kama Bagamoyo ndio hali mbaya ,DAS Erika Yegella na DC Majid Mwanga msilale simamieni hili ,nendeni kwenye matukio kuyashughulikia”aliagiza mhandisi Ndikilo.
Aliomba kamati za ulinzi na usalama ,wakurugenzi na wakuu wa wilaya wasimamie amani na utulivu ndani ya jamii ili mkoa uendelee kuwa salama na kushughulikia masuala ya wakulima na wafugaji ili kuleta amani katika pande hizo.
Mhandisi Ndikilo,hakusita kuziomba mahakama kumaliza kwa wakati kesi za wakulima na wafugaji kwani ni kesi nyingi zimejaa mahakamani bila matokeo.
Alisema haiwezekani kesi zinazidi kuongezeka ,wakulima na wafugaji wanzidi kudhuliana huku mahakama zikiwa hazioni hilo.
Nae kamanda wa polisi mkoani Pwani ,Boniventure Mushongi,alisema jeshi la polisi mkoa linashughulikia na kusimamia malalamiko yanayofikishwa kwao na kuchukua hatua za kupelekea mahakamani.
Alisema hadi sasa kuna kesi walizopeleka mahakamani ambapo wilaya ya Kibaha kuna kesi 21,Mkuranga 3 ,Bagamoyo 6,Kisarawe 11 ,Rufiji 165 na Chalinze 52.
Alisema kati ya kesi hizo zote hakuna hata mtu mmoja ambae ameweza kufungwa ama kuchukuliwa hatua za kimahakama.
Kamanda Mushongi,alieleza wakulima ni tatizo kutokana na wenywe kupenda kumaliza kesi zao na wafugaji majumbani kwa kupatiwa fidia za 200,000 ama 300,000 na hatiamae kuongeza matatizo.
Alisema wakati mwingine wanawauzia maeneo wafugaji hao kwenye maeneo yao ama wenyeviti wa vijiji wanawauzia heka hadi 50 za vijiji kwahiyo inakuwa ngumu kuwaondoa wakati wameuziwa maeneo na ni miongoni mwa wanavijiji.
Kwa upande wake meneja wa wakala wa barabara mkoani Pwani,Tumaini Sarakikya alisema mifugo ni tatizo kubwa kwani huharibu miundombinu ya barabara.
Alisema mifugo hiyo hupitishwa katikati ya barabara kuu ya Dar es salaam –Morogoro na kuharibu barabara kwa kutoboatoboa ama kubonyea kwenye baadhi ya barabara hiyo.
Sarakikya alisema hatua za serikali ya mkoa kudhibiti kuhusiana na kero hiyo itasaidia hata barabara hasa za lami kuendelea kudumu kwa kipindi kirefu.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania