CURRENT NEWS

Monday, September 12, 2016

WAKALA WA UFUNDI NA UMEME TEMESA PWANI WATUPIWA LAWAMA

Na Mwamvua Mwinyi
WAKALA wa ufundi na umeme (TEMESA)mkoani Pwani,umelalamikiwa kuwa na mafundi wa mitaani lukuki na kuzorota katika kufanyakazi zake ipasavyo huku ikitoza gharama kubwa za matengenezo katika magari ya serikali.
Wakala huo unatupiwa lawama za kutengeneza kwa gharama kubwa kuanzia 500,000 hadi mil.11 kwa gari moja wakati magari hayo yangepelekwa kwa mafundi wa kawaida gharama zingekuwa nafuu.
Licha ya hayo magari ya mkuu wa mkoa huo sambamba na katibu tawala wa mkoa bado yapo kimatengenezo kwa zaidi ya miezi mitatu sasa . kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya ufundi licha ya gharama zao kuwa juu.
Hayo yalisemwa na baadhi ya wabunge,wenyeviti wa halmashauri,wakuu wa wilaya na viongozi wengine wa serikali ya mkoa wa Pwani kufuatia kero kubwa wanayoipata mara wanapopeleka magari kutengenezwa na TEMESA.
Waliiomba serikali iangalie njia nyingine ya kutengeneza magari yake ya serikali badala ya kutumia wakala huo ambao hauwasaidii zaidi ya kupoteza fedha nyingi.
Changamoto hiyo pia imemkuta mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo ambae anasema hata yeye gari lake liko linatengenezwa huko,hivyo kuna haja ya sheria ya utengenezaji magari kuangaliwa upya.
Nae mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha Mansoor Kisebengo ,alisema  wamepeleka magari yao matatu kwa ajili ya matengenezo na kila gari limetakiwa gharama ya mil.11.
Alisema badala ya kutengenezwa kwa magari hayo lakini baada ya matengenezo yamerudishwa yakiwa na hali mbaya zaidi hivyo kuwapa hasara.
Kisebengo alisema serikali inawajibu wa kuliangalia jambo hilo kwani fedha hizo zingeweza kutumiwa na mambo mengine ya kijamii kuliko kuzipoteza .
Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze,Saidi Zikatimu alieleza kwamba ni vyema serikali ikaawamini kama wanavyowaamini katika matumizi mengine ya fedha kwa kuwaruhusu kutengeneza magari kwa mafundi wa nje.
Alisema walipeleka magari yao TEMESA lakini magari hayo bado ni mabovu hayafanyi kazi na hela imepotea.
Zikatimu alisema wakala huo wamekuwa wakitengeneza magari hayo kwa fedha nyingi huku yakiwa chini ya kiwango na kusababisha magari hayo kutofanya kazi baada ya kutengenezwa.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kibiti, Alvera Ndabagoye alisema serikali inapaswa kuliangalia jambo hilo kwa umakini.
Alisema kwasasa hakuna haja ya kuwa na Temesa kwani wamekuwa wakifanyakazi kwa kutokuwa na umakini .
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa alisema wamefanya utafiti juu yao na kugundua kuwa uwezo wao ni mdogo ,na siku chache zilizopita walitengeneza gari la wagonjwa la Kwala ambapo gharama zilikuwa ni mil.5 lakini baada ya muda mfupi limeharibika na sasa liko sokoni wakitaka kuliuza.

Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Pwani Abdi Isango alisema kuwa gharama za wakala hao ni kubwa na hazikidhi lakini kwa mafundi wengine toka nje wanatengeneza kwa uhakika .
Akijibu malalamiko hayo, meneja wa Temesa mkoa wa Pwani,Richard Mutagulwa, alisema ni vema walalamikaji wakafanya utafiti .
Alisema huwa wakitengeneza magari hayo bila matatizo na lengo lao ni kutoa huduma bora kwa wateja wao.
Mwisho.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania