CURRENT NEWS

Tuesday, November 8, 2016

DC MWANGA AANZA KUELEKEZA NGUVU ZAKE KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA MADARASA

VIONGOZI mbalimbali wakionekana kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Kibindu Chalinze wilayani Bagamoyo,katika ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya msingi Kibindu ,akiwemo mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alhaj Majid Mwanga na kamanda wa polisi mkoani Pwani Boniventure Mushongi.(Picha zote na Mwamvua Mwinyi) 

Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
SERIKALI wilayani Bagamoyo,mkoani Pwani,imeanza kuelekeza nguvu zake katika kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi na sekondari wilayani humo baada ya kukamilisha zoezi la madawati.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,alhaj Majid Mwanga ,aliyasema hayo wakati baadhi ya viongozi wa wilaya walipoweka kambi katika shule ya msingi Kibindu ,jimbo la Chalinze,kushirikiana na wananchi kwenye ujenzi wa madarasa mawili.
Alisema zoezi hilo ni la kata zote zilizopo wilayani Bagamoyo lengo ni kuhakikisha wanamaliza tatizo la upungufu wa madarasa lililopo kwasasa.
Alhaj Mwanga alisema lengo jingine ni kuhakikisha wanafunzi wanaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza na wanaoandikishwa darasa la kwanza mwakani wasikose madarasa ya kusomea.
Aidha alieleza kuwa kila kata sasa hivi ina siku yake maalum ya kujitolea kufanya shughuli za serikali nje ya siku ya kufanya usafi.
"Tunachokifanya kwasasa ni kuhakikisha tunamaliza tatizo la madarasa wilayani Bagamoyo,haiwezekani wanafunzi wakasoma kwenye mazingira yasiyo bora hata kidogo,kwa pamoja tutaweza kuboresha sekta ya elimu”alisema alhaj Mwanga.
Alhaj Mwanga aliomba wananchi wawaunge mkono kumaliza adha ya uhaba wa majengo hasa ya madarasa na vyoo katika shule za msingi na sekondari.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,alifika katika shule hiyo kutembelea kujua namna ujenzi unavyoendelea na kushirikiana na wananchi katika ujenzi huo.
Mkuu huyo wa mkoa alimpongeza mkuu wa wilaya hiyo kwa hatua ya kuhamasisha ujenzi wa kuongeza majengo ya madarasa wilayani humo kwani ni jitihada nzuri na ya kuigwa katika wilaya nyingine.
Mhandisi Ndikilo alisema tatizo la upungufu wa madarasa wilayani hapo limebaki historia hivyo ni wakati wa kuunga mkono jitihada za mkuu wa wilaya kuelekeza nguvu katika kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa .
Alisema viongozi wanapaswa kujitoa,kuwa wabunifu badala ya kujibweteka wakisubiria kufuatwa na wananchi maofisini hali ambayo inapaswa ibadilike.
Mhandisi Ndikilo aliiomba jamii kujenga tabia ya kushirikiana na serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pasipo kuiachia serikali pekee.
Aliahidi kuendelea kutafuta wadau watakaoweza kuwezesha vifaa vya ujenzi vitakavyosaidia kumaliza ujenzi uliobakia na kukarabati baadhi ya shule zilizo kwenye zoezi lililoanzishwa na wilaya hiyo.
Diwani wa kata ya Kibindu ,Ramadhani Mkufya alisema shule ya msingi Kibindu inakabiliwa na changamoto ya madarasa lakini wanashukuru wananchi wamejitolea nguvu kazi ili kukamilisha ujenzi huo.
Mkufya alisema kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete,amesaidia mifuko ya saruji 200 na mabati 120 ambayo ndio wameanzia kazi ya ujenzi hivyo wanamshukuru kwa msaada huo.
“Shule hiI itakapomalizika itakuwa na madarasa saba ,na anaomba wadau wa elimu waweze kujitolea misaada mbalimbali ikiwemo nondo,mbao ili kumaliza tatizo la majengo katika shule zilizopo kata ya Kibindu “alielezea Mkufya.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kibindu ,Furaha Funga ,alisema mwaka 2014 baadhi ya madarasa katika shule hiyo yaliezuliwa na mvua zilizonyesha kipindi hicho.
Alisema msaada alioutoa mbunge wa jimbo la Chalinze umesaidia kuanza kwa ujenzi wa madarasa hayo ili yaweze kusaidia kuondoa adha iliyopo.
Mwalimu Funga alibainisha kwamba hivi karibuni Ridhiwani pia alitoa mabati 800 na mifuko ya saruji 1,110 vyenye thamani ya sh.26 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa madarasa ya shule za msingi za Machala,Malivundo na Kwaikonje ikiwemo Kibindu.
Alimshukuru mkuu wa wilaya alhaj Mwanga, mbunge Ridhiwani na mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Ndikilo kwa kuonyesha moyo wao wa kuhamasisha nguvu kazi na wadau.
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania