CURRENT NEWS

Wednesday, September 7, 2016

WAKAZI WA MIHUGWE WAMDAI MIL.200 ZA FIDIA MWEKEZAJI KILUWA GROUP

 Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mihugwe wilayani Kisarawe ,baada  ya kupata malalamiko yao,kutoka kwa ofisi ya wilaya hiyo, juu ya kucheleweshwa kwa fidia yao ya hekari 774 kati ya 2,032 aliyoinunua mwekezaji Kiluwa group.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kisarawe

WAKAZI wa kijiji cha Mihugwe ,wilayani Kisarawe mkoani Pwani,wamemtaka mwekezaji Kiluwa group,kuwalipa fidia yao iliyobaki ya kiasi cha sh.mil 200 katika heka 774 alizozichukua kwao,ili waweze kumpisha .

Wamesema endapo ikifika octoba mosi mwaka huu ,pasipo kuwalipa fidia yao basi arudishe ardhi hiyo mikononi mwa wananchi.

Kufuatia msimamo huo mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,pamoja na kamati ya ulinzi na usalama wilayani Kisarawe,wamelazimika kuubeba mzigo wa mwekezaji huyo kwa kumsisitiza amalize deni hilo tr.28 mwezi huu.

Mkuu huyo wa mkoa,akizungumza na wanakijiji hao ,alisema atahakikisha mwekezaji Kiluwa Group anamaliza fidia hiyo ambayo ni asilimia 28 pekee kati ya malipo ambayo tayari ameshayalipa ya hekari 2,032 kwa gharama ya zaidi ya bil.1.

Mhandisi Ndikilo aliwataka wananchi hao kuvuta subira kwani wameshavumilia kwa muda mrefu hivyo siku 21 walizoahidiwa kuanzia sasa sio muda mrefu.

“Mniamini sana na mkuu wa wilaya ,tumpe nafasi mwekezaji,tusiwe wanyonge naimani atatimiza,maana naangalia tunapokwenda ni pafupi kuliko tulikotoka”

“Mambo makubwa yatafanyika katika kijiji hiki,kupata mwekezaji mkubwa kama huyu ni lazima tujenge ushirikiano nae kuanzia mwanzo,ikifika tarehe sept 28 na mimi nitarudi tena hapa na mkuu wa wilaya yenu huku tukiwa na mwekezaji tena akiwa na fedha ”alisema mhandisi Ndikilo.

Aidha mhandisi Ndikilo,alieleza kuwa baada ya kupokea malalamiko ya wanakijiji kutoka kwa mkuu wa wilaya hiyo Happiness Seneda ,aliamua kumpigia simu mwekezaji ambapo ameahidi kulipa tarehe 28 mwezi huu.

Alisema amekubali kumpa muda wa siku 21 bila kumuangusha ili kuwapa haki yao wananchi hao na hatimae waweze kupisha mchakato na hatua nyingine zinazoendelea kufanyika za umilikishaji ardhi kwa mwekezaji.

Hata hivyo ,mhandisi Ndikilo alisema mwekezaji Kiluwa group anatarajia kujenga makampuni 50 tofauti katika eneo hilo la kijiji cha Mihugwe hivyo kutapatikana ajira na kuinua maendeleo na uchumi wa kijiji hicho.

Alisisitiza kuwa mkoa wa Pwani umejipanga kuwa ukanda wa uwekezaji hivyo kwa kuendelea kutenga na kutoa maeneo kwa wawekezaji kutasaidia kufanikisha adhama hiyo.

Mhandisi Ndikilo,alimtaka mkuu wa wilaya hiyo kuendelea kusimamia suala la uwekezaji na ulinzi na usalama wilayani hapo .

Wanakijiji akiwemo Omary Msese,Hamis Seif ,Zainab Ramadhani na Shaban Masenga walimshukuru mkuu wa mkoa  huyo kuwaunga mkono na kuwakimbilia kuwasikiliza malalamiko yao.

Masenga alisema mwekezaji alitoa siku 10 tangu tr 16 agost mwaka huu lakini muda huo umepita hivyo kuwa na sintofahamu.

“Amefanya kutukamata kama mchumba lakini siku ya harusi anaagiza wawakilishi na kutoa ahadi,kwa sasa tumechoka ikifika octoba 1,tutaomba mkuu uje uturejeshee ardhi yetu aliyoshindwa kuilipia fidia ,tuna mengi ya kufanya”alisema Masenga.

Nae mkuu wa wilaya ya Kisarawe,Happiness Seneda alisema,mwekezaji amenunua kwa mwananchi mmoja mmoja na kila mwananchi ameridhia kwa hiari yake kutoa ardhi kwa mwekezaji.

Anasema awamu ya kwanza malipo yamefanyika katika hemari 2,032  kwa asilimia 72 na heka 774 asilimia 28 haijalipwa na kwa sasa hatua zinaendelea kwa ajili ya kupitisha hati ya mwekezaji.

Happiness alisema kamishna wa ardhi msaidizi kanda ya Mashariki aliomba taratibu zilizobaki zikamilishwe ili hati ya mwekezaji itoke ikiwemo kumtaka apeleke taarifa ya mtaji wake na mpango wa biashara yake na tayari wameshamuandikia barua hiyo.

Alimuomba mwekezaji kuweka maelewano baina yao na wanakijiji ili kulinda maslahi ya jamii ili kukamilisha zoezi hilo.

Happiness alisema katika mchakato wa kumpa eneo mwekezaji hatua mbalimbali zilipitiwa kisheria ikiwemo ngazi ya kijiji,wilaya kupitia kamati ya umilikishaji ardhi ,baraza la madiwani na kamishna kanda ya Pwani kisha kufikisha ngazi nyingine za juu ili kummilikisha mwekezaji huyo.

Awali mtendaji wa kijiji cha Mihugwe,Juma Somekeza alisema kijiji hicho kina vitongoji viwili vya Bidiga na Mihugwe ,wakazi 605 ,ambao wamempokea mwekezaji Kiluwa group toka mwaka 2014.

Juma alisema ,kufikia tr.2 march mwaka huu malipo yalifanyika katika hekari 2,032 kati ya hekari 2,806 na bado wanadai malipo ya hekari 774
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania