CURRENT NEWS

Friday, September 16, 2016

SERIKALI INA UWEZO WA KUGUNDUA BARABARA IILIYOJENGWA CHINI YA KIWANGO

Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma
Serikali ina uwezo wa kugundua barabara iiliyojengwa chini ya kiwango kwa kukagua miradi inayotekelezwa wakati wote wa ujenzi wa miradi hiyo hata baada ya kukamilika kabla ya muda wa ukaguzi wa mwisho kupita.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani alipokuwa akijibu swali la Miza Bakari Haji Mbunge wa Viti Maalum lililohoji kama Serikali inaweza kugundua ni barabara ngapi zilizotengenezwa chini ya kiwango nchini.

Mhandisi Ngonyani alizitaja barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami ambazo zilikuwa matatizo mbalimbali kabla ya muda uliotarajiwa kuwa ni pamoja na Kilwa ambayo inaanzia Mbagala Rangi Tatu hadi Bendera Tatu, Sekenke hadi Shelui, Kyamorwa hadi Buzirayombo na Nangurukuru hadi Mbwemukulu.

Barabara hizo zilipokamilika yalijitokeza matatizo mbalimbali kabla ya muda uliotarajiwa yanayotokana na mapungufu kwenye ubora kama mashimo katika barabara hizo na kuharibika kwa tabaka mbili za juu.

Mhandisi Ngonyani amesema kuwa ujenzi wa barabara hutengenezwa kwa kuzingatia mikataba kati ya TANROADS na Mkandarasi na kati ya TANROADS na Mhandisi Msimamizi na viwango vinavyotakiwa kwenye ujenzi wa mradi huo wa barabara vimetajwa kwenye mkataba husika.

“Endapo kunatokea tatizo lolote kuhusu ubora wa kazi, kwa mfano barabara kujengwa chini ya kiwango, vipengele vya mkataba husika vitatumika kubaini nani aliyesababisha mapungufu hayo kati ya Mkandarasi, Mhandisi Msimamizi au mwajiri na hatimaye kuwajibika” alisema Mhandisi Ngonyani.

Katika kudhibiti nidhamu ya kuheshimu mikataba, Mhandisi Ngonyani alisema kuwa kutokana na mapungufu yaliyojitokeza katika mradi wa ujenzi wa barabara husika hatua zilichukuliwa kulingana na vipengele vya mikataba husika na Mkandarasi wa miradi hiyo walirekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika barabara hizo kwa gharama zao wenyewe.

Wingi wa magari nao umeainishwa kuwa ni sababu nyingine ambayo inasababisha uharibifu wa barabara kutokana na wingi wa magari makubwa ya mizigo yanayotumia ekseli zenye tairi moja.

Ili kuhakikisha uthibiti wa uzito wa magari, Serikali inafanya utaratibu wa kufanya mabadiliko ya kanuni za usalama barabarani za mwaka 2001 ziweze kuoana na Sheria ya Uthibiti wa uzito wa magari ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ambayo imeweka kiwango cha uzito wa tani 8.5 kwenye ekseli zenye tairi moja.

Akijibu swali la Mbunge wa Nanyumbu Mhe. Dua William Nkurua aliyehoji ni lini Serikali itatekeleza miradi ya barabara wilaya ya Nanyumbu, Mhandisi Ngonyani alisema kuwa Wakala wa Barabara Tanzania imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Nangomba hadi Nanyumbu hatua ambayo itasaidia kujengwa kwa barabara hiyo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania