CURRENT NEWS

Saturday, October 1, 2016

SMMRP YAENDELEA KUBORESHA MAJENGO OFISI ZA MADINI

Taswira ya mbele ya mwonekano ya jengo la ofisi ya madini kanda ya kusini mkoani Mtwara.
 Mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Malcom Investment Co Ltd (mwenye tshirt ya bluu) waliojenga jengo hilo, akikabidhi ufunguo kwa Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali watu wa Wizara ya Nishati na Madini Bibi Joyceline Lugora (katikati) wakati wa kukabidhi jengo hilo kwa kanda ya madini kusini mkoani Mtwara hivi karibuni.
 Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (aliyeshika ufunguo) baada ya kupokea kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali watu wa Wizara ya Nishati na Madini, Joyceline Lugora (katikati) tayari kuanza kulitumia jengo hilo kabla ya kuzinduliwa rasmi hivi karibuni.
 Msanifu Majengo wa SMMRP, Joseph Ringo,( mwenye shati nyeusi) akijaribu moja ya kifaa kinachotoa sauti kuashiria hatari pindi hitilafu au dharura ya moto itakapotokea katika jengo
 Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka,(kulia) akifungua mlango kukagua baadhi ya vyumba katika jengo hilo wakati wa makabidhiano hayo.

Taswira ya mbele ya mwonekano ya jengo la ofisi ya madini kanda ya kusini mkoani Mtwara.

Zuena Msuya, Mtwara

Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ulio chini ya Wizara ya Nishati na Madini, umekabidhi Jengo la kisasa kwa Kanda ya Madini Kusini ambalo linatarajiwa kurahasisha utendaji kazi kwa kutumia mfumo wa teknolojia ya kisasa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi jengo hilo mkoani Mtwara hivi karibuni, Msanifu Majengo wa SMMRP, Joseph Ringo alisema kuwa, ujenzi wa jengo hilo umefadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia mradi huo kwa lengo la kuboresha Sekta ya Madini nchini.

Ringo alisema kuwa, jengo hilo ambalo litatumika kama kituo cha Kisasa cha Madini (Center for Excellence) limeunganishwa katika mfumo wa kisasa wa TEHAMA kwa kuhifadhi taarifa pamoja na kumbukumbu mbalimbali za kidijitali za madini za Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake na endapo itatokea tatizo katika mfumo huo itakuwa ni rahisi kupatikana.

Alifafanua kuwa, jengo hilo limeunganishwa na mfumo wa kisasa wa TEHAMA, Ofisi za watendaji wa wizara, maktaba ya kisasa ya kuhifadhia taarifa za madini yanayopatikana katika ukanda wa kusini pamoja na uwepo wa vyumba maalumu vyenye vifaa kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa wachimbaji wa madini.

Aidha, Ringo alifafanua kuwa, mradi wa SMMRP umelenga katika kuboresha miundombinu hasa ya majengo kwa kuweka mifumo ya kisasa pamoja na kuimarisha shughuli za rasilimali madini katika Ofisi za Kanda na Mikoa nchini.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka alisema kuwa hivi sasa jengo hilo litawasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi kwakuwa lina uwezo wa kukidhi miundombinu yote ya wafanyakazi.

Vilevile, amewataka wafanyakazi watakaokuwa wakitumia jengo hilo kuitunza na kulinda miundombinu ya jengo hilo.
Jengo hilo limebuniwa na Kampuni ya OGM Architects Consultants na kujengwa na kampuni ya ukandarasi ya Malcom Investment Co Ltd.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania