CURRENT NEWS

Saturday, October 22, 2016

JAFO:ALIKINGIA KIFUA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA(KEC)NA TUMBI

Naibu waziri  ofisi  ya rais  TAMISEMI, Selemani Jafo  ,akizungumza jambo na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Pwani,watumishi na uongozi wa shirika la elimu Kibaha na kamati ya kudumu ya bunge  ya utawala na serikali za mitaa .(Picha zote na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Naibu waziri ofisi ya rais TAMISEMI,Selemani Jafo ,ameitaka kamati ya kudumu ya bunge ya utawala na serikali za mitaa kuhakikisha wanasimamia changamoto zinazolikabili  shirika la elimu Kibaha (KEC)ikiwemo ufinyu wa fedha hali inayosabaisha kusuasua .
Aidha ameiomba wizara ya afya kwa kushirikiana na kamati hiyo,kupigania kitengo cha dharura katika hospital ya rufaa ya Tumbi kiweze kupandishwa hadhi na kuwa kama ilivyo Muhimbili ndani ya miaka mitano ijayo.
Aliyasema hayo ,wakati alipoambatana na kamati hiyo kutembelea shirika la elimu Kibaha ,hospital ya rufaa ya Tumbi na kiwanda cha uzalishaji kuku Organia,mfumo wa malipo ya kielektroniki na mtambo wa oxygen.
Jafo alieleza kuwa asilimia 80 ya ajali hutokea katika barabara kuu ya Morogoro-Dar es salaam ,Chalinze-Segera na kusababisha hospitali hiyo kuhemewa hivyo ameitaka kamati hiyo kuangalia umuhimu wa hospital hiyo.
Alisema endapo kitengo cha dharura kitapandishwa hadhi basi itasaidia kunusuru vifo vinavyotokana na kukosa huduma ya haraka ama iliyo bora.
Jafo alisema pia shirika la elimu Kibaha linafanyakazi kubwa sanjali na hospital ya rufaa ya Tumbi hivyo kuna kila sababu ya kusemea changamoto zinazozikabili.
“Kamati muangalie kwa jicho la huruma na kuifanya Kibaha iwe modal na shokonzoba ya matatizo mbalimbali ambapo kwa kufanya hivyo itafika mbali”alisema Jafo .

Hata hivyo alizitaka hospitali za mikoa na wilaya kuchukua mifumo ya malipo ya kielektronik inayobuniwa na watanzania badala ya kutumia  mifumo inayotoka nchi za nje yenye gharama kubwa ili kujiongezea mapato.
Akizungumzia miradi mbalimbali ya uwekezaji wa kuku na hospitali ya Tumbi ,Jafo alisema wamejionea mifumo na ubunifu wa watanzania walioifanya katika suala zima la kukusanya fedha ,kodi za serikali kuimarisha sekta ya afya.

Alisema mbali ya hilo wameona ni  jinsi gani wataalamu wakifunga mitambo ambayo sasa hewa ya oxygen kwa wagonjwa na mitungi inatengenezwa hospitalini hapo ambapo katika halmashauri huwagharimu kununua kwa gharama kubwa .


Kwa niaba ya wizara aliwashukuru na kuomba waungane mkono na kamati hiyo kuongea kwa kauli moja kuiangalia hospitali hiyo kwa kuiboresha ili kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa kukimbilia Muhimbili.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo,kamati iwe msemaji mkubwa wa Tumbi na kushauri michakato mbalimbali ya bajeti ili hali mwisho wa siku jamii iweze kunufaika na ubunifu ulipo katika hospitali hiyo na huduma inazozitoa.
Nae mwenyekiti wa kamati hiyo,Dickson Rweikiza  alilipongeza shirika hilo kwa kazi wanazozifanya.
Alisema ardhi ni mali hivyo shirika hilo litumie fursa ya ardhi kubwa iliyonayo kuwekeza ili kujipatia kipato na kuongeza ajira .
Makamu mwenyekiti wa kamati Mwanne Mchemba,alisema kumbe wapo watanzania ambao ni wabunifu  na mfano wake ni wa kuigwa kwenye uwekezaji,kutengeneza mitungi ya gesi na mfumo wa ukusanyaji fedha.
Alimpongeza mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Ndikilo kwa juhudi anazozifanya hasa kwenye suala la kupanua wigo wa uwekezaji na viwanda.
Mwanne alisema ufinyu wa bajeti unakera na kusababisha shirika kukwama kutoka na ufinyu lakini kwa wimbo wa pamoja wanaimani bajeti ya safari hii kwa malengo na mipango ya shirika bajeti itaongezeka na kufikia hata asilimia 50 kama sio 100.
Amliema kilio chao wamekisikia na waahidi kukifanyiakazi ili kutoka walipo ili kuwahudumia wananchi kikamilifu.
Awali mkurugenzi wa shirika la elimu Kibaha,Cyprian Mpemba ,alisema fedha waliyopata hadi kufikia mwezi huu ni asilimia 17 pekee fedha ambayo ni ndogo ukilinganisha na mahitaji ya shirika.
Alisema walitegemea kupata fedha zaidi ya asilimia 70 hivyo kusababisha shirika kuwa katika hali mbaya licha ya kuendelea kujiendesha wenyewe kupitia fedha za ndani na kuandika maandiko na ubunifu .
Mpemba alisema shirika linakabiliwa na tatizo la upungufu wa watumishi 450 ambapo kwasasa wapo watumishi 830 pekee huku mahitaji yakiwa ni 1,280 na uhaba wa madawa.
Mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Ndikilo,alieleza shirika hilo, ni muhimu kimkoa na taifa tangu lianzishwe mwaka 1970  na kufanya shughuli zake ikiwemo kutoa huduma za kiafya ,kielimu na kilimo.


Ndikilo aliomba kupitia kamati hiyo iangalie namna gani ya kusaidia kusukuma upatikanaji wa duka la dawa kwani wameshapeleka maombi hayo wizara ya afya .
Alisema kuwepo kwa duka hilo pasipo kutegemea duka la dawa la muhimbili kwakuwa mgao wa dawa hautoshi kulingana na mahitaji kuwa makubwa.
Ndikilo alisema kuwa kuna fursa kubwa ya ardhi na inaweza kutumika kwa kuwekeza ukizingatia Dar es salaam imejaa hivyo kupitia bodi yao waweze kutumia ardhi hiyo kama fursa na kuwekeza ili iweze kujinufaisha.
Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya Rufaa ya Tumbi,dk.Bryceson Kiwelu ,alifafanua wanakusanya fedha  kwa kutumia mfumo wa kielektronik.
Alisema safari hiyo imeanza mwaka 2011 walikuwa wakikukusanya 300,000 kwa siku kwa kutumia njia ya risiti lakini baada ya kutumia mfumo huo mapato yaliongezeka  na sasa wanakusanya mil.3 kwa siku.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania