CURRENT NEWS

Tuesday, October 4, 2016

WALIMU MKOANI PWANI WADAI MALIMBIKIZO YA MADENI ZAIDI YA BIL.2


Katibu wa chama cha walimu mkoani Pwani, (CWT),Nehemiah Joseph ,pichani akionekana akizungumza na waandishi wa habari,kuhusiana na hali ya  malimbikizo ya madeni ya walimu kimkoa.
(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
KATIBU wa chama cha walimu mkoani Pwani(CWT),mwl.Nehemiah Joseph ,amesema walimu mkoani humo,wanaidai serikali,malimbikizo ya madeni zaidi ya sh.bil .2.158,183 katika kipindi cha mwaka 2015/2016.
Kati ya fedha hizo ,walimu wanaofundisha shule zinazomilikiwa na shirika la elimu Kibaha(KEC) wanadai kiasi cha sh.mil.700 katika kipindi hicho.
Amesema madai hayo ni kwa ajili ya fedha za likizo,uhamisho,gharama za masomo,safari za nje, matibabu ,ajira mpya,ukaguzi na nauli za wastaafu .
Mwl.Joseph aliyasema hayo ,ofisini kwake mjini Kibaha,baada ya kuulizwa na waandishi wa habari ,hali ya taaluma na madeni ya walimu mkoani humo kijumla.

Katibu huyo alisema walimu wa shule za msingi,sekondari na vyuo vya ualimu ikiwemo chuo cha Vikindu ndio hawajalipwa fedha hizo .

Aidha Joseph alitaja gharama zinazodaiwa kwenye  likizo ni mil.428,280,457.91,ajira mpya mil.47,153,868,matibabu ni mil.47,157,825,masomo mil.228,783,501,uhamisho mil .517,197,438 ,safari za nje mil.2.835 na nauli za wastaafu mil.186,772,400 ambayo jumla yake ni bil.1,458,183,489.91.

Alifafanua ,shule zinazomilikiwa na shirika la elimu Kibaha(KEC)kutokana na waraka wa mwaka 2010/2011,mapunjo ya mshahara,ambao uhakiki wao ulifanywa na msajili wa HAZINA ,ulibaini madai ya mil.700 na kufikisha jumla kuu ya deni zaidi ya bil.2.158.183 kimkoa.

Hata hivyo mwl.Joseph alieleza kuwa serikali imeshalipa malimbikizo ya fedha kwa walimu katika madai ya miaka ya nyuma yakiwemo ya 2013-2014/2015 lakini kipindi cha 2015/2016 bado hawajalipwa.

“Walimu mkoani hapa bado wanadai haki yao ya malimbikizo hayo ya madeni mbali mbali, hivyo kauli ya inayodaiwa kusemwa kuwa walimu hawaidai serikali sio kweli kwani imemaliza madeni ya nyuma na sio ya 2015/2016”

“Kwani kauli za kusema fedha zimelipwa na kwamba serikali haidaiwi inawavunja moyo walimu,kwasababu walimu wanamadai mengi hasa fedha za kwenda likizo ambazo hazilipwi kwa muda ama zikilipwa zinakuwa pungufu”alisisitiza mwl Joseph .

Joseph aliiomba serikali kuangalia kwa jicho tatu kero zinazoendelea kuwakabili ili kurejesha molari na ari kwa walimu waweze kuinua taaluma mkoani Pwani

Kuhusu walimu wastaafu ,aliipigia goti serikali kuharakisha kutoa fedha zao za nauli ili waweze kujikimu ambapo pia amewaasa wastaafu wa shule za msingi na sekondari,kutumia mafao wanayopata vizuri badala ya kutumia kifahari hatimae kuishiwa na kubaki maskini ndani ya jamii.
Nae mmoja wa walimu wastaafu wilayani Kibaha, Ally Mkunga ,alisema kwa sasa wapo katika hali ngumu ya kimaisha hivyo serikali inapaswa kuwajali kwa ari na mali kwa  kuhakikisha inawalipa stahiki zao.

Alisema walimu hasa wanaostaafu  wamekuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kucheleweshwa na kuzungushwa kupata mafao yao kwa wakati kwa visingizio vya kukosa bajeti ya fedha.

Mkunga alisema wanaimani na serikali ya awamu ya tano kwamba itasikia kilio chao kutokana na kujali kwake maslahi ya watumishi na kupigania haki za wanyonge.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania