CURRENT NEWS

Friday, September 9, 2016

TANZANIA NA CHINA ZAANZA MAZUNGUMZO YA KUWAWEZESHA WAFANYABIASHARA WADOGO

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Serikali imeanza mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya China kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati Afrika ikiwemo Tanzania.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Susan Kolimba alipokuwa akijibu swali la Mhe. Munde Tambwe lililohusu mkakati wa Serikali kupitia diplomasia ya uchumi na nchi ya China kuunganisha wajasiriamali wadogo.
Dkt. Kolimba amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 4 barani afrika ambazo Serikali ya China imechagua kuwekeza viwanda vyake katika miaka mitatu ijayo.
Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa, Serikali ya china imeanzisha mfuko maalumu wa fedha kwa ajili ya kuwezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati wa afrika ambapo Serikali ya Tanzania imeshafanya mazungumzo na Benk ya maendeleo ya China.
“Serikali imeanza mazungumzo na benki ya maendeleo ya china kwa ajili ya kuwezesha mabenki nchini yaweze kukopa fedha hizo na hatimaye kuweza kuwakopesha wajasiriamali wetu wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya viwanda kwa kushirikiana na wenzao wa china,” alifafanua Dkt. Kolimba.
Aidha, amesema kuwa matarajio ya Serikali ni kuona mabenki nchini yanakidhi vigezo na masharti ya kuchukua fedha kutoka Mfuko wa China ili watanzania waanze kupata mitaji mapema iwezekanavyo.
Mbali na hayo Balozi wa Tanzania nchini China umekuwa ukishawishi wafanyabiashara kutoka china kuwekeza nchini nan a kuandaa ziara za makampuni mbalimbali ya China kutembelea kituo cha uwekezaji (TIC) nchini.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania