CURRENT NEWS

Monday, October 24, 2016

NDIKILO -WAJASIRIAMALI TUMIENI MAONYESHO YA 9 MWAKA HUU KUJITANGAZA NA KUSAKA MASOKO

Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza jambo kuhusiana na uzinduzi wa maonyesho ya tisa(9) ya wajasiriamali mwaka 2016 yanayotarajiwa kufanyika wilayani Bagamoyo. (Picha na Mwamvua Mwinyi)

WAJASIRIAMALI hasa wadogowadogo wametakiwa kuchangamkia fursa ya kutangaza na kutafuta soko la bidhaa zao katika maonyesho ya tisa (9)ya wajasiriamali mwaka 2016, yanayotarajiwa kufanyika wilaya ya Bagamoyo kuanzia octoba 26 hadi 31 mwaka huu.

Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, alitoa rai hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia mkoa huo kupata heshima ya kuwa mwenyeji wa maonyesho hayo yanayoratibiwa na sido Kanda ya Mashariki.

Katika maonyesho hayo wajasiriamali zaidi ya 280 kutoka mikoa ya kanda hiyo ikiwemo Pwani, Morogoro, Lindi, Dar es salaam na Mtwara wanategemewa kushiriki.

Alisema shughuli hiyo itafanyika katika uwanja wa CCM, Mwanakalenge karibu na chuo cha sanaa, Bagamoyo (TASUBA).

Aidha alieleza mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa maonyesho anatarajiwa kuwa waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, Charles Mwijage (mb).

"Kauli mbiu ya maonyesho ya mwaka huu ni uchumi wa viwanda unategemea viwanda vidogo ambapo maadhimisho ya maonyesho haya nitafunga mimi mkuu wa mkoa "alifafanua mkuu huyo wa mkoa.

Mhandisi Ndikilo alisema endapo fursa hiyo itatumika ipasavyo itasaidia wajasiriamali hususan wa vijijin lakini na wa mjini kutangaza bidhaa zao.

Hata hivyo alielezea kuwa maonyesho hayo yatawawezesha kuwakutanisha wazalishaji wa bidhaa mbalimbali ili waweze kubadilishana uzoefu wa kiufundi, masoko na ubora wa bidhaa.

Mhandisi Ndikilo alisema  wafanyabiashara hao watakuza ubora wa bidhaa, kupata mbinu za ushindani, kuwajengea uwezo wajasiriamali kujiamini na kuona wanaweza kuuza bidhaa.

Madhumuni mengine ni kupata mafunzo yanayoandaliwa na sido kabla ya maonyesho na maandalizi kwa ajili ya soko la Afrika mashariki na utandawazi.

Mhandisi Ndikilo, alifafanua kuwa wananchi na viongozi pia wataweza kuona bidhaa zinazozalishwa na kutambua uwezo wa wajasiriamali husika.

Alisema wilaya ya Bagamoyo ni wilaya ya kiutalii, ipo shwariiii na hatua stahiki za kiusalama zitachukuliwa ili kuhakikisha wageni na wajasiriamali wanakuwa salama.

Meneja wa sido mkoani Pwani, Agnes Yesaya alitaja bidhaa zinazotarajiwa kuonyeshwa ni pamoja na mashine mbalimbali za uzalishaji bidhaa zilizosindikwa.

Bidhaa nyingine ni zile zinazotokana na kazi mbalimbali za mikono, sabuni, bidhaa za ngozi, bidhaa mchanganyiko zinazotoka kwenye mikoa na kanda nyingine.

Agnes alisema taasisi za serikali na binafsi ikiwemo shirika la viwango (TBS), bodi ya biashara za nje (BET)nazo zitakuwepo kwa ajili ya uhamasishaji wa wajasiriamali kuhusu viwango na ubora na namna ya kuuza bidhaa nje ya nchi.

Serikali mkoa wa Pwani na sido mkoa, walitoa wito kwa pamoja kuiomba jamii na wadau wa kibiashara kujitokeza kufika Bagamoyo kuona na kununua bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

"Watanzania wabadilike kwa kupigania na kununua bidhaa zinazotokana na ubunifu na mikono ya watanzania wenzao"walisema.

Mhandisi Ndikilo na meneja wa Sido mkoa wanasema ni faraja kununua bidhaa za nchini kwani hazinatofauti na zile za nje ya nchi na zinauzwa kwa gharama nafuu.
Mwisho 
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania