CURRENT NEWS

Tuesday, October 18, 2016

DIWANI WA VIGWAZA AWAOMBA WANANCHI KUVUTA SUBIRA KWA KERO YA MAJI SALAMA

Baadhi ya waandishi wa habari na wananchi wakimsikiliza diwani wa kata ya Vigwaza, Mohsin Bharwani ,wakati alipokuwa akielezea mipango ya serikali katika kutatua kero ya maji na namna anavyosimama tatizo hilo linalowakabili wakazi wa kata hiyo.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Diwani wa kata ya Vigwaza, Mohsin Bharwani ,akizungumza jambo na mkazi wa kata hiyo baada ya kukutana na baadhi ya viongozi na wakazi wa kijiji cha Ruvu darajani na Vigwaza .(picha na Mwamvua Mwinyi)


Na Mwamvua Mwinyi, Vigwaza
Wakazi wa kata ya Vigwaza ,wilayani Bagamoyo mkoani Pwani,wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji salama hali inayosababisha kutumia maji ya visima na kununua maji ,ndoo kwa gharama ya sh.500 hadi 700 .

Adha hiyo ni kubwa kutokana na kupata maji kwa mgao hivyo kupelekea kununua maji kwa watu wenye matanki ya maji ambao huyauza kwa gharama kubwa .

Hayo yalielezwa na mtendaji wa kata hiyo,Saidi Omary wakati diwani wa kata ya Vigwaza,Mohsin Bharwani,alipokwenda kutimiza ahadi yake ya kuchangia matofali 1,000 na mifuko ya saruji 30 katika zahanati ya Ruvu darajani na kutoa madawa katika zahanati hiyo na zahanati ya Vigwaza.

Omary alisema tatizo hilo ni la muda mrefu ambalo linawapa shida kwani licha ya kutegemea visima kwasasa vimekauka na wengi wao kushindwa kumudu gharama za kununua maji kila siku.

Nae mkazi wa kijiji cha Vigwaza Zulfa Hassan ,alieleza  wanalazimika kununua madumu ya maji madumu ama ndoo tatu hadi tano kwa siku kulingana na matumizi ya familia.

“Uwezo wa kutoa sh.2,000 kila siku ama 1,000 kwa siku kwa ajili ya maji pekee inatugharimu sana,tunakuomba diwani utusaidie kusimamia suala hili ili huduma ya maji iboreshwe na kuondokana na kero hii”alisema Zulfa.

Kufuatia changamoto hiyo ,Mohsin aliahidi kupeleka mtu  wa kuuza maji kwa gharama nafuu kwa kiasi cha sh.200-250 ili kuwapunguzia mzigo wakazi hao.

Alieleza kuwa kuanzia mwezi ujao watapata maji kwa gharama nafuu tofauti na ilivyosasa wakati wakisubiri serikali ikitekeleza mpango wake wa kusambaza maji katika mji wa Chalinze ikiwemo Vigwaza.

Mohsin alisema anatambua kuhusiana na kero hiyo tangu kipindi cha kampeni ambapo aliahidi kusimamia na kuendela kufuatilia katika idara husika ili hali kuweza kupunguza ama kuondokana nayo.

Aidha anasema kwasasa serikali inaendelea na mpango wake wa kushughulikia tatizo la maji ambapo kazi inaendelea ya kusambaza na kutandika mabomba .

"Matanki pia yanajengwa ila  ndugu zangu mtambue kazi hizi zinachukua muda mrefu,tuvute subira,kwani serikali yetu inatujali na naamini katika kipindi kifupi tutaondokana na adha  hii"

"Adha mnayopata ni kubwa kununua maji kwa gharama kubwa ,nimemuomba jamaa yangu aje auze maji hapa kwa kutumia gari na atayauza kwa sh.200 hadi 250 ili kuwapunguzia makali mnayoyapata" alisema Mohsin.

Hata hivyo alisema ataendelea kutimiza ahadi zake kulingana na uwezo wake kwani mwanzoni mwa mwaka huu alishanunua mashine ya kuvuta maji kutoka katika chanzo cha maji cha mto Ruvu na kuyafikisha kwenye shule ya msingi kijiji cha Kidogozero.

Kwa mujibu wa diwani huyo amenunua pia mabomba ya nchi mbili mita 600 yatayotumika kwa ajili ya kutoa maji kutoka katika chanzo hicho mpaka shuleni hapo ,ambapo mashine na mabomba hayo yamegharimu mil.4.

Mohsin alibainisha wakati mchakato wa ukamilishwaji wa mradi wa maji ya Wami -Chalinze ukiendelea ameona ni vema aanze na juhudi hizo lengo likiwa kuwaondolea adha wananchi hao.

Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira  Chalinze (CHALIWASA) Injinia Christer Mchomba  aliwahi kusema katika utekelezaji wa mradi wa  maji  wa awamu ya tatu  unaofanyika chini ya mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani mil.4.3 utapunguza tatizo la maji lililopo.

Alisema kutaongezwa tekeo la chanzo cha maji cha mto Wami  kutoka lita M.7.2 zinazozalishwa kwa sasa hadi kufikia lita M.11.0. kwa siku.

Injinia Mchomba alisema kukamilika kwa mradi huu utapunguza matumizi makubwa ya umeme  ambayo yamekuwepo katika kusukumia,na wanatarajia kuongeza matenki mengi ya kuhifadhia  maji na mitambo hivyo kuwa na uhakika wa maji kwa kiasi kikubwa.

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania