CURRENT NEWS

Sunday, October 30, 2016

MADIWANI MJI WA KIBAHA WASTAAJABISHWA KUSHUKA KWA MAKUSANYO YA USHURU WA STEND NA MCHANGA/WAHOFU KUNA HUJUMA


MKUU wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama akizungumza na madiwani na watendaji wa halmashauri ya Mji wa Kibaha katika kikao cha baraza la  madiwani.
Diwani wa viti maalum Tuaje Ponza,akizungumza jambo katika kikao cha baraza la  madiwani wa halmashauri ya mji wa Kibaha .
Madiwani mbalimbali wa halmashauri ya Mji wa Kibaha wakimsikiliza kwa makini  mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama wakati alipoinuka kutolea  maelekezo suala la  ufinyu wa mapato yanayokusanywa kwenye ushuru wa stend na mchanga (picha zote na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MADIWANI wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,wamesikitishwa  kushuka kwa makusanyo ya mapato ya ndani yanayotokana na ushuru wa stend ya mabasi Mailmoja,machinjio na mchanga na kuhofia kuna hujuma inafanyika.
Mapema mwezi agost ,halmshauri hiyo ilidai inatarajia kuokoa kiasi cha sh.mil.516.792 katika mwaka wa fedha 2016/2017,zilizokuwa zikipotea katika makusanyo ya vyanzo hivyo kutokana na udanganyifu wa baadhi ya mawakala.
Wakizungumza katika kikao cha madiwani,baadhi ya madiwani hao,diwani wa kata ya Tumbi, Hemed Chanyika ,diwani wa viti maalum Selina Wilson na Tuaje Ponza walishangaa makusanyo hayo kushuka zaidi ukilinganisha na ukusanyaji uliokuwa ukifanywa na mawakala wasio wa serikali.
Aidha walisema madiwani waligundua  kuna ubabaishaji kipindi cha nyuma ambapo halmashauri ingeokoa  mil.335.392 zilizokuwa zikipotea kwa mwaka kwenye ushuru wa mchanga.
Walieleza katika ushuru wa mchanga walikuwa wakipokea mil.264.608 kwa mwaka baada ya kutuma madiwani waligundua watakuwa wakipata mil.600 kwa mwaka.
Chanyika alifafanua, katika ushuru wa stend ,halmashauri ilikuwa ikipokea makusanyo ya sh.mil.320 kwa mwaka baada ya uchunguzi wa madiwani wakabaini kuwa wangepata mil.458 kwa kipindi hicho na kuokoa mil 138 zilizokuwa zikipotea.

Alisema kuanzia hapo ndipo halmashauri ilianza kutumia vibarua watakaokuwa wanakusanya ushuru wa vyanzo hivyo kwa usimamizi wa watendaji wa halmashauri badala ya mawakala .


“Matokeo yake mambo yanaenda ndivyo sivyo ,mapato yanayotokana na vyanzo vya mapato vya stend na mchanga sasa yanashuka siku hadi siku tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma ”

“Stend ni ile ile mabasi ni yale yale lakini tangu tenda irudi serikalini mapato ndio yanadidimia kila mwezi sasa hatujui kuna hujuma ili tenda hii irudi kwa mawakala ama”alisisitiza Chanyika.

Tuaje Ponza alisema wastani kwa mwaka waliojiwekea ni kukusanya mil 458 katika ushuru wa stend ambapo kwa mwezi ni wastani wa mil.35-40 lakini haifikii lengo kwani wanakusanya mil.27 hadi 30 .
Hata hivyo alieleza,ushuru wa mchanga makisio ilikuwa ni kukusanya sh.mil. 600 kwa mwaka na kwa mwezi ilitakiwa wakusanye mil.50 na badala yake wanapata mil 21-31 sawa na asilimia 15 ambayo haifikii malengo ya asilimia 80.
Selina Wilson alitaka kujua mpango utakaofanywa ili kukerekebisha hali hiyo hatimae kunusuru vyanzo hivyo.
Alisema chanzo cha stend ya mabasi ni muhimu,kinastahili kupewa kipaombele  hivyo utata uliopo ufuatiliwe bila mzaha.
Akizungumzia chanzo cha machinjio ,Selina aliomba huduma ya maji ipelekwe na isichukue muda  ili machinjio hiyo iweze kujiendesha  na halmashauri ipate mapato yakutosha.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha,Amkawane Ngilangwa ,alikiri ni kweli mapato yanaonekana kushuka hasa kutokana na mabasi mengine kukwepa kuingia stend.

Alisema kwasasa wamejiwekea mkakati wa kufuatilia kwa mkuu wa kituo cha polisi Kibaha(OCD) na askari wa usalama barabarani Mailmoja pamoja na kusimamia na kuhakikisha mabasi  yote yanaingia stend ili chanzo hicho kiendelee kuongeza mapato.
Katika hatua nyingine mweka hazina wa halmashauri ya Mji wa Kibaha,Suzana Chaula, alisema ni kweli ushuru wa mchanga haupatikani kama inavyotakiwa kutokana na mchanga unaotoka nje ya halmashauri hiyo huwa hautozwi ushuru na baadhi ya machimbo yanafungwa .
Alisema tayari menejiment imefanyia kazi kwa kushirikiana na madiwani ,wenyekiti wa mitaa na watendaji wa kata,kupata takwimu halisi ya machimbo ya mchanga mara kwa mara.
Suzana alisema menejiment pia imeunda timu ya wataalamu wa kufuatilia kwa kina suala la mchanga na kuteua msimamizi  kwenye ushuru wa mchanga .
Mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama alisema hawezi kuliachia suala hilo atafuatilia kujua chanzo kinachosababisha kuzorota kwa mapato hayo .
Alisema haiwezekani kuona serikali inakusanya mapato hafifu wakati mawakala wasio wa serikali walikuwa wakikusanya mapato kwa kiwango kinachoridhisha.
Assumpter alisema inashangaza serikali haina meno na  uwezo wa kukusanya kodi na kushuka kuliko makampuni ,kwa hilo hawezi kulifumbia macho.
“Nina wasiwasi kuna hujuma inafanyika ama kuna watu ambao wanaweka fedha mifukoni,nataka kupewa jibu kwanini makusanyo yameshuka,na iwekwe mkakati kuwa ni lazima mabasi yote yaingie stend’alisema Assumpter.
Aliwataka wasimamizi wawe macho ili fedha ikusanywe ipasavyo na kumtaka OCD  asimamie suala hilo na endapo ikigundulika kuna mabasi yanaendelea kupita bila kulipia ushuru askari aliyekuwepo zamu  aondoke.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Amkawane ,alisema ameyachukua maelekezo yaliyotolewa na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha makusanyo ya vyanzo hivyo.

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania