CURRENT NEWS

Wednesday, September 14, 2016

WAKURUGENZI WA MANISPAA, MIJI NA HALMASHURI WAAPISHWA TAMISEMI MJINI DODOMA LEO.

Wakurugenzi wapya 13 wa halmashauri wameapa kulinda maadili na kukabidhiwa majukumu ya kufuatilia maagizo ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, kwenye maeneo yao na kutoa mrejesho wa hatua za utekelezaji wake. 

Kiapo hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki aliyewataka kutilia mkazo ufuatiliaji wa maagizo na kupambana na tatizo la watumishi hewa ambao idadi yao imefikia 17,102 waliogundulika katika kipindi cha kuanzia Machi mpaka sasa. 

Wakurugenzi hao walioteuliwa hivi karibuni na Rais, John Magufuli waliapishwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene katika ukumbi wa Tamisemi mjini Dodoma.

 Akizungumza mara baada ya kiapo hicho, waziri Kairuki aliwataka wakurugenzi hao kutekeleza matamko yote yanayotolewa na viongozi wa ngazi za juu serikalini, kwa kutoa mrejesho wa utekelezaji wake. 

Kairuki aliwataka kufanya kazi kwa bidii ili wawatumikie wananchi wanaowaongoza. 

Alisema katika ziara nyingi alizozifanya, amekuta wakurugenzi hawafuatilii matamko yanayotolewa na viongozi wa ngazi za juu serikalini katika maeneo yao. 

“Hata kwa wale ambao wanayafuatilia huwa hawatoi mrejesho wa hatua zilizofikiwa katika kutekeleza matamko hayo, hivyo ninawaomba mkayatekeleze maagizo na kurudisha mrejesho kwa kiwango kinachotakiwa,” alisema Kairuki. 

Pia, aliwataka wakurugenzi hao kwenda kusimamia fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali hadi senti ya mwisho, ili kuhakikisha inatekelezwa kwa asilimia 100. 

Alisema kuna baadhi ya miradi ya maendeleo, inatekelezwa kwa fedha za Serikali na wakati huo huo inatumia fedha za wafadhili. 

Waziri Kairuki aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha kuwa miradi yote inayotumia fedha za Serikali inasimamiwa ipasavyo. 

“Utakuta mradi mmoja unafadhiliwa na pia unatumia fedha za Serikali, kwa hiyo wafadhili wakija kukagua wanaonyeshwa jengo likiwa limekamilika na Serikali nayo ikija kukagua inaonyeshwa jengo hilohilo. Nataka mkasimamie fedha zote za Serikali kwenye mamlaka zenu,”alisema Kairuki. 

 Alisema kuna baadhi ya maeneo ambako fedha za Tasaf (mpango wa kunusuru kaya maskini), zimetumika kujengea maabara na kununulia madawati kinyume na malengo yaliyokusudiwa. 

Pia, aliwataka kuhakikisha kuwa hatua kali za kinidhamu zinachukuliwa kwa wakati kwa watumishi waliosimamishwa kazi katika kipindi cha miezi sita na si zaidi ya hapo. 

Alisema mtumishi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kufukuzwa au kusimamishwa kazi, mchakato wake wote ufanyike ndani ya miezi sita. 

Aliwataka pia wakurugenzi hao kufuata maadili ya viongozi wa umma, kwani wakikiuka watafikishwa kwenye baraza la maadili ya viongozi wa umma ambalo kwa sasa limeongezewa meno. 

Waziri Kairuki aliwataka wakurugenzi hao kusimamia suala la rasilimali watu, kwani utafiti ulionyesha kuwa asilimia 80 hadi 90 ya watumishi wa umma ni watoro.

Alisema katika baadhi ya maeneo kuna wakaguzi na waratibu wa elimu wa kata, lakini hawatembelei shule zao kuona kama walimu wanahudhuria shuleni au la. 

Kadhalika, aliwataka wakurugenzi hao kuachana na tabia ya kuwatumia viongozi wa Serikali walioko chini yao, kama vile watendaji wa kata, vijiji na wenyeviti wa vijiji kuwalimia mashamba yao.

Alisema watakaobainika kufanya vitendo hivyo, watachukuliwa hatua kali za kinidhamu. 

Waziri Simbachawene aliwataka wakurugenzi hao kwenda kuchapa kazi bila kumwonea yeyote. Aliwaambia kuwa kukusanya  mapato kiwe ni kipaumbele chao cha kwanza, kwani kipimo cha mamlaka yoyote kujitegemea ni uwezo wake wa kukusanya mapato. 

Aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha kuwa wanawatembelea watumishi wao wote ili kujua penye upungufu, idadi yao na hata ikiwezekana kuwajua kwa majina yao. 

Wakurugenzi walioapishwa jana ni Godwin Kunambi (Dodoma) Elias Ntiruhungwa (Tarime), Mwantumu Dau (Bukoba) na Frank Bahati (Ukerewe) Wengine ni Hudson Kamonga (Mbulu), Mwailwa Pangani (Nsimbo), Godfrey Sanga (Mkalama), Yusufu Semuguruka (Ulanga), Bakari Mohamed (Nachingwea), Juma Mnweke (Kibondo), Butamo Ndalahwa (Moshi), Waziri Mourice (Karatu) na Fatma Latu (Bagamoyo). 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene akiwapongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi baada ya Wakurugenzi wa Manispaa, miji na Halmashauri baada ya kiapo mjini Dodoma Septemba 13 2016.
Baadhi ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wakila kiapo wakati wa hafla maalum ya kukabidhiwa majukumu yao katika ofisi za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mjini Dodoma Septemba 13.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene akiwapongeza baadhi ya Wakurugenzi wa Manispaa, miji na Halmashauri baada ya kiapo mjini Dodoma jana.
Baadhi ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wakila kiapo wakati wa hafla maalum ya kukabidhiwa majukumu yao katika ofisi za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mjini Dodoma Septemba 13.

Katibu msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma Ofisi ya Kanda ya kati Dodoma, Cathlex Makawia (kulia) akiwaapisha wakurugenzi 13 wa manispaa, miji na na halmasahuri mjini Dodoma. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Bernard Makali. (Picha na Robert Okanda) 

Baadhi ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wakila kiapo wakati wa hafla maalum ya kukabidhiwa majukumu yao katoka ofisi za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mjini Dodoma. 


Baadhi ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wakila wakitia saini viapo vyao baada ya kuapa  wakati wa hafla maalum ya kukabidhiwa majukumu yao katika ofisi za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mjini Dodoma Septemba 13 2016. 

Baadhi ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wakila wakitia saini viapo vyao baada ya kuapa  wakati wa hafla maalum ya kukabidhiwa majukumu yao katika ofisi za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mjini Dodoma Septemba 13 2016.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki akiwapa mawaidha na ushauri wa kiutendaji Wakurugenzi baada ya kuapa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene akiwapa mawaidha Wakurugenzi wa Manispaa, miji na Halmashauri 13 baada ya kiapo mjini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene akiwapongeza baadhi ya Wakurugenzi wa Manispaa, miji na Halmashauri baada ya kiapo mjini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki wakifahamiana na baadhi ya wakurugenzi.
Waziri Kairuki akibadilishana mawasiliano na Mkurugenzi wa Manispaa ya Mbulu, Hudson Kamoga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene akiwapongeza baadhi ya Wakurugenzi wa Manispaa, miji na Halmashauri baada ya kiapo mjini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene (katikati), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jaffo (wa pili kushoto), Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma Ofisi ya Kanda ya kati Dodoma, Cathlex Makawia (kushoto) pamoja Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Bernard Makali (kulia) wakiwa katika pichAa ya pamoja na wakurugenzi hao. (Imeanaliwa na Robert Okanda Blogs)
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania