CURRENT NEWS

Wednesday, November 23, 2016

MCHENGRWA AWATULIZA WANANCHI WAKE NI BAADA YA SAKATA LA MAUAJI YA WATU WAWILI


Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mohamed Mchengrwa akizungumza na umati wa wananchi wa kijiji cha Kilimani Kata ya Ngorongo Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, katika mkutano maalumu wa dharula kwa ajili ya kurudisha hali ya amani na utulivu baada ya kutokea kwa watu wawili kupoteza maisha kufuatai mapigano ya wakulima na wafugaji.

NA VICTOR MASANGU, RUFIJI

WATU wawili wamepoteza maisha baada ya kutokea  kwa vurugu kubwa na kusababisha mapigano baina ya jamii ya wafugaji na wakulima katika kijiji cha Kilimani kata ya Ngorongo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani baada ya wafugaji hao kuamua kuingiza ng’ombe zao kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa katika mashamba na kufanya uharibufu wa mazao.

Katika matukio hayo mawili ya mauaji ya kusikitisha  imeelezwa kuwa yametokea juzi majira ya saa 2:30 za asubuhi  baada ya mkulima mmoja aliyetambulika kwa jina la Mwidini Mpange (23)pamoja na Jugi Bushini (23) ambaye ni mfugaji walipoteza maisha kutokana na kuibuka kwa mapigano hayo ambayo yaliweza kuleta hali ya taharuki na hofu kubwa  na uvunjifu wa amani kwa wananchi  wa eneo hilo.

Kufuatia kutokea kwa mauaji hayo Tanzania daima  imeweza kufika katika eneo la kijiji hicho na kuzungumza na Baba mdogo wa marehemu ambaye ni mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Omary Mpange  ambapo amesema mwanaye alipatwa na umauti baada kundi la wafugaji jamii ya wasukuma zaidi ya 50  waliamua kumvamia na kumshambulia kwa mikuki,masime pamoja na mapanga kisha kwenda kumtupa mashambani.

Mpange alisema kwamba sababu kubwa ya mauaji hayo ni kutokana na wafugaji hao kuingiza mifugo yao katika shamba lake ndipo walipoamua kuwakamata ng’ombe hao ili hatua nyingine za kisheria zimewe kuchukuliwa lakini wafugaji hao waliweza kuamua kufanya kitendo cha kumvamia motto wake na kumuuwa.

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji hicho cha kilimani akiwemo Bashiri Mkwiku, ,Said Athuman pamoja na Zainabu Salumu amesema kuwa tukio hilo la mauaji  ya kikatili kwa upande wao  limewasikitisha sana na kuiomba serikali kuingilia kati sakata hilo haraka iwezekanavyo ikiwemo kuwaondoa wafugaji wote katika maeneo yao.

Wanakijiji hao wakizungumza kwa masikitiko makubwa walisema kwamba ili kuweza kuondokana na mapigano hayo serikali ya awamu ya tano inapswa kulivalia njuga suala hilo kwa kuhakikisha inawaondosha wafugaji wote ambao wamevamia maeneo na kuamua kuvunja sheria kwa kwenda kulishia mifugo yao mashambani.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Sadina Madega amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la mauaji ya kikatili ambapo amebainisha kuwa marehemu Mwidini Mpange ambaye alikuwa ni mkulima mwili wake ulikuwa na majereha makubwa katika mwili wake ikiwemo kukatwa kwa baadhi ya viungo vyake.

 Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa ambaye aliweza kwenda kuonana na wananachi wa kijiji hicho katika mkutano  wa dharula ulioandaliwa kwa lengo la kuweza kurudisha hali ya amani na utulivu kwa wananchi  amesema kuwa halmashauri  imetoa siku 30 tu kwa wafugaji wote kuiondoa mifugo yao ambayo ipo kinyume na sheria.

Mchengrwa alisema kuwa kwa sasa tatizo sugu la mifugo lililopo linachangiwa na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Rufiji kuwa na tabia ya kuendekeza masuala  la rushwa hivyo ameahidi kulivalia njuga suala hilo kwa lengo la kuweza kurudisha hali ya amani na utulivu kwa wanaanchi wake wa Rufiji.

Pia Mbunge huyo aliwaomba wananchi wake kwa sasa wasiwe na hasira ya kulipiziana kisasi na badla yake wavute subira kwani vyombo vya usilinzi na usalama kwa sasa vipo kwa ajili ya kuhakikisha hali ya amani katika maeneo mbali mbali ya Rufiji inakuwepo .

Kadhalika alibainisha kwamba katika kulitatua tatizo hilo halmashauri imeshatoa siku 30  ili wafugaji wote ambao wameingia katika maeneo ya rufiji bila ya kufuata sheria na taratibu waondoke mara moja ili wakulima waweze kuendelea na kilimo chao amabcho kinawasaidia katika kujipatia chakula.

Naye  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani  Boniventure Mushongi kwa njia ya simu  kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo amekiri kuwepo kwa mauaji hayo na hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa katika maeneo mbali mbali ya Rufiji  japo alisema kwa sasa  hakuna hata mtu mmoja  ambaye amekamatwa.

“Ni kweli mwandishi hali hiyo ipo na tukio hio limejitokeza japo kwa sasa siwezi kulizungumzia kwa undani zaidi, kwani bado tunalifuatailia kwa ukaraibu, lakini ni kweli watu wawili wamepoteza maisha katika tukio hilo,”alisema Mushongi.

SAKATA la migogoro kuwepo kwa migogoro ya siku nyingi baina ya wafugaji na wakulima katika Wilaya ya Rufiji Mkoani pwani bado linaoeneka kuwa ni kitendawili kikubwa kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la mifugo inayoingizwa kinyume cha sheria na taratibu bila ya kutengewa maeneo yao maalumu kwa ajili ya marisho ili kuepeukana na vurugu ambazo zimekuwa zikichochea kuwepo kwa uvunjifu wa amani .
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania