CURRENT NEWS

Thursday, November 10, 2016

MAMA MKAPA:WATOTO YATIMA WAANGALIWE KWA JICHO LA TATU

Watoto wanaolelewa katika kituo cha watoto yatima  cha Kibaha Children’s village centre (KCVC)kilichopo chini ya taasisi ya mfuko wa fursa sawa kwa wote(EOTF)wakiwa wanafuatilia yaliyojiri katika hafla ya uzinduzi wa madarasa matatu na ofisi ya walimu yaliyojengwa kwa msaada wa taasisi ya kifedha ya Bayport

Mke wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa,Mama Anna Mkapa,wa pili kutoka kushoto na Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama,wa kwanza kushoto mwenye nguo za njano wakifuatilia jambo katika hafla ya uzinduzi wa madarasa matatu na ofisi ya walimu yaliyojengwa kwa msaada wa taasisi ya kifedha ya Bayport.

Mama Anna Mkapa akizungumza katika uzinduzi wa madarasa matatu na ofisi ya walimu yaliyojengwa katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Kibaha Children’s village centre (KCVC)kilichopo chini ya taasisi ya mfuko wa fursa sawa kwa wote(EOTF)yaliyojengwa kwa msaada wa taasisi ya kifedha ya Bayport  yaliyogharimu mil.250.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama akizungumza.


Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha


MKE wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa,Mama Anna Mkapa ,amesema kuna kila sababu ya wadau na jamii inayojiweza kusaidia ongezeko kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima nchini hasa kwenye sekta ya elimu.
Amesema watoto hao wanakosa haki hiyo pamoja na kuishi mitaani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo unyanyasaji ,kutelekezwa na kufiwa na wazazi.
Mama Mkapa ameeleza kwa kutambua changamoto hiyo mfuko wa fursa sawa kwa wote (EOTF)ikaamua kuwekeza kijiji cha Simbani wilayani Kibaha,mkoani Pwani kwa kuanzisha kituo cha kulelea watoto yatima ili kuwezesha watoto wa aina hiyo.
Aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa madarasa matatu na ofisi ya walimu katika kituo cha watoto yatima  cha Kibaha Children’s village centre (KCVC)kilichopo chini ya mfuko huo ambapo taasisi ya kifedha ya Bayport Tanzania imesaidia ujenzi wa majengo hayo uliogharimu sh.mil 250.
Mama Anna Mkapa alieleza,wameanzisha kituo hicho ili kupunguza makali na mateso wanayopata watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa utaratibu kupitia ustawi wa jamii.
“Katika kituo hiki kwasasa kuna watoto 16,shule hii watasoma watoto kutoka kwenye kituo hiki na wanaotoka katika maeneo jirani walio watanzania”alisema.
Alisema katika kufanikisha adhama yao ya kuwa na shule kituoni hapo ndipo walipojitokeza Bayport  kujenga madarasa matatu na ofisi kwa hatua ya kwanza.
Mama Mkapa ambae pia ni mlezi wa kituo hicho ,alisema juhudi zinaendelea huku wakihakikisha wanatunza raslimali hiyo vizuri na kuwaletea elimu bora watoto hao.
Aliishukuru taasisi hiyo kwa kujitolea kuwasaidia kwani ndoto yao ilikuwa ni kuwa na shule ili watoto wanaolelewa na kituo hicho waweze kupata elimu kituoni hapo badala ya kusoma  mbali na kituo .
Mama Mkapa alibainisha kujengewa madarasa hayo kutasaidia kuongeza idadi ya watoto ambao wanaishi kwenye mazingira magumu ili waweze kupata elimu ambayo itawasaidia katika maisha yao.
Alisema kuwa ongezeko kubwa la watoto wa mitaani limesababisha watoto hao kukosa elimu ambayo ni msingi na ufunguo wa maisha yao.

Akikabidhi majengo hayo kwa mke wa rais mstaafu Benjamin Mkapa , mkurugenzi wa Bayport John Mbaga ,alisema wameamua kufanya hivyo kwa lengo la kuisaidia jamii.
“Ni furaha kwetu Bayport kufanya kuzindua madarasa haya ikiwa ni sehemu ya sherehe ya miaka 10 tangu taasisi hii ianzishwe lengo likiwa ni kuhudumia jamii kwenye nyanja mbalimbali za kimaenedeleo ikiwemo elimu”alisema Mbaga.


Mbaga alielezea kuwa wamesema suala la asilimia kubwa ya watoto kuzagaa mitaani sio jambo jema hivyo taasisi ,wadau na watu mbalimbali kwa kushirikiana itasaidia kupunguza tatizo hilo hasa nchini Tanzania.

Nae mgeni rasmi katika hafla hiyo,mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama aliipongeza taasisi ya Bayport kwa msaada walioutoa.

Aliwaomba wajikite na maeneo mengine mkoani Pwani na Kibaha kuwezesha masuala mbalimbali mengine ikiwemo meza na viti kwa ajili ya walimu katika shule za msingi na sekondari.
Assumpter aliomba wasimamizi wa kituo hicho cha KCVC kuhakikisha wanaendesha kituo kwa madhumuni lengwa badala ya kukigeuza kitega uchumi .
Alisema wapo baadhi ya watu wanaanzisha vituo hivyo kwa ulaji pekee na kuwaachwa walwngwa ambao ni watoto wakitaabika zaidi hivyo alikemea tabia hiyo na kuwaasa isijitokeza kituoni humo.

Assumpter alisema mfuko wa fursa sawa kwa wote umesaidia serikali kupata suluhu ya watoto wa mitaani na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu hivyo serikali itakuwa bega kwa bega nao katika kila hatua.Mwisho.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania