CURRENT NEWS

Sunday, October 23, 2016

RC GAMBO APOKEA MSAADA WA BATI 500 NA MIFUKO YA SARUJI 500

Mkuu wa Mkoa Mrisho Gambo akipokea msaada wa mabati na saruji kutoka kwa  Meneja Mradi wa Kampuni ya ujenzi ya Hanil - Jiangsu Joint Venture Ltd, inayojenga barabara ya Sakina - Tengeru, Km 14.1 na barabara ya Mchepuko yenye Km 42.4. 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Gambo akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Dararro mifuko 100 ya saruji na mabati 100  kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kinachojengwa eneo la "kwa mama mbauda

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Gambo akimshukuru Meneja Mradi wa Kampuni ya ujenzi ya Hanil - Jiangsu Joint Venture Ltd, inayojenga barabara ya Sakina - Tengeru, Km 14.1 na barabara ya Mchepuko yenye Km 42.4. 

Nteghenjwa Hosseah - Arusha

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amepokea msaada wa bati 500 pamoja na mifuko ya saruji 500 kwa ajili ya kuwezesha huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati pamoja na shule za msingi na sekondari za Mkoa wa Arusha.

Mara baada ya kukabidhiwa wa msaada huo nje ya jengo la Ofisi ya Mkuu huyo, Gambo alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Dararro mifuko 100 ya saruji na mabati 100  kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kinachojengwa eneo la "kwa mama mbauda" kata ya Muriet Jijini Arusha.

Alisema msaada huo utawezesha kila wilaya kunufaika nao kwani kila wilaya za mkoa wa Arusha kuna changamoto za uhaba wa vyumba vya madarasa pamoja na mahitaji ya majengo ya zahanati ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Alimshukuru Meneja Mradi wa Kampuni ya ujenzi ya Hanil - Jiangsu Joint Venture Ltd, inayojenga barabara ya Sakina - Tengeru, Km 14.1 na barabara ya Mchepuko yenye Km 42.4. 

Xie Jianbao wametoa msaada huo kama sehemu ya kurudhisha kwa jamii ya watanzania ili kukuza mahusiano na kujali jamii na Taifa ambalo limewapa kazi hiyo kubwa ya ujenzi wa barabara zitakazogharimu takribani Bil. 139.

"Naishukuru kampuni hii kwa kutoa msaada huo kwa ajili ya kuleta maendeleo na naahidi tutautumia ipasavyo katika kuleta maendeleo na kila wilaya nitakayofanya ziara." Alisema  Mkuu wa Mkoa na kuongeza, "msaada huu nitaupeleka katika wilaya zote ili kupunguza changamoto mbalimbali kwa jamii yetu ya Arusha".

Naye Meneja Mradi wa kampuni hiyo, Bw. Xie alisema kampuni yao imeona umuhimu wa kuchangia jamii kwani wao ni wajenzi wa barabara na wanastahili kurejesha faida kwa jamii inayowazunguka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Gabriel Daqarro alimshukuru Gambo kwa msaada huo na kusisitiza kuwa mifuko hiyo 100 ya saruji pamoja na bati 100 zitasaidia ujenzi wa kituo cha afya kinachojengwa Kata ya Muriet Jijini Arusha.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia alishukuru kwa msaada huo utakaosaidia ujenzi wa kituo cha afya kujengwa na kukamilika ndani ya miezi miwili na kuahidi kwamba atasimamia ipasavyo ili kuhakikisha Kituo kinajengwa katia ubora unaostahili.

Katika  makabidhiano hayo yaliyohudhuriwa na wabunge wa Viti maalum wanawake Mkoa wa Arusha, Catherine Magige na Aminah Mollel, walitoa rai kwa nyakati tofauti kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kumuunga mkono Mhe. Gambo pamoja na Serikali ili kuwezesha maendeleo kusonga mbele.

"Kokote alikopita Gambo, kumepiga hatua kubwa ya maendeleo. Ni kiongozi mwana maendeleo. Anastahili kuungwa mkono ili wananchi wetu wapige hatua kubwa ya maendeleo," walisema.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania