CURRENT NEWS

Monday, October 3, 2016

MKURUGENZI ARUSHA AFAFANUA TUHUMA ZA UBADHIRIFU WA JENGO LA UTAWALA KALIUA


Na Woinde Shizza,Arusha 

Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha, Athumani Kahamia ametoa ufafanuzi kuhusu tuhuma ya matumizi mabaya ya fedha kiasi cha sh, 500 milioni zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala katika halmashauri ya Kaliua na kusema kwamba fedha hadi anahamishwa fedha hizo hazikuwahi kuletwa katika halmashauri hiyo kutoka serikali kuu. 

Hivi karibuni kumekuwa na tuhuma mbalimbali zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii nchini ambapo Kahamia anatuhumiwa kutumia kiasi hicho cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala katika halmashauri ya Kaliua wakati akiwa mkurugenzi wa Kaliua kabla ya kuhamishiwa jijini Arusha. 

Akihojiwa na mwandishi Wa Habari hizi Kahamia alisema kwamba aliripoti mnamo febuari 2015 katika halmashauri hiyo na kukuta ujenzi wa jengo la utawala ukiendelea ambapo katika bajeti ya halmashauri ya Kaliua mwaka wa fedha 2015/16 waliomba fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo katika awamu ya kwanza lakini serikali haikuleta pesa hizo. 

Alisema ya kwamba lakini pamoja na kutenga bajeti ya fedha hizo halmashauri hiyo haikupokea kiasi hicho kutoka serikali kuu na kusisitiza kwamba hadi anaondoka Kaliua fedha hizo hazikuwahi kuzipokea. 

"Hadi tarehe 30 juni mwaka huu hizo fedha tulikuwa bado hatujazipokea mpaka leo tunavyoongea hizo fedha hazijapokelewa taarifa kwamba nimezitafuna zinalenga kunichafua "alisema Kahamia 

Hatahivyo, alifafanua tuhuma kwamba tayari ameandikiwa barua ya kurudishwa Kaliua ili kujibu tuhuma zinazomkabili na kusema si kweli kwani hadi sasa hajapokea barua yoyote wala wito kutoka mamlaka yoyote kumtaka arudi kujibu madai hayo. 

Hatahivyo, alifafanua tuhuma za kumwingilia mkandarasi kutoka kampuni ya Saram Company Limited iliyopewa zabuni ya kujenga jengo hilo la utawala na kusema yeye kama mwajiri alivunja mkataba na kampuni hiyo kwa mujibu wa sheria kwa kuwa mkandarasi huyo alionekana kusuasua katika majukumu yake. 

Alisema kwamba baada ya mkandarasi huyo kuonyesha udhaifu katika mkataba wake walimpa onyo na kisha nitosi kabla ya kuvunja mkataba wake ambapo alikimbilia mahakamani lakini walimshinda kesi hiyo. 

"Huyu mkandarasi alipaswa kumaliza kazi mwezi Mei mwaka 2015 lakini hadi Septemba mwaka huo alikuwa bado hajamaliza kazi yake ndipo tukavunja mkataba wake Akakimbilia mahakamani tukamshinda akakata rufaa tukamshinda tena mchezo ukaishia hapo hapo "alisema Kahamia 

Alisema kwamba wakati wa kuvunja mkataba na mkandarasi huyo zoezi hilo lilisimamiwa na timu ya wanasheria wa halmashauri ya Kaliua pamoja na mkaguzi wa ndani chini ya usimamizi wa mkuu wa mkoa wa Tabora wakati huo, Ludovick Mwananzila. 

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua, Haruna Kasele alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo kwa njia simu alisema kwamba ni kweli halmashauri hiyo katika bajeti ya mwaka 2015/16 waliomba kiasi cha sh,500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo lakini hadi mwaka wa fedha wa serikali unakwisha hawakuwahi kupokea fedha hizo. 

Hatahivyo,alithibitisha taarifa za halmashauri hiyo kuvunja mkataba na mkandarasi huyo chini ya baraza la madiwani na kusema sababu iliyopelekea ni baada ya mkandarasi huyo kusuasua na kushindwa kumaliza kazi aliyopewa kwa wakati mwafaka. Kuhusu madai ya Kahamia kuandikiwa barua ya kuitwa ili kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo mwenyekiti huyo alisema kwamba hakuna jambo kama hilo na wala hawajaandika barua ya kumwita kumhoji mkurugenzi huyo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania