CURRENT NEWS

Sunday, October 9, 2016

MADEREVA WA MAGARI YABEBAYO MCHANGA WAITISHIA TANROADS PWANI

Kamanda wa Usalama barabarani  mkoani Pwani , Abdi Issango,akizungumza na baadhi ya madereva wa magari ya matipa ya mchanga ambao walitishia kugoma  katika zoezi la  kukaguliwa na wakala wa barabara  (TANROADS) kutokana kujaza mchanga  na kusababisha uchafuzi wa miundombinu ya barabara (picha na Mwamvua Mwinyi)Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

MADEREVA wa matipa ya mchanga ,wanaotumia barabara kuu ya Dar es salaam –Morogoro, wamefanya mgomo baridi ,kulalamikia wakala wa barabara (TANROADS)mkoani Pwani,unaowakamata kutokana na kutofunga mchanga vizuri na kuwapiga faini ya sh.500,000.

Madereva hao waliweka mgomo huo katika eneo la Tamco ambapo ndipo watendaji wa wakala huo walikuwa wakiwasimamisha kwa ajili ya kukagua wale waliojaza mchanga hali inayosababisha kuchafua miundombinu ya barabara.

Dereva Martine Magari na Emmanuel Shao,walisema ni kweli wapo madereva wasiofunga vizuri maturubai ya magari yao lakini tatizo kubwa ni kukosa elimu ya kufunga kwa ubora .

Shao aliziomba idara ama mamlaka husika kutoa elimu juu ya sheria mbalimbali kwani inakuwa sio rahisi kuelewa sheria zote zinazotungwa bila kupatiwa elimu ya kutosha.

“Unaona fuso dogo kama lile,huwezi amini ni sh.500,000 kikweli ni kubwa ,sasa unakuta tunalalamika kutokana na kwamba hatujui lolote kuhusu sheria zao”

“Halafu hatujafundishwa kufunga hooks wanavyotaka wao wakala wa barabara,kila mtu anaufungaji wake lakini endapo watatuelewesha vizuri haina shida .

"Sasa wao wanapanda juu ya gari na kuchokonoa  chokono matokeo yake ndio inakuwa shida ,mchanga unamwagika”alisema Shao.

Magari aliutaka wakala huo kukagua kwa macho na sio kupekenyua maturubai kwa kuingiza mikono kwani kwa kufanya hivyo ni lazima mchanga mwagike .

“Madereva pia wamekasirika kwa hilo huwezi kukagua hadi uingize mikono ,kwakuwa mikono inasababisha mchanga kumwagika halafu unatozwa hela yote hiyo”alifafanua Magari.

Kwa mujibu wa kaimu meneja TANROADS mkoani Pwani,injinia Yudas Msangi,alisema wapo kwenye operesheni ya kukagua magari ,kwa kufuata sheria ya barabara ya mwaka 2007 namba 13 kifungu namba 46C, inayokataza kuchafua barabara .

Alieleza kuwa hakuna anaewaonea madereva hao ,kwani wanatambua vilivyo kuhusu sheria hiyo na mara kwa mara huwa wakielimishwa kuacha tabia ya kuzembea kufunga mchanga vizuri.

Injinia Msangi alisema,wanatoa muda hadi jumatatu ijayo zoezi hilo litaendelea ili kudhibiti uchafuzi huo wa miundombinu ya barabara.

Alisema wanatakiwa wasijaze mchanga kwakuwa unaathiri matairi ya magari mengine yanayopita,kusababisha ajali ,kufukia mifereji na kufuta alama za barabarani na hatimae kuipa mzigo wakala huo.

Injinia Msangi alisema lengo ni kuacha kumwagwa mchanga na kufunga matipa ya mchanga kwa ubora ili kuepusha matatizo na kuiondolea hasara TANROADS.

Aliwataka madereva wa matipa ya mchanga kuacha kudharau sheria zilizopo ili kuepuka migongano isiyo na tija.

Awali kamanda wa usalama barabarani,Abdi Issango ,alifika eneo la tukio na kuzungumza na madereva hao ,uongozi wa tanroads mkoa,akiwemo kaimu meneja,msaidizi wake pamoja na meneja wa barabara mkoa mama Urio.


Alisema ni kweli madereva wengi wamekuwa hawafungi vizuri mchanga kwa kutumia kifungio(hooks)kwenye maturubai ili kuzuia mchanga usimwagike.

Hata hivyo kamanda Issango,alisema kwa kushirikiana na wakala wa barabara mkoani humo,wameamua kutoa muda ili kurekebisha mapungufu yaliyopo ambapo kuanzia jumatatu atakaekiuka maelekezo yaliyotolewa atalipa faini ya sh.500,000.

Akizungumzia kiwango cha faini kinacholalamikiwa,alieleza kila idara ina sheria zake, kwa usalama barabara ukikiuka sheria adhabu yake ni sh.30,000 lakini kwa Tanroads ni 500,000  na kutoingia kwenye mizani faini zake huwa ni mil.2 .

Baada ya kamanda huyo kuzungumza na pande hizo mbili ,madereva hao walitawanyika na kuridhia maelekezo waliyopatiwa sambamba na kukubaliana kuanza kwa zoezi hilo wiki ijayo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania