CURRENT NEWS

Tuesday, November 22, 2016

JUMAA ATOA VIFAA TIBA VILIVYOGHARIMU MIL.11 KATIKA KITUO CHA AFYA MLANDIZI

Mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini,mkoani Pwani Hamoud Jumaa kushoto akifungua box mojawapo lenye vifaa tiba ambavyo amevitoa kwenye kituo cha afya Mlandizi,vifaa ambavyo vimegharimu kiasi cha sh.mil 11.5,kulia ni mganga mfawidhi wa kituo hicho dokta Mpola Tamambele.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha Vijijini

MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini,mkoani Pwani,Hamoud Jumaa,ametoa msaada wa vifaa tiba na mashine za kupimia magonjwa mbalimbali ,katika kituo cha afya cha Mlandizi vilivyogharimu sh.mil 11.5.


Aidha ameelezea kuwa msaada huo utasaidia kuimarisha huduma zinazotolewa kituoni hapo na kupunguza changamoto ya upungufu wa vifaa tiba .

Jumaa aliyasema hayo wakati akimkabidhi vifaa hivyo, mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi,dokta Mpola Tamambele.

Alielezea kwamba ameguswa kutoa msaada huo baada ya kutembelea kituo hicho na kujionea changamoto kubwa ikiwemo ukosefu wa mashine za kupimia magonjwa ya kisukari,presha,vifaa tiba na viti vya kubebea wagonjwa.

Hata hivyo ,Jumaa alisema tatizo jingine lililopo kituoni humo ni ukosefu wa uzio hali inayosababisha watu kupita ndani ya kituo na kupelekea usumbufu kwa wagonjwa.

Alifafanua ,makamu wa rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kusaidia tatizo hilo lakini nae akiwa ni mbunge wa jimbo hilo anasema ataanza kuunga mkono jambo hilo.

“Uzio huo hauna gharama kubwa hivyo kwa jitihada zangu nikiwa ni mbunge wenu nitaanza na ujenzi wa uzio ili hali kuondoa tatizo hili na kuwaondolea kelele wagonjwa”alisema Jumaa.

Jumaa alisema kituo cha afya Mlandizi ni kikubwa na kinahudumia wagonjwa wengi hususan wa ajali za barabarani hivyo kinapaswa kupandishwa hadhi na kuwa hospitali ya wilaya.

Alisema suala hilo analisimamia kwa nguvu zote na limeshafikishwa wilaya,mkoa na ngazi nyingine likishughulikiwa ili adhma hiyo ifikie.


Jumaa alisema ataendelea kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo katika sekta ya afya,maji,elimu na kusaidia makundi maalum ikiwemo vijana,walemavu ,wanawake na wazee.

Alimuomba mganga mfawidhi kituoni hapo,kutunza vifaa vinavyotolewa na serikali pia wadau ambao wanashiriki kuunga mkono juhudi za serikali kukabiliana na changamoto za sekta ya afya kwani vinagharimu fedha nyingi.


Nae mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi,dokta Mpola Tamambele ,alisema vifaa hivyo  vitawezesha kuimarika kwa huduma za matibabu na kuvutia hasa akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki na kujifungulia kituoni.


Alisema awali kulikuwa na upungufu mkubwa wa vifaa tiba na mashine za kupimia magonjwa lakini kwa sasa kituo kinatoa huduma ya kupiga picha mionzi (utra sound) na kupima presha na kisukari.

Dokta Tamambele alielezea huduma zimeboreka kwasasa,akinamama wanajitokeza kwenda kliniki hadi kufikia asilimia 95 na kujifungulia kituoni.

Alisema anaimani kituo kinaelekea kuvuka matarajio ya kitaifa yanayotakiwa angalau asilimia 46 ya akinamama wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya afya na hospitalini.

Dokta Tamambele alibainisha licha ya kupokea msaada huo lakini bado wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa mashine ya kufulia suala linalowasababisha kufulia kwa kutumia mikono na uzio.


Kituo cha afya Mlandizi kinahudumia zaidi ya wagonjwa 35,000 kwa mwezi kutoka wilaya ya kibaha na maeneo jirani .

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania