CURRENT NEWS

Tuesday, November 22, 2016

KISUTU YAMUONYA LISSU, YASEMA HAIMWOGOPIHabari na Mwene Said wa Blogu ya Jamii, Dar es Salaam.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema haimuogopi kumwadhibu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na  imemuonya tabia yake ya kushindwa kufuata taratibu za kisheria anapokuwa na udhuru siku kesi yake inapopangwa kusikilizwa.

Kadhalika imesema Lissu anatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii, mshtakiwa huyo alishindwa kufika mahakamani mara tatu mfululizo kusikilizwa kesi yake na wenzake watatu dhidi ya mashtaka ya uchochezi kupitia gazeti la Mawio.

Onyo hilo lilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya mahakama yake kutoa amri ya kukamatwa Lissu Novemba 3, mwaka huu.

"Pamoja na nafasi yako uliyonayo kwa jamii lakini ujue kwamba mahakama hatukuogopi labda upande wa Jamhuri ulioshindwa kuja kukukamata ... mahakamani hakuna kuoneana bali taratibu za kisheria zinachukua mkondo wake" alisema Hakimu Simba.

ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya hakimu na Lissu:
Hakimu Simba ; Awali ulikwenda Ujerumani bila kutoa taarifa mahakamani unadhani tunakuogopa?

Lissu; Sina nia mbaya mheshimiwa hakimu nilipelekwa Ujerumani kwa dharula.

Hakimu Simba ; Je, kesi ya Uchaguzi wa Jimbo la Bunda nayo ilikuwa ni dharula?

Lissu; Mheshimiwa hakimu nilipotoka Ujerumani nilikuta kesi ya Bunda imepangwa kusikilizwa na ilikuwa na muda maalumu, niliandika barua Hakimu Mfawidhi wa mahakama hii ya Kisutu na nakala nilielekeza kwa upande wa Jamhuri sina nia ya kuidharau mahakama.
Hakimu; Kutokana na nafasi yako katika jamii ujue kwamba mahakama hatukuogopi labda upande wa Jamhuri ulioshindwa kukukamata na kukuweka chini ya ulinzi.

Kabla ya majibishano hayo, upande wa utetezi ukiongozwa na Mawakili, Peter Kibatala, John Mallya na Rwekama Rweikiza ulidai kuwa mshtakiwa wa nne Lissu, ametii amri ya mahakama amejisalimisha mwenyewe.

Kibatala alidai kuwa Lissu alikuwa na anaendesha kesi ya Uchaguzi wa Jimbo la Bunda na kwamba pamoja na kuwa mshtakiwa pia ni wakili wa kujitegemea.

Akijibu hoja za utetezi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita alidai kuwa, Lissu ni ofisa wa mahakama kama wakili na kwamba anajua taratibu za kufuata anapokuwa na udhuru wa kufika mahakamani lakini ameonyesha dharau kuondoka bila kibadi cha mahakama hiyo.

Hakimu Simba alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 20, mwaka huu na dhamana za washtakiwa wote zinaendelea.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine ni, Wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa magazeti, Ismail Mehboob.
 
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, mwaka huu,  Dar es Salaam, Lisu na wenzake  walikula njama ya kuchapisha
chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Pia Lissu na wenzake walidaiwa  Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa nia ya kuleta chuki na uchochezi  kati ya wananchi na mamlaka halali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walichapisha chapisho hilo lenye uchochezi.

Aidha, Lissu alidaiwa siku hiyo kinyume cha sheria na bila ya mamlaka waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar   wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

Washtakiwa walikana mashtaka hayo kwa nyakati tofauti.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania