CURRENT NEWS

Wednesday, November 2, 2016

MSHAMA:VIJANA WALIME/WAJISHUGHULISHE BADALA YA KUPOTEZA MUDA WAKISUBIRIA KUCHEZA POOL

MKUU wa wilaya ya Kibaha ,mkoani Pwani,Assumpter Mshama

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha ,mkoani Pwani,Assumpter Mshama ,amekemea tabia inayofanywa na baadhi ya vijana kusubiria muda wa kufunguliwa mchezo wa pool baada ya mchezo huo kupigwa marufuku kuchezwa katika muda wa kazi.
Ametoa rai kwa vijana hao kuacha kukaa vijiweni na kucheza pool bali watumie fursa mbalimbali zinazowalenga ikiwemo ujasiliamali na kilimo .
Aidha Assumpter alishangazwa kuona vijana hao wakijibweteka bila kufanya shughuli yoyote na kusubiria kucheza pool .
Hayo aliyasema wakati akizungumza na watendaji wa halmashauri ya Mji wa Kibaha na baadhi ya madiwani wa mji huo juu ya mstakabali mzima wa ukosefu wa ajira kwa vijana na namna ya kuwasaidia vijana hao.
Aliwataka vijana kuanzia sasa wajipange kwa kujiwekea mkakati wa kujiendeleza kimaisha badala ya kuamka asubuhi hadi jioni wakisubiria kucheza michezo ambayo haina tija kwao.
Hata hivyo Assumpter alieleza kuna kila sababu ya maafisa ugani kuwasaidia wananchi na makundi ya vijana ili waweze kujiingiza katika kilimo hali itakayosaidia kuondokana na maisha ya utegemezi.
“Ni wakati wa kuondokana na maisha haya wanayoenda nao,yaani vijana hawana mkakati wowote jamani,kuanzia asubuhi mtu anaamka bila kufanya shughuli hata ya kuuza juice,maji,biscuit hata kulima vijituta vya mhogo”
“Tuazimie tuu vijana hawa kila mmoja awe na tuta moja la mhogo ambalo atakuwa analima na akizalisha anauza na kujipatia fedha kuliko kukaa bure kama wanavyofanya sasa hivi”alisema mkuu huyo wa wilaya.
Alisema kuwa ifikie hatua ya halmashauri kuwezesha makundi ya vijana na wanawake katika mafungu ya fedha wanayotenga kwa ajili ya kuwakopesha bila ubaguzi hali itakayowasaidia hasa vijana kupata mtaji.
Assumpter aliomba madiwani hao kuazimia kwa pamoja kuhusiana na mkakati huo kwa lengo la kupunguza makali ya maisha wanayoishi vijana wa Kibaha .
“Eti wanasubiria kucheza pool ,wanakaa asubuhi hadi saa 9.55 jioni,halafu wanaanza kushangilia eti muda (fungulia mbwa)hee,hii sio hali nzuri .Hali hii inazalisha wezi,wavuta bangi na watoto wasio na maadili kutokana na kwamba hawana kitu cha kufanya”aliongezea Assumpter.
Assumpter aliwaasa vijana kijumla wilayani humo kuachana na tabia ya kukaa bila kujishughulisha na kuepukana na maadili yasiyo mema jambo linalowasababisha kujiingiza katika uhalifu mbalimbali.
Alisema ni wakati wa kufanya mabadiliko kwa kundi la vijana ,kwa kujenga tabia ya kujiajili wenyewe ,pasipo kutegemea kuajiliwa maofisini jambo ambalo linawachelewesha kimaendeleo.
Nae diwani viti maalum Elina Mgonja ,aliwataka vijana wajitambue na kuacha kutumiwa kama ngazi na baadhi ya watu kwa ajili ya maslahi yao binafsi na badala yake wajikite kwenye shughuli ndogondogo za kujiongezea kipato.
Anasema vijana wabadilike kwa kuchangamkia fursa zilizopo sanjali na kujiajiri ili hali kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Elina Mgonja alibainisha  ipo tabia kwa baadhi ya vijana ambao hushawishiwa kujiingiza kwenye mambo yasiyo na tija katika maisha yao kuliko kuwashawishi kuwajengea uwezo wa kuinua uchumi wao kimaisha.
Anaeleza  vijana hao wajitambue kwa kutumia fursa chache zilizopo ikiwemo kuanzisha vikundi vya kiujasiliamali,kutumia mafungu ya fedha zinazotengwa na halmashauri,licha kuwepo changamoto za mtaji .


Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania