CURRENT NEWS

Wednesday, November 16, 2016

MAKAMU WA RAIS AWAHAKIKISHIA WAKAZI WA MWANZA KUWA SERIKALI YA AWAMU YA TANO NI YA KUTENDA ILICHOAHIDI

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakazi wa kijiji cha Nsola ambapo alikagua miradi mbali mbali ya ufugaji samaki ikiwa sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua shamba la kilimo cha kisasa Greenhouse (Bandakitalu) la Ngongoseke lililopo kijiji cha Nsola  wilayani Magu mkoa wa Mwanza
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza kwa makini mwanafunzi Evodia Anatori wa shule ya sekondari ya kata ya Idetemya akionyesha kwa vitendo namna ya kuchanganya kemikali kwenye maabara ya shule hiyo iliyopo wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapungia wananchi wa Idetemya mara baada ya kufungua bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari ya kata ya Idetemya wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi waliojitokeza kwa wingi kumsalimia kwenye maeneo ya  Nyakato mkoani Mwanza.
                                                      ........................................................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi mkoa wa Mwanza kuimarisha maradufu doria katika Ziwa Victoria kama hatua ya kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu ambao umepunguza kwa kiasi kikubwa samaki kwenye ziwa hilo.
Makamu wa Rais ametoa maagiza hayo katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika wilaya za Kwimba, Misungwi na Magu mkoani  Mwanza katika ziara yake ya kikazi ambayo imeigia siku ya PILI mkoani humo.

Makamu wa Rais amewataka viongozi hao kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaokamatwa wakivua kwa zana haramu ua kwa sumu ili kukomesha tatizo hilo katika Ziwa Victoria.
Ameonya kuwa wavuvi haramu wakiachwa waendelee kufanya uvuvi huo wataharibu ziwa lote hasa mazalia ya samaki hali ambayo itasababisha viwanda wa kusindika samaki mkoani humo kufungwa na mamia ya watu kukosa ajira kutokana na shughuli za uvuvi.

Akizindua na kuweka mawe ya msingi kweye mabweni  ya wanafunzi wasichana katika shule za sekondari ya Idetemya wilayani Misungwi na shule ya Sekondari ya Archbishop Anthony Mayala wilayani Kwimba, Makamu wa Rais amepongeza juhudi za viongozi wa mkoa wa Mwanza na wadau wa maendeleo kwa kujenga mabweni hayo ambayo yatasaidia wasichana kuondokana na mazingira hatarishi ikiwemo kupata mimba.

Makamu wa Rais amewaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuweka mikakati madhubuti ya kujenga mabweni ya wasichana kama hatua ya kukabiliana na tatizo la wanafunzi kupata mimba na kuacha shule.
Akisalimia mamia ya wananchi wa maeneo ya Igoma na Nyakato jijini Mwanza waliojitokeza barabarani ili kumsalimia, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi hao kuwa ahadi zote zilizotolewa na viongozi hao wakati wa kampeni zitatekelezwa ikiwemo tatizo la ajira kwa vijana.

Amewahimiza wananchi waunge mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano katika kubaini walarushwa na watendaji wanaohujumu miradi ya maendeleo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano inataka kuona rasilimali zilizopo nchini zinatumika vizuri kwa ajili ya manufaa ya wananchi wote na sio kwa idadi ya watu wachache.

Akiwa mkoani Mwanza Makamu wa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekagua,kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara na kuwaeleza mipango ya mikakati ya serikali ya awamu ya Tano ya kuwaletea wananchi hao maendeleo.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amechangia mabati 100 na mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika shule ya sekondari ya wasichana ya Archbishop Anthony Mayala wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania