CURRENT NEWS

Thursday, November 17, 2016

HII NDIKILO-WENYEVITI NA WATENDAJI WA VIJIJI NA KATA MSIUZE ARDHI ZA VIJIJI KWA MASLAHI YENU


Na Mwamvua Mwinyi,Soga

MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amewataka baadhi ya watendaji na wenyeviti wa vijiji na kata kuacha kujihusisha na uuzaji wa ardhi za vijiji na maeneo ya wawekezaji ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima.

Aidha amesema wapo baadhi ya viongozi hao ambao wanageuza ardhi hizo kutunisha mifuko yao hali inayosababisha serikali za vijiji kukosa mapato.

Hayo aliyasema kwa wananchi wa kata ya Soga ,Kibaha Vijijini,baada ya kutembelea mipaka ya eneo la ardhi ya mwekezaji Mohammed Interprises ,ambalo lina mgogoro na wananchi hao.

Mhandisi Ndikilo,alieleza kuwa kuna taarifa kuwa wapo wenyeviti na watendaji wa vijiji wanaozuza ardhi za vijiji hekari zaidi ya 50 zinazotakiwa kisheria na kuuza hadi hekari 100-300.

Alifafanua kwamba anafanya uchunguzi na endapo yupo atakaebainika kuuza ardhi kiholela hatoweza kumvumilia na sheria itafuata mkondo wake.

Mkuu huyo wa mkoa alisema inashangaza kuona kiongozi badala ya kusimamia masuala ya serikali ndio ana kuwa chanzo cha kuchonganisha migogoro kwenye jamii.

“Kama huna doa wala makandokando yoyote fanyakazi kwa amani lakini kama ndio mmoja kati ya viongozi wanaoangalia maslahi yao pekee bila kujali wananchi na serikali itabidi atupishe”

“Wenyeviti wa vijiji,watendaji wa vijiji na kata na maafisa tarafa ndio serikali ,mnajua mengi ,simamieni masuala yaliyo chini ya serikali bila kuficha na kujihusisha na mambo yasiyo na tija kwenu’alisema mhandisi Ndikilo.

Akizungumzia kuhusu eneo la Mohammed Interprises  alisema mgogoro huo ni wa muda mrefu hivyo anaendelea kuufuatilia kwa kina na kuutafutia ufumbuzi.

Mhandisi Ndikilo alibainisha anayo taarifa kuwa kuna baadhi ya wananchi walimega upande wa eneo la mwekezaji huyo na baadhi ya wenyeviti kugeuza mtaji.

Mhandisi Ndikilo alisema hataki kuona wananchi wananyanyaswa lakini hataki pia kuona upande wowote unaonewa mwenye haki yake apewe.

Alikemea tabia ya kumega ardhi za wawekezaji wenye hati miliki halali na kuachana na kuvamia maeneo hayo kinyume na sheria.

Nae mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaa ,alisema anashirikiana vizuri na mkuu wa mkoa,wa wilaya juu ya tatizo la mwekezaji huyo na wananchi.

Alisema mgogoro huo baina ya wananchi  na Mohammed Interprises umedumu kwa zaidi ya miaka 20 sasa,inabidi umalizwe ili kila mmoja aendelee na shughuli zake za kujenga taifa.

Jumaa aliwaomba wananchi wajenge tabia ya kusikiliza viongozi na kujenga tabia ya kuepukana na migogoro inayochelewesha muda wa kufanya mambo mengine ya kimaendeleo na isiyo na manufaa.


Baadhi ya wakazi wa kata hiyo, akiwemo Hussein Maro,Ramadhani Rashid ,Iddi Muhunzi na mwenyekiti wa kijiji cha Kipangege Shomary Mwinshehe ,walisema wanaimani na serikali kuwa itaangalia suala hilo na kupata suluhisho .


Maro aliiomba serikali iangalie upya umiliki wa eneo hilo kwani lina ukubwa wa hekta 20,000 na kusababisha wananchi kupungukiwa  na maeneo ya kujishughulisha ikiwemo kilimo.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania