CURRENT NEWS

Sunday, October 23, 2016

SERIKALI MKOANI PWANI YAONGEZA MIEZI MITATU KUWABOMOLEA WALIO NDANI YA HIFADHI YA BARABARA NDANI YA MITA 60


Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

SERIKALI mkoani Pwani ,imewaongezea muda wafanyabiashara na wananchi waliojenga kwenye eneo la hifadhi ya barabara kuu ya Dar es salaam –Morogoro waliotakiwa kubomolewa novemba 23 mwaka huu badala yake itakuwa January  2017.

Zoezi hilo lilikuwa likihusisha walioingia ndani ya barabara hiyo kuanzia eneo la Kiluvya-Tamco na soko la Mailmoja ambapo wameongezewa miezi mitatu kutokana na soko jipya kuchelewa kujengwa chini ya halmashauri ya Kibaha Mji.

Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara hao na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Bwawani Kibaha.
Aliwataka wahusika hao kuanza kubomoa na kuhama kwa hiari ,ndani ya kipindi hicho kilichoongezwa kabla ya january 23 mwakani .
Hata hivyo mhandisi Ndikilo,alieleza kuwa wafanyabiashara hao hawataondolewa hadi halmashauri ya Mji wa Kibaha itakapojenga soko jingine.
“Maandalizi ya kuhamia kwenye soko jipya hayajakamilika na hakuna chochote kilichojengwa ambapo ni miezi miwili imepita toka TANROADS walipotoa notisi kwa waliojenga kwenye hifadhi hiyo kuondoka likiwemo na soko hilo”


“Maelekezo yametolewa na waziri wa ujenzi ,uchukuzi na mawasiliano kwamba zoezi la bomoabomoa ni mita 60 na siyo mita 120 kama ilivyoonyesha na kutangazwa na wakala wa barabara Tanzania (TANROADS)mkoa wa Pwani,”alisema mhandisi Ndikilo.


Mhandisi Ndikilo alisema  mkurugenzi Jeniffer Omolo kasema mkandarasi kapatikana hivyo namtaka ajenge soko ndani ya siku 30 ili ibakie kujenga vizimba na ujenzi uanze kuanzia wiki ijayo ili wafanyabiashara wapate eneo lao la kufanyia biashara zao.
Alisema ujenzi wa soko utafanyika kwenye eneo la Mnarani maarufu kama Sagulasagula ama Loliondo na wanatarajia kutakuwa na huduma muhimu ikiwemo maji na huduma nyingine zitapatikana.
Alifafanua muda uliopangwa wa miezi mitatu sawa na siku 90 vitu vyote viwe vimekamilika kwani hakutoongezwa muda mwingine hivyo wale waliojenga kwenye eneo ambalo ni hifadhi ya barabara ndani ya mita 60 waanze kuvunja wenyewe bila kusubiri kushurutishwa.
Mhandisi Ndikilo anasema  walionunua kwenye eneo la kitovu cha Mji wanapaswa kujenga haraka.Huu ni wakati wa jamii kukubali mabadiliko hayo ambayo yapo ndani ya sheria ili mji wa Kibaha uweze kuwa katika mpangilio mzuri.


"Lengo letu ni halmashauri ya Mji kuwa manispaa hivyo moja ya vigezo ni kupanga Mji huu ,wananchi watuelewe na wote tunahitaji kupanga Mji wetu alisisitiza .


Nae mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoa wa Pwani ,Abdallah Ndauka alimshukuru mkuu wa mkoa kwa kutoa muda huo ili kutekelezwa agizo hilo na halmashauri.
Ndauka alisema kuwa utekelezaji wa ujenzi wa soko hilo umechukua muda mrefu kutokana na baadhi ya watendaji kutowajibika ipasavyo na kusababisha mipango mingi kushindwa kukamilika.
Awali mkurugenzi wa mji wa Kibaha Jeniffer Omolo , alikuwa na wakati mgumu baada ya wafanyabiashara kuinua mabango wakitaka mkurugenzi huyo atumbuliwe ama mkuu wa mkoa wa Pwani aondoke nae wakidai ameshindwa kuwajibika .


Kufuatia hali hiyo mhandisi Ndikilo ,alisema anatoa muda wa miezi mitatu kuitisha mkutano mbele ya wananchi ambao watapiga kura endapo kutakuwa na mtendaji ambae ni kero

na ataondoka nae.

Alisema serikali ya sasa si ya kubembelezana kwani inahitaji watumishi wa umma  wanaowatumikia wananchi badala ya kufanya kazi kwa mazoea.


Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha Jennifer alieleza  kwamba mchoro wa soko ulizinduliwa tangu mwaka 2014 .
Alisema tatizo kubwa ni uhaba wa fedha licha ya mpango uliopo ni kumaliza ujenzi  mapema iwezekanavyo.
Jennifer alisema  soko kwa sasa litahamia eneo la Sagulasagula na fedha zipo na tangazo la kumpata mkandarasi limeshatoka.


Alisema endapo zoezi la bomoa bomoa litafanyika itawasaidia halmashauri kupanga Mji na kuwa na kujenga mabanda ya kupumzikia abiria eneo la stend ya sasa.

Kwa mujibu wa Tanroads mkoani Pwani,awali zoezi hilo lilikuwa lifanyike mwezi agost lakini muda uliongezwa hadi mwezi novemba na kudai wapo watu wengine walishawekewa alama ya X tangu mwaka 2004 .


“Sheria ya barabara ya mwaka 1932 na kufanyiwa marekebisho 1958 kifunga na 52 na marekebisho ya sheria ya barabara na 13 ya mwaka 2007 “
Taratibu za sheria za usimamizi wa barabara kifunga na 30 (b) eneo la hifadhi ya barabara,mita 120 sawa na futi 400 kwenda kila upande kutoka katikati ya barabara ni marufuku kufanya maendelezo yoyote katika eneo hilo.
Mwisho. 
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania