CURRENT NEWS

Wednesday, October 12, 2016

RPC MUSHONGI-STOP KUFUNGA BARABARA /KUPIGA VIBIRITI MAGARI


Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali mjini Chalinze ,wajitokeza kwenye maandamano kuungana na kikosi cha usalama barabarani mkoani Pwani,kwenye uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani,yaliyofanyika
viwanja vya polisi Chalinze.

Baadhi ya madereva pikipiki Chalinze ,wajitokeza kwenye maandamano kuungana na kikosi cha usalama barabarani mkoani Pwani,kwenye uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani,yaliyofanyika viwanja vya polisi Chalinze

Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Boniventure Mushongi,akizungumza katika uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani,mkoani humo,yaliyofanyika
viwanja vya polisi Chalinze.

Katibu wa kamati ya usalama barabarani ambae pia ni kamanda wa kikosi hicho mkoani Pwani,Abdi Issango,(aliyeshikiwa mic)akizungumza katika uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani,mkoani humo,yaliyofanyika
viwanja vya polisi Chalinze(Picha na Mwamvua Mwinyi)Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

KAMANDA wa polisi mkoani Pwani ,Boniventure Mushongi,ameiasa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi ikiwemo kufunga barabara ama kupiga vibiriti magari kwani kwa kufanya hivyo ni uvunjifu wa amani.

Aidha amewataka madereva pikipiki(bodaboda)kuacha mbwembwe wawapo barabarani na  kutumia vilevi ili kuepukana na ajali zembe.

Aliyasema hayo katika uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoani Pwani,yaliyofanyika viwanja vya polisi Chalinze.

Kamanda Mushongi alisema kwasasa wataendelea kuwa wakali kudhibiti vitendo mbalimbali vinavyoashiria uvunjifu wa amani na kudhibiti ajali hususan barabara kuu.

Alisema ifikie wakati sasa watu kufuata sheria badala ya kupelekea madhara kwa wengine wasio na hatia.

Alieleza kuwa hivi karibuni kuliwahi kutokea matukio yaliyohusisha wananchi kufunga  barabara kwa masaa kadhaa,ikiwemo WAMI wakidai polisi haina ushirikianao nao hali iliyosababisha kero kwa madereva na wasafiri waendao mikoani.

Kamanda Mushongi alisema endapo kuna mtu ataona hatendewi haki achukue hatua za kisheria na sio kubughudhi watu wengine.

“Askari mmoja anahudumia watu 1,500 unategemea wakati wewe umekutwa na tatizo muda huo kuna wengine wangapi wanakuwa na tatizo kama wewe”

“Ifikie hatua ya kuoneana huruma na kujali kazi za mwingine kwani ukiambiwa atashughulikia suala lako ni kwamba inahitaji muda ili kila mmoja apate huduma stahiki”alisema kamanda Mushongi.

Alieleza kwamba jeshi la polisi lipo pamoja na watu ili kuhakikisha wanalinda usalama wa raia na mali zao na kuwasaidia pale panapohitajika .

Akizungumzia suala la madereva bodaboda kupata ajali alisema serikali iliruhusu pikipiki kutumika kama chombo cha usafiri rahisi nchini  na kuwatengenezea ajira vijana wasio na ajira.

Kamanda mushongi alisema lakini waendesha pikipiki wengi wamevamia biashara hiyo bila kuwa na mafunzo ya kuendesha hivyo imekuwa janga la taifa kwa kupata ajali nyingi za vifo na majeruhi.

“Tunapoteza nguvu kazi kubwa  kwa vijana hawa kufanya mzaha wawapo barabarani wengi wao wamevamia tuu fani hii,hawana mafunzo ya udereva.

Kamanda huyo aliiomba kamati ya usalama barabarani mkoani humo kutoa elimu za kutosha kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuchoma magari na kufunga njia ovyo.

Hata hivyo aliitaka kamati hiyo kuendelea kutoa mafunzo kwa madereva bodaboda ili kuondokana na ajali za mara kwa mara.

Nae katibu wa usalama barabarani mkoani hapo,Abdi Issango ambae pia ni kamanda wa usalama barabarani mkoa,alieleza kuwa watu 165 wamekufa kutokana na ajali za barabarani zilizotokea katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2016.

Isango alisema vifo hivyo ni pungufu ya watu 18 ikilinganishwa na vifo vya ajali katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2015.

“Vifo hivyo vimetokana na ajali 376 ambazo ni pungufu kwa asilimia 6 huku watu 402 walijeruhiwa na kuwa na upungufu ya watu 235 na vifo vilikuwa 148 ongezeko ikiwa ni 10
katika kipindi cha mwaka 2015,”

“Madereva waliokufa walikuwa 27 ikiwa ni ongezeko la madereva 14 ikilinganishwa na waliokufa kipindi kama hicho walikuwa 13 ongezeko likiwa ni asilimia 107.6 ,abiria waliokufa walikuwa 36 pungufu ikiwa ni vifo 39 sawa na asilimia 52 wapanda baiskeli vifo vilikuwa 13 ongezeko la vifo 11,” alisema Issango.

Issango alisema Pwani ni moja ya mikoa yenye ajali nyingi za barabarani hapa nchini kutokana na Jiografia kwani magari yote yatokayo Dar es Salaam kwenda mikoani na nchi jirani kwenda Jijini Dar es Salaam.

Akielezea changamoto ya barabara kuu ya Dar es salaam-Chalinze aliiomba serikali kuipanua barabara hiyo ambayo ni finyu kwani wakati mwingine barabara ufunga na kusababisha foleni na ajali.

Alitaja tatizo jingine ni ukosefu wa breakdown ya serikali hasa barabara ya Dar es salaam /Chalinze hivyo kunapotokea ajali basi trafik hupata shida kuyatoa.

Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo Injinia Michael Mrema ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema suala la ukosefu wa breakdown na ufinyu wa barabara atalifikisha kwa mkuu wa mkoa  kwa hatua zaidi.

Alisema awali kulikuwa na tatizo la mabonde na barabara kuwa mbaya eneo la mlandizi hadi Chalinze lakini wakala wa barabara TANROADS imelitatua tatizo hilo.

Mrema alisema kwasasa serikali inaendelea na mipango mingine ya kuboresha na kujenga barabara na kupanua ikiwemo barabara hiyo ambayo inatarajiwa kuwa barabara ya njia sita miaka ijayo.

Alikipongeza kikosi cha usalama barabarani kwa kuendelea kukabiliana na makosa ya usalama barabarani kwa lengo la kupunguza ajali ambapo alikitaka kuendelee kufanya kazi kwa juhudi ili kuondoa tatizo hilo.

Mwisho.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania