CURRENT NEWS

Friday, September 30, 2016

SERIKALI YATOA RAMBIRAMBI KWA WAFIWA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGERA

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu akiongea na wawakilishi wa familia waliopoteza ndugu zao (hawapo pichani) kwa tetemeko la ardhi lililotokea mapema Septemba 10 mwaka huu Bukoba mjini wakati wa kukabidhiwa rambirambi iliyotolewa na Serikali milioni 17 pamoja na kampuni ya simu ya Halotel ambayo imetoa shilingi milioni 15.kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Maafa.
Yusta Jonas mkazi wa Hamugembe Manispaa ya Bukoba akipokea rambirambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ambayo imetolewa na Serikali pamoja na kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.
Mzee Vedasto Kato kutoka mtaa wa Hamgembe Manispaa ya Bukoba akipokea rambirambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ambayo imetolewa na Serikali pamoja na kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu (katikati aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa wanafamilia waliofiwa na ndugu zao wakati wa tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka huu. (Picha na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba)

Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba

Familia 15 zilizofiwa na ndugu zao 17 wakati wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani wa Kagera zimepokea rambirambi ya jumla ya shilingi milioni 32 ikiwa ni mkono wa faraja kwa msiba uliwafika familia hizo na taifa kwa ujumla.

Rambirambi hiyo imetolewa mjini Bukoba na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kwa niaba ya Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya simu za mkononi nchini ya Halotel ili kuwashika mkono wafiwa hao kwa kupoteza ndugu na jamaa zao.

Katika rambirambi hiyo, Serikali imetoa shilingi milioni 17 na kampuni ya simu ya Halotel imetoa shilingi milioni 15 ambapo kila familia ya mfiwa amepokea shilingi 1,000,000 kutoka Serikalini na shilingi 885,000 kutoka kampuni ya Halotel.

Hatua hiyo inapelekea kila familia ya mfiwa kupokea jumla shilingi 1,885,000 ambapo familia mbili zilizopoteza ndugu zao wawili wawili wamepokea jumla ya shilingi 3,770,000 ikiwa ni rambirambi kwa kila ndugu aliyefariki wakati wa tukio hilo la tetemeko la ardhi.

Akikabidhi rambirambi hiyo kwa familia hizo, Mkuu wa Mkoa wa huo akiwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa mkoa Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amesema kuwa Serikali imetoa rambirambi hiyo kwa lengo kuwapa pole wafiwa hao kutokana na kuwapoteza ndugu na jamaa zao wakati wa tetemeko hilo lililotokea  Septemba 10, mwaka huu.

Katika kuwahakikishia usalama na utunzaji wa fedha walizopokea wafiwa hao, Mkuu wa mkoa huo amewaasa wasikuwa na akaunti wafungue akaunti katika benki yeyote ili waweze kuziweka fedha hizo walizopokea ili kuwahakikishia usalama badala ya kutembea nazo mkononi.

Wawakilishi wa familia zilizopokea rambirambi hiyo ni pamoja na Vedasto Katto (Hamugembe), Geofrey Gerald (Mafumbo), Alex Felix (Hamugembe), Orestus Aron (Hamugembe), Justa Mkalisa Jonas (Hamugembe), Albert Tibangayuka (Barabara ya Sokoine), Sheikh Mikidadi Abdallah (Hamugembe) na Maria Stella John (Hamugembe).

Wanafamilia wengine waliopokea rambirambi ni Swidick Miyonga (Hamugembe), Jackson Evason (Rwamishenye), Jasson Rugemalila (Rwome), Augustine Muhigi (Rwome), Edson S. Rwetabula (Kashenye), Anitha Evalista (Omurushaka) na John Mulokozi Kahangwa (Kanyigo-Kikukwe).

Aidha, mkuu huyo wa mkoa ameishukuru Kampuni ya simu ya mkononi ya Halotel kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutoa rambirambi na kuwafuta machozi familia za marehemu hao na kuwahakikishia kuwa Serikali inathamini mchango wao kwa jamii.

Akitoa neno la shukrani mara baada ya kupokea rambirambi hiyo kwa niaba ya wafiwa wenzake, Mzee Vedasto Kato kutoka mtaa wa Hamgembe Manispaa ya Bukoba ametoa shukrani kwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona haja ya kuwashika mkono baada ya kupoteza ndugu zao.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutujali wafiwa tuliopoteza ndugu zetu wakati wa tetemeko la ardhi lililotokea katika mkoa wetu mwezi huu na kutuonea huruma katika kipindi hiki kigumu kilichotuachia majonzi makubwa katika familia zetu” alisema mzee Vedasto.

Mzee Vedasto amesema kuwa hatua iliyochukuliwa na Serikali katika kuwapa mkono wa pole imewapa faraja na ameiomba Serikali kuendelea kuwajali wananchi wake kama ilivyokuwa kwao.

Tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera mapema mwezi huu, limesababisha vifo ambapo wananchi 17 waliopoteza maisha yao, majeruhi 440 ambao walitibiwa katika vituo mbalimbali vya afya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.


Pamoja na rambirambi hiyo, Serikali pia iliwahudumia marehemu waliopoteza uhai wakati wa tukio hilo kwa kutoa majeneza pamoja na usafiri wa kusafirisha miili ya marehemu hao kutoka Bukoba mjini hadi kwenye maeneo ambayo familia zao walipo ambapo yalipofanyika maziko ya wapendwa wao.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania