CURRENT NEWS

Sunday, September 18, 2016

UTOKOMEZAJI WA TB, UKIMWI NA MALARIA UENDE SANJARI NA UTEKELEZAJI WA SDG'S:BAN

Ban Ki-moon Montreal Canada:Picha na Global Fund

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema lengo la fuko la kimataifa la kupambana na ukimwi , kifua kikuu na malaria lijulikanalo kama Global Fund, ni kuhakikisha hakuna yeyote anayesalia nyuma bila kujali wapi atokako, ni kabila gani au anafuata imani gani.
Na hivyo anajivunia juhudi za Umoja wa Mataifa zilizofanyika na zitakazoendelea kufanyika katika kusaidiana na mfuko huo. Ban ameyasema hayo katika mkutano wa tano wa kutunisha fuko la kimataifa , Global Fund unaofanyika mjini Montreal Canada leo Jumamosi.
Ametoa wito wa mshikamano kwa miaka 15 ijayo ili kufikia malengo 17 ya maendeleo endelevu yaani SDG's kwa ajili ya kila mtu kila mahali kwani malengo hayo yanajikita katika kuhakikisha usawa wa kijinsia, haki za binadamu, maji na usafi, elimu, utawala bora, amani na utulivu. Na hivyo

Kufanya kazi kutokomeza HIV, kifua kikuu (TB) na malaria ni sifa kuu ya malengo ya SDGs, na kila lengo lina wajibu wa kuhakikisha maisha yenye afya na kuchagiza maisha bora kwa wote na katika rika zote."
Ameongeza kuwa ndio maana ripoti ya Global Fund inasisitiza umuhimu wa shule na usawa wa elimu, fursa sawa kwa wasichana vigori kuzuia HIV, na ndio sababu ni lazima kuboresha hali ya maisha kwenye mitaa ya mabanda iliyofurika mijini kupambana na kifua kikuu, na kushughulikia udhibiti wa maji na usafi ili kukomesha malaria.
Amesema zaidi ya asilimia 40 ya uwekezaji wa Global Fund ni katika kuimarisha mifumo ya huduma za afya na kuna mkakati wa kuongeza asilimia hiyo. Amewachagiza wadau kujitoa kimasomaso kutunisha mfuko huo na walioahidi kutimiza ahadi zao kwani

"Tuna ufahamu na nyenzo za kutokomeza HIV, TB na Malaria ifikapo 2030. Hili ni lengo letu , matamanio na mtazamo wetu wa kuifanya dunia hii kuwa bora, sayari yetu kuwa yenye afya na mazingira endelevu, ambapo kila mtu ataweza kuishi bila hofu na pia utu"
Tangu kuanzishwa kwake miaka 15 iliyopita fuko la kimataifa, Global Fund limeshaokoa maisha ya watu zaidi ya milioni 20.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania