CURRENT NEWS

Thursday, September 22, 2016

NEC YAANZISHA PROGRAMU ENDELEVU ZA KUTOA ELIMU YA MPIGA KURA.Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akizungumza na waandishi wa Habari mjini Musoma kuwaeleza mkakati wa NEC wa kuwafikia wananchi moja kwa moja kuwapatia elimu ya mpiga kura.


Na. Aron Msigwa – NEC, Musoma

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kutekeleza programu endelevu za kutoa elimu ya mpiga kura ili kuwaelimisha wananchi waliofikisha umri wa kupiga kura kutekeleza wajibu na haki waliyonayo kikatiba ya kupiga kura katika chaguzi zijazo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani wakati akizungumza na waandishi wa Habari mjini Musoma kuhusu mkakati wa NEC wa kuwafikia wananchi moja kwa moja kuwapatia elimu ya mpiga kura.

Amesema kuwa Tume hiyo imeanza kutoa elimu hiyo kwa kushiriki maonesho na mikutano mbalimbali ukiwemo mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika mjini Musoma kuanzia Septemba 22 hadi 24 mwaka huu. 

“Tumeamua kushiriki kwenye mkutano huu kwa kuwa hawa ni watendaji wa Serikali katika ngazi za mitaa, tumekuja kutoa elimu ya mpigakura kwani suala la elimu tunalipa kipaumbele” Amesema Bw. Kailima.

Amesema Tume imeandaa programu ya kuwafikia wapiga kura moja kwa moja kwa kuweka mkakati wa kuhudhuria mikutano yote ambayo iko kihalali ikijumuisha ile ya Mawaziri na Naibu Mawaziri , Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.

Amebainisha kuwa tayari NEC imewasiliana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili iweze kupata ratiba ya vikao vya kamati za ushauri za mikoa na wilaya ili iweze kupata fursa ya kutoa elimu ya mpiga kura ndani ya vikao hivyo.

Aidha, amefafanua kuwa Tume imemwomba Katibu Mkuu TAMISEMI ratiba ya vikao vya Mabaraza ya madiwani ya halmashauri zote nchini kwa lengo la kuwezesha wataalam wa Tume hiyo kutoa elimu ya Mpiga kura.

“Tumemwomba Katibu Mkuu TAMISEMI atusaidie kuweka ajenda ya kudumu kuhusu utaratibu mzima wa uendeshaji wa uchaguzi na uelimishaji wa mpiga kura kwenye vikao vya mabaraza ya Madiwani ambapo maafisa wa Tume walio katika ngazi za halmashauri watapata fursa ya kutoa elimu ya mpiga kura katika vikao hivyo” Amesisitiza.

Ameeleza kuwa NEC imejipanga kupanua wigo wa utoaji wa habari kupitia vyombo vya habari hasa Televisheni,Redio, Magazeti na Mitandao ya kijamii ili kuwawezesha wananchi wengi kupata elimu ya mpiga kura na taarifa sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi na majukumu yake.

“Tumejipanga kutumia vyombo vya habari, kila wiki tutakuwa na taarifa na mada fupifupi zinazohusu mchakato mzima wa uchaguzi kwa maana ya uandikishaji na zoezi zima la upigaji kura kujenga uelewa kwa jamii nzima kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi” Amefafanua.

Amesema kuwa kifungu Na 4 (c) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 kinaelezea wazi kuwa pamoja na mambo mengine Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina jukumu kutoa elimu ya Mpiga kura, kuratibu Taasisi na watu wenye uwezo wa kutoa elimu ya mpiga kura ili kuongeza uelewa miongoni mwa jamii.

“Tunategemea kuanzia mwanzoni mwa mwezi Oktoba tutatoa tangazo la kuzialika Asasi na taasisi zinazotaka kutoa elimu ya mpiga kura ziwasilishe maombi yao Tume ya Uchaguzi pamoja na zana zao za kutolea elimu ili tuweze kuwapatia kibali cha miezi 6 na baadaye tutafanya tathmini juu ya ufanisi wa kazi wanayoifanya” Amebainisha Bw. Kailima.

Amesema lengo la kuzishirikisha taasisi na Asasi hizo ni kuondoa ombwe lililokuwa linaonekana la utoaji wa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi pekee kwa kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kila wakati ili kuongeza uelewa wa wananchi katika chaguzi zijazo.

Aidha, amesema NEC imeandaa mpango mpya wa kuzifikia shule mbalimbali za Sekondari hapa nchini utakaowawezesha wanafunzi wa shule zitakazochaguliwa kuwa na Klabu za elimu ya mpiga kura.

Amesema programu hiyo itaiwezesha Tume kuwaelimisha wanafunzi waliofikisha umri wa kupiga kura na wale ambao bado hawajafikia umri huo ili kujenga uelewa wao kuhusu elimu ya Mpiga kura.

“Tumeanza program hii kwa kuzitembelea shule mbili za Sekondari za Isange (wasichana) na Shule ya Ufundi Musoma zilizo katika Manispaa ya Musoma, tutaongea na wanafunzi ambao wamefikia umri wa kupiga kura lakini bado hawajajiandikisha kupiga kura na wale ambao bado hawajafikisha umri wa kupiga kura, tumenalenga kuanzisha klabu ya Elimu ya mpiga kura kwenye shule moja katika kila wilaya ya Tanzania” Amesema.

Amefafanua kuwa kuanzishwa kwa klabu hizo kutawawezesha wanafunzi kujadiliana kwa kina kuhusu mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura kwa mujibu wa sheria iliyopo ili kufikia lengo la kuwa na shule moja yenye Klabu ya elimu ya mpiga kura katika kila wilaya ifikapo Januari 2020.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania