CURRENT NEWS

Wednesday, September 28, 2016

Serikali kununua ndege nyingine mpya mbili aina ya JET


Moja ya ndege mpya za abiria ya Bombadier- 8 Q400 iliyonunuliwa na Serikali kutoka nchini ikiwa katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Jijini Dar es Salaam.  Ndege hizo zinatarajia kufanya safari zake katika mikoa 12 nchini pamoja na Nchi ya Comoro.


 Rais Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ndege mpya za abiria aina ya Bombedier- 8 Q400 zilizonunuliwa na Serikali kutoka nchini Canada.  Wengine katika picha kutoka kushoto ni Balozi wa Canada nchini, Ian Myles na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Spika wa Bunge, Job Ndugai pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.


 Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akiwekeana saini ya makabidhiano ya ndege mpya za abiria aina ya Bombadier- 8 Q400 baina yake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamuhilo wakati wa hafla ya uzinduzi wa ndege hizo leo Jijini Dar es Salaam.


 Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akipeana mkono na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Dkt. Leonard Chamuhilo mara baada ya kuwekeana  saini ya makabidhiano ya ndege mpya za abiria aina ya Bombadier- 8 Q400 zilizonunuliwa na Serikali kutoka nchini Canada, wakati wa hafla ya uzinduzi wa ndege hizo leo Jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya Marubani wa ndege mpya za Serikali aina ya Bombadier -8 Q400 zilizonunuliwa kutoka nchini Canada wakifualtilia kwa makini hotuba mbalimbali za Viongozi wa Serikali wakati wa hafla ya uzinduzi wa ndege hizo leo Jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Wananchi Tanzania Tanzania (JWTZ) Canada wakifuatilia kwa makini hotuba mbalimbali za Viongozi wa Serikali wakati wa hafla ya uzinduzi wa ndege hizo leo Jijini Dar es Salaam.


   Baadhi ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa ndege mpya za Serikali aina ya Bombadier – 8 Q400 zilizonunuliwa nchini Canada, wakati wa hafla iliyofanyika katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere leo Jijini Dar Salaam.

Baadhi ya Wajumbe wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wakifuatilia jambo wakati wakati wa hafla ya uzinduzi wa ndege mpya za Serikali aina ya Bombadier- 8  Q400 kutoka nchini Canada

Kikundi cha Ngoma kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikitumbuiza Viongozi na wananchi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa ndege mpya za Serikali aina ya Bombadier – 8 Q400 kutoka nchini Canada leo Jijini Dar es Salaam.

    Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Salum Hapi wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa ndege mpya za Serikali aina ya Bombadier- 8 Q400 zilizonunuliwa na Serikali kutoka nchini Canada.

  Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mkewe Mama Janet Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi na Mawaziri mara baada ya hafla ya uzindzi wa ndege mpya za abiria aina ya Bombadier – 8 Q400 zilizonunuliwa na Serikali kutoka nchini  Canada.


     Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na marubani wa ndege mpya za abiria zilizonunuliwa na Serikali kutoka nchini Canada aina ya Bombadier – 8 Q400 mara baada ya kuzinduliwa rasmi leo Jijini Dar es Salaam.
 Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali mara baada ya uzinduzi  wa ndege mpya za abiria zilizonunuliwa na Serikali kutoka nchini Canada aina ya Bombadier- 8 Q400 leo Jijini Dar es Salaam.

(Picha na Ismail Ngayonga)


Na. Sheila Simba

Dar es Salaam

RAIS  John Magufuli amesema Serikali imejipanga kununua ndege mbili  aina Jet zenye uwezo wa kubeba abiria 160 na 242 pamoja na kutenga Tsh. Bilioni 100 kwa ajili ya ukarabati viwanja vya ndege nchini.


Amesema hayo leo Jijini Dar Es Salaam wakati wa uzinduzi wa ndege mpya mbili za abiria aina ya  bombardier – 8 Q400 zilizonunuliwa na Serikali kutoka nchini Canada ,na kuongeza kuwa ndege hizo zitasaidia kuboresha sekta ya usafiri wa anga nchini.


“Ndege hizi ni nzuri sana, kwani ukitaka kujenga nchi yenye uchumi wa kisasa huwezi kujenga bila kuwa na ndege na ukitaka watalii lazima uwe na ndege” alisema Rais Magufuli

Alisema  kuwa ndege hizo mbili zitakazonunuliwa na Serikali zitakuwa na uwezo wa kubeba kusaidia watalii kuja nchini moja kwa moja bila kutua nchi nyingine.


“Tunataka watalii wanaokuja nchini kuja moja kwa moja bila kushuka nchi nyingine ili kuongeza mapato yetu na kukuza utalii duniani na kuwa na ndege nyingi zaidi kama nchi nyingine” alisema Rais Magufuli.


Akizungumzia ubora wa ndege za bombardier alisema kuwa ndege hizo zinaenda na mazingira ya hapa nchini na zina uwezo wa kutua katika viwanja vyenye lami na vile ambavyo havina lami na uendeshaji wake ni wa gharama nafuu.


Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema kuwa ndege za bombardier zinatumia mafuta kidogo ikiwemo gharama ya tsh Milioni 1 za mafuta kwa safari moja ikilinganisha na ndege nyingine zenye kutumia tsh. Milioni 28 kwa safari.


Rais Magufuli aliitaka bodi ya shirika la ndege Tanzania (ATCL) kufanya kazi nzuri ya kusimamia ndege hizo na kutoa huduma nzuri na kuhakikisha wanapata faida ili serikali waweze kununua ndege nyingi zaidi.


Alisema kuwa bodi ya ATCL wana kazi kubwa ya kufanya kuboresha shirika hilo, kutokana na uzembe wa wafanyakazi wake kutokuwa makini na kuwataka kupanga vizuri safari za ngede hizo kwani zina uwezo wa kwenda mpaka nchi jirani.


“lazima mjue mnaingia kwenye ushindani na washindani wenu hawawezi kufurahia wapo hujuma ili shirika lisisonge mbele sasa fanyeni kazi”alisema Magufuli.


Aidha amewaomba ATCL kutotumia mawakala katika kukatisha tiketi na kuzingatia muda wa safari ulipangwa na kutoa huduma nzuri kwa wateja wao ili kukuza utalii nchini  na kuwaomba watanzania kuwa wazalendo kwa kutumia usafiri huo.


Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa alisema ndege hizo zilizozinduliwa zinauwezo wa kubeba abiria 76 na abiria 6 wakiwa ni wa daraja la biashara na 70 ni daraja la kawaida na ina uwezo wa kubeba mzigo wa tani moja.


Ameongeza kuwa shirika la ATCL lina upungufu mkubwa wa watalaamu katika maeneo mbalimbali ikiwemo, marubani, wahandisi, wanasheria, maafisa biashara, wahasibu na menejimenti na hatua inayosabisha shirika hilo kushindwa kujiendesha vizuri.


Waziri Mbarawa alisema kuwa ATCL wamejipanga kutoa huduma za usafiri katika viwanja vya Dodoma, Dar Es Salaam Bukoba, Tabora, Zanzibar, Mbeya, Kilimanjaro, Mtwara, Mwanza Kigoma, Arusha na Comoro.
    

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania