CURRENT NEWS

Wednesday, November 23, 2016

MSHAMA AMSWEKA NDANI KWA MASAA, MWENYEKITI WA MTAA WA MAILMOJA

Mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama akizungumza jambo na wenyeviti na watendaji wa mitaa wa mji wa Kibaha,wakati alipoitisha mkutano kuzungumza nao sambamba na kutoa maelekeo na maagizo ili kuyafanyia kazi kwenye majukumu yao .

Picha/stori na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama amelazimika kumsweka ndani kwa masaa kadhaa, mwenyekiti wa mtaa wa Mailmoja,Chichi Mkongota ,kwa kile kinachodaiwa kumdharau wakati akitoa maagizo na maelekezo kwenye kikao cha wenyeviti na watendaji wa mitaa.
Aidha amemuagiza mwenyekiti wa mtaa wa Msangani Ally Gandi,kupeleka risiti za makusanyo ya ushuru wa mtaa huo,na taarifa ya maandishi kwanini ametumia zaidi ya mil.16 kwenye ujenzi wa zahanati badala ya mil.9 halmashauri iliyoingia mkataba na mkandarasi kampuni ya Rich.
Aliyasema hayo katika mkutano aliouitisha kuzungumza na wenyeviti na watendaji wa mitaa iliyopo wilayani humo.
Assumpter alisema kwa mamlaka aliyonayo anaweza kuweka ndani mtumishi ambaye anaonekana kuvunja utaratibu na sheria za serikali za mitaa.
Alieleza kuwa Chichi ni mwenyekiti hivyo anapaswa kufuata ama kutii maagizo na maelekezo anayoyatoa mkuu yeyote wa serikali kwa maslahi ya wananchi.
Alisema alichokifanya yeye ni kutoa maagizo kwa mwenyekiti wa mtaa wa Msangani ambae ametumia fedha bila idhini ya halmashauri na kuvunja mkataba uliosainiwa.
Assumpter aliwataka viongozi wa mitaa na kata kuachana na tabia ya kuweka uchama mbele wakati kipindi cha siasa kimeisha na kilichobaki ni kuwatumika wananchi.
“Serikali iliyopo madarakani ni ya chama cha mapinduzi(CCM),hivyo iwe ni mwenyekiti wa Chadema,Cuf,Nccr Mageuzi,wa CCM ,Ukawa sijui nini, inapaswa afanyekazi kwa kufuata maagizo ya serikali na kutekeleza ilani ya CCM”
“Watu wasiweke uchama katika kutekeleza masuala ya serikali kwani kinachoelekeza sio chama bali ni serikali yake’alisema Assumpter.
Akizungumzia ubadhilifu wa fedha uliofanyika katika ujenzi wa zahanati ya mtaa wa Msangani alisema Gandi alikusanya fedha kwenye mtaa wake na kusema ni mali yao wakati zilitakiwa zipelekwe kwenye mfuko wa halmashauri.
Alisema wamevunja mkataba ambao halmashauri ya Mji waliingia na mkandarasi kampuni ya Rich kujenga zahanati ya mtaa huo.
Alielezea kwamba kitendo walichofanya ni cha kusikitisha kwani kiwango cha msingi cha mil.9 lakini wao walimkataa mkandarasi na kujenga kwa zaidi ya sh mil.16.
“Walikusanya kwenye utaratibu wa ushuru bila kupeleka fedha hizo halmashauri na kujenga kwa gharama kubwa tofauti na ilivyopangwa na halmashauri."
"Hii ni kinyume na utaratibu wa kukusanya na kutumia fedha kinyume na sheria za halmashauri , na yeye sio mkusanyaji wa kodi’alisisitiza.
Assumpter aliagiza kufika ijumaa mwenyekiti huyo apelekea  risiti za makusanyo hayo,kutumia mil.16 kinyume na sheria ,apeleke kwa maandishi nani alimruhusu kuvunja  mkataba uliotolewa na halmashauri na baraza la madiwani .
Ndipo Chichi alipodakia bila kuinuliwa wala kunyoosha kidole ,akimwambia mkuu wa wilaya kuwa suala hilo kwenye kata nyingi linafanyika kutumia fedha zinazokusanywa kwenye ushuru mbalimbali.
Chichi alielezea kuwa Gandi ana haki ya kupanga mipango yake ya mtaa bila kuingiliwa na mtendaji kwani na yeye ana mandet ya kuamua jambo.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha,alimuonya zaidi ya mara moja kuwa anyamaze kwani anachoagiza anamaanisha lakini Chichi alitoa sauti ya kusema haogopi kwa lolote.
Assumpter alilazimika kumuamuru polisi aliyekuwepo kwenye mkutano huo amtoe kwenye ukumbi na kumweka ndani kwa masaa ili iwe fundisho kwa viongozi wa aina hiyo.
Baadhi ya wakazi katika kata ya Msangani,akiwemo George Pascal, alisema kwasasa wanakabiliwa na tatizo la kukwama kwa miradi mbalimbali ikiwemo zahanati kutokana na siasa.


Alielezea kuwa mradi huo ulianzishwa tangu mwaka 2008 lakini bado unasuasua licha ya halmashauri kuonyesha juhudi na jitihada ya kutenga fedha kwa ajili ya zahanati hiyo.


Pascal alisema aliwaasa viongozi kuondoa misuguano ya kisiasa baina yao na badala yake wajikite kutatua kero zinazoikabili jamii ili kuinua maendeleo kwenye mtaa huo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania